RAIS Samia Suluhu Hassan amesema amekuwa akisumbuliwa na sauti ya mtangulizi wake Hayati John Magufuli juu ya utekelezaji wa miradi aliyoianzisha. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea)
Rais Samia ametoa kauli hiyo leo tarehe 9 Februari, 2022 wakati akihutubia katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje ya jiji la Dodoma.
Barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 112.3 inajengwa katika eneo la Vyeiyula.
Rais Samia amesema mara kadhaa amekuwa akiteswa na sauti ya mtangulizi wake John Magufuli juu ya utekelezaji wa miradi iliyoanzishwa na mtangulizi wake.
“Siku kama ya leo ninapozindua miradi nimeteswa sana na sauti ya mtangulizi wangu ambaye alikuwa na maono ya kuanzisha miradi mikubwa, kuhamia makao makuu lakini hakika miradi yote nitaikamilisha.
“Nitatekeleza kikamilifu maono yote ambayo yametolewa na Baba wa Taifa ya kufikiria kuhamia Dodoma pamoja kufanya mambo yote ya kimaendeleo,” amesema.
Kwa upande mwingine Rais Samia amesema ataendelea kuzungumza na Benki ya Maendeleo ya Afrika ili izidi kutoa fedha za kukuza uchumi wa watanzania hususani akina mama na vijana.
Aidha, amesema mradi utakuwa kichocheo muhimu cha kukuza uzalishaji na usafirishaji wa mazao ya kilimo pamoja na bidhaa za viwandani.
Ameuagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroad), Mkandarasi na wasimamizi wote wa mradi huo kufanya kila jitihada kuhakikisha ujenzi huo unakamilika kwa muda uliokusudiwa.
“Mradi utatoa fursa kwa wananchi ili waweze kujiongeze kipato a kukuza maendeleo ya jiji la Dodoma na Taifa kwa ujumla.
Huu ni moja ya miradi mingi inayotekelezwa na Serikali kwa mkopo nafuu kutoka Benki ya Afrika. Kuna barabara nyingi ambazo benki imetusapoti,” amesema.
from Author
Post a Comment