Na Dotto Mwaibale, Singida
KAMPUNI ya Uchimbaji Madini ya Shanta iliopo Wilaya ya Ikungi mkoani Singida imetoa zaidi ya Sh.200 Milioni kwa ajili ya kusaidia miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani humo.
Hayo yalifahamika jana katika Sherehe za maadhimisho ya miaka 45 tangu kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) yaliyofanyika Kata ya Mang'onyi wilayani Ikungi mkoani Singida jana wakati wa kukabidhi miradi hiyo kwa Serikali.
Akizungumza wakati akitoa taarifa hiyo Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni hiyo Mhandisi Kundaeli Ntiro alisema fedha hizo zilitumika kusaidia miradi hiyo kwa mwaka 2020/2021.
Aliitaja miradi waliyoikabidhi kuwa ni ya elimu ambapo wamejenga madarasa mawili ya Shule ya Msingi Mlumbi, ujenzi wa madarasa mawili mawili na ofisi Shule Shikizi namba 7, kuweka sakafu madarasa mawili ya zamani Shule Shikizi namba 7 na kuweka sakafu darasa moja la zamani na ofisi Shule ya Msingi Mlumbi.
Alitaja mradi mwingine kuwa ni ujenzi wa vyoo kwa shule zote mbili ambao unatarajiwa kukamilika ndani ya mwezi Februari na kuwa ujenzi huo umezingatia umuhimu wa makundi yote kulingana na mwongozo, michoro na kuelekezwa kutoka kwa Mhandisi wa wilaya hiyo.
Akizungumzia miradi ya Afya alisema wamefanya ukarabati wa Zahanati ya Kata ya Mang'onyi kwa kujenga uzio kwenye tanuru la kuchomea taka, kuweka miundombini ya TEHAMA kwenye jengo la Zahanati hiyo ili kuunganishwa kwenye mfumo wa afya wa Serikali sambamba na kutoa vifaa kompyuta tatu na printa moja.
Alitaja kazi nyingine walioifanya kukarabati wa chumba cha maabara, kujenga ukuta wa kuzuia maji ya mvua na kumwaga zege sehemu ya kuingilia zahanati na ujenzi wa mabenchi manne ya zege ya kupumzikia wagonjwa ambao ujenzi wake unaendelea.
Katika mradi wa maji alisema kampuni imetandaza mtandao wa mabomba wenye urefu wa kilometa 4.6 na kujenga vituo vitatu vya kuchotea maji kwa ajili ya wananchi wa vijiji vya Mang’onyi na Mlumbi wanaoishi kandokando ya bomba kuu linalopeleka maji mgodini.
Kwa upande wa barabara alisema kampuni imesaidia kutengeneza barabara kwenda Mlumbi shuleni kutoka Kisima Namba 08 yenye urefu wa kilometa tatu na barabara ya kwenda Mwau Sekondari kutokea barabara kubwa yenye urefu wa kilometa moja.
Alisema kazi zote za ujenzi zilifanyika kwa kutumia mafundi na wasaidizi kutoka katika maeneo yanayozunguka miradi iliyoorodheshwa na kuwa jumla ya kiasi cha fedha ambayo imetumika kwenye huduma za jamii na mahusiano ya serikali kwa mwaka 2021 ni Sh.235,495,327.00.
Akipokea miradi hiyo Mkuu wa Wilaya ya Ikungi Jerry Muro aliishukuru Kampuni hiyo kwa kuunga mkono jitihada za Serikali za kuwaletea maendeleo wananchi wa wilaya hiyo na kuagiza itunzwe na kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wawekezaji katika wilaya hiyo.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika wilaya hiyo Mika Likapakapa aliwaambia wananchi kuondoa dhana ya kuamini maneno ya watu wasio penda maendeleo kuwa wawekezaji hao hawana tija yoyote katika wilaya hiyo na kuwa faida ya kuwepo kwao wilayani humo wanaiona na wamekuwa wakifuata sheria zote za uchimbaji na kulipa kodi.
By Mpekuzi
Post a Comment