MJINGA AKIEREVUKA MWEREVU YU MASHAKANI |Shamteeblog.


Adeladius Makwega-DODOMA.

Eneo la Mtoni Mtongani lina makaazi ya watu kadhaa masikini na wenye maisha ya kawaida mno. Eneo hilo limejaliwa kuwa na kituo kidogo cha polisi kimoja ambacho kimejengwa enzi za Augustino Mrema akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.

Eneo hilo lina makanisa kadhaa ambayo ninayakumbuka kwa wakati huo, kwanza wale Walutheri wana kanisa la muda mrefu sana ambalo ni Ushariki wa Mtoni Mtongani, wengi wao wanalitambua kama Kanisa la Kwaya ya Lulu, kwani ile kwaya iliyotunga wimbo huo miaka 1980 ilikuwa inapatikana kanisani hapo.

Kanisa Katoliki nalo lipo umbali wa dakika kama tano kwa mguu kutoka kituo cha mabasi cha Mtoni Mtongani kama unaenda mjini mkono wa kushoto unaingia kwa ndani kidogo, kwa wale wanaofahamu historia ya eneo hilo zamani Wakatoliki walikuwa wakitoka Mtongani na kwenda kusali Mbagala Misheni ndipo ilipokuwa Parokia ya Mbagala. Huku Wakristo Waanglikana walikuwa wakisali Temeke Mwisho.

Katika eneo hilo kuna misikiti mikubwa miwili, nayo ni Masjidi Al-Nuur, huu upo kando ya Barabarani ya Kilwa jirani na Stendi ya Mtoni Mtongani kuelekea mjini, msikiti huo awali ulibomolewa wakati wa kupanuliwa kwa Barabara ya Kilwa na ukalipwa na kujengwa Msikiti mpya kwa ramani ile ile ya awali ya Masjid Al-Nuur wa mwanzo jirani.

Ukiwa unaenda Mtoni Relini ukitokea stendi ya mabasi ya Mtoni Mtongani unakutana na njia inayoshuka utakutana na Msikiti wa Maboksi, hilo ni jina lililozoeleka sana.

Kwa hakika msikiti huu upo jirani na Soko la Mtoni Relini linalowahudumia wakaazi wengi wa eneo hilo, kukiwa na bidhaa kadhaa zinazopatikana kwa wingi japokuwa maeneo mengine hapa na pale yana magenge madogo madogo mengi.

Kati ya mwaka 1998-2000 nilwahi kuishi katika eneo hilo jirani na huu Msikiti. Kulikuwa na eneo ambalo CCM waliwaruhusu wadau kujenga majengo kwa mikataba na sie tulikuwa ni miongoni mwa wadau hao kukiwa na vibiashara kadhaa

Kwa kuwa biashara hizo zilikuwa jirani na Msikiti wa Maboksi, hapo palikuwa jirani mno na shekhe mmoja ambaye alikuwa akifundisha shule ya dini ya Kiisilamu akiitwa Mpembenue.

Nikiwa hapo nilijifunza wafanyabiashara wanavyofanya biashara, kila siku jioni wakipiga mahesabu na wakidamka asubuhi katika maduka ya jumla kununua bidhaa na kufungasha na kurudi nazo dukani.

Kwa wale wenye magenge nawao waliamka asubuhi na kwenda kuchukua bidhaa katika masoko makubwa huku wakifungasha mizigo na kuipakia katika gari linalokodiwa kwa pamoja na kuipeleka sokoni mapema, kukicha wateja wanakuta bidhaa na vyakula vimejaa katika maduka na meza zao tayari kuuza.

Kuhusu mazao yalikuwa yanafungashwa kutoka mikoani mathalani Shinyanga, Mbeya na Morogoro. Wafanyabiashara wakubwa wakiwamo Wapemba kutoka Zanzibar walileta mizigo alafu waliisambaza kwa wateja wao madukani kwa MALI KAULI (mkopo).

Wenye maduka hukubaliana baada ya muda fulani kulipwa pesa alafu wanaletewa mizigo mingine, hiyo ndiyo MALI KAULI.

Nikiwa hapo kuna wakati mmoja nilipata rafiki ambaye alikuwa na umri kama miaka kati ya 53-58. Mzee huyu mwanzoni alikuwa akija dukani kama mteja ambaye alikuwa akinunua bidhaa kadhaa wa kadhaa kwa malipo.

Ndugu huyu alikuwa rafiki yangu mkubwa huku tukiaminiana sana. Urafiki huo ulidumu kwa muda mrefu sana.

Kuna siku mzee huyu alinifuata akiniomba kumuhifadhia pesa zake. Nikamjibiu sawa basi ndugu huyu alikuwa kila akitoka kibaruani kwake analeta pesa namuwekea.

Zoezi hilo la kuweka pesa dukani kwangu lilifanyika kwa muda fulani, baada ya miezi kadhaa akawa sasa anakuja kuchukua pesa yake hiyo kwa matumizi na kila akija niliweka kumbukumbu za kuchukua pesa katika daftari langu la ANKARA.

Japokuwa ndugu yangu huyu alikuwa mnywaji wa pombe na kwa kuwa pesa ilikuwa ni yake mimi jukumu langu ni kumpa haki yake na kuhifadhi kumbukumbu vizuri. Binafsi nilijiuliza swali kwanini ndugu huyu pesa yake anahifadhi kwangu?

Mimi nilijiongeza kidogo kwani pesa hiyo nilikuwa naizungusha katika biashara hiyo. Huku nikiwa na fedha ya tahadhari pale akija kuchukua pesa.

Siku moja nyumbani kulikuwa na sherehe kwa hiyo duka halikufunguliwa, basi ndugu huyu alipofika dukani alinikosa, alimuona Ustadh Mpembenue na kumueleza kuwa anamtafuta yule kijana wa dukani? Aliulizwa tena akajibu kuwa yule kijana Mkristo? Akajibi Ndiyo. Kwa kuwa alikuwa amelewa kidogo ilichukua muda watu kumuelewa.

Mwalimu huyu aliongozana naye hadi kwetu, nakupiga hodi, walipokelewa na kumsikiliza ndugu huyu akaniambia kuwa nyumbani kwake ana mgonjwa kwa hiyo anaomba pesa ampeleke mgonjwa huyo hospitali.

Kweli nilichukua ufunguo wa dukani nikiambatana nao hadi dukani. Nikampa pesa yake na ndugu huyu kuondoka zake.

Mwanakwetu huyu Ustadh Mpembenue alikuwa na mdogo wake aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Ilala wakati huo. Alipoondoka nilibaki mimi na Shekhe Mpembenue tukizungumza naye, akinieleza namna alivyoongea na ndugu huyu hadi akamleta nyumbani.

Nilimuuliza Shekhe Mpembenue Je ndugu huyu alisema kwanini anahifadhi pesa dukani kwangu?

“Unajua nyumbani kwake hakutaka watambue kuwa ana fedha, pili anasema watu wanaofanya biashara za maduka wanaaminiwa sana, tatu nyumbani kwake anadai kuwa usalama ni mdogo sana na mwisho mkewe anadai kuwa ni mkorofi mno.” Aliniambia Ndugu Mpembenue.

Basi nilimaliza mazungumzo na shekhe huyu, huku akiniambia mbona mnasherehekea wenyewe sherehe hiyo? Nilimjibu kuwa pale kuna nyama na nguruwe unaiweza kuila?

Shekhe huyu alijibu na kusema ASTAGHAFIRU!

Nilirudi nyumbani kuendelea na sherehe hiyo. Nilimtafakari mzee wangu aliyekuwa anaweka pesa kwangu na uwoga wake kwa mkewe kumuona na pesa nyingi, nikasema moyoni:

“Mjinga akierevuka, mwerevu yu mashakani.”

Leo hii mwanakwetu fikiria namna ya kuaminiana huko sokoni baina ya wafanyabiashara na wafanyabiashara; wafanyabiashara na watu wanaonunua bidhaa. Je kama soko linaungua kwa moto hasara inakuwaje? Jibu lake ni hasara kubwa na kuwapeleka kundi la watu katika umasikini kufumba na kufumbua.

Mbinu ya wafanyabiashara kulinda masoko yao wenyewe ni jambo la msingi kama nilivyoshauri katika matini yangu ya MITAJI INAWATENGANISHA MADHARA YANAWAUNGANISHA.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 


 

 

 

 

 



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post