RAIS SAMIA: Serikali Itajenga Stendi na Soko Lamadi |Shamteeblog.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itajenga kituo cha mabasi na soko katika mji wa Lamadi Wilayani Busega. Samia ameyasema hayo wakati akiwa njiani kuelekea mkoani Mara tarehe 04/02/2022 ambako atakuwa na ziara ya siku nne.
Akiongea na wakazi hao wa Lamadi ambao walijitokeza asubuhi na mapema kwa wingi, Rais Samia amesema suala la stendi tumelichukua na Serikali itajenga kituo cha mabasi na soko. “Nimemsikia hapa Mkuu wa Mkoa amesema kiasi cha ujenzi wa stendi ni takribani TZS bilioni 1.6, kwa kiasi hicho cha fedha Serikali hainshindwi kujenga stendi, tutajenga hiyo stendi na soko hapa Lamadi” aliongeza Mhe. Samia.
Aidha, Rais Samia ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii kuhakikisha wanatatua kero za wananchi wa Lamadi ya kuvamiwa na wanyama ikiwemo tembo na viboko. “Pamoja na juhudi mnazoendelea kufanya lakini hakikisheni mnaweka kituo cha maliasili maeneo haya ili kupunguza adha ya wanyama hatarishi kwa wananchi”, alisema Rais Samia.
Awali, Mkuu wa Mkoa wa Simiyu Mhe. David Kafulila ameweza kueleza juhudi kubwa ambazo Serikali ya awamu ya sita inazifanya katika mkoa wa Simiyu, ikiwemo uboreshwaji wa miundombinu ya barabara, shule na huduma za maji na kueleza baadhi ya kero na changamoto zinazowakabili wakazi wa Lamadi ikiwemo kutokuwepo kwa stendi na soko la uhakika ambavyo vimekuwa kero kwa wakazi hao. Kafulila amesema Simiyu imekuwa ikiendelea kwa kasi kutokana na juhudi za Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan. “Katika kipindi cha awamu ya sita mkoa wa Simiyu umepokea zaidi ya TZS bilioni 126 kwaajili ya miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wa Simiyu, aliongeza Kafulila.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Busega Simon Songe amemshukuru sana Mhe. Rais kwa kazi anayoendelea kuifanya kwani mpaka sasa mambo makubwa yamefanyika katika Wilaya ya Busega, hivyo anashukuru sana kwa maendeleo yanayoendelea kufanyika chini ya Serikali sikivu ya awamu ya sita. “Tunashukuru sana kwa fedha nyingi ikiwemo fedha za ujenzi wa madarasa 95 ambayo yamesaidia upungufu wa madarasa katika jimbo la Busega, kwani watoto wote waliofaulu kujiunga kidato cha kwanza wameanza masomo kwa pamoja, sisi wananchi wa Busega hatusemi tu kwamba unaupiga mwingi bali unaupiga mwingi sana”, aliongeza Songe.
Pamoja na hayo, Mhe. Samia Suluhu Hassan amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuri ya Wilaya ya Busega Veronica Sayore kwa kusimamia vyema ujenzi wa vyumba vya madarasa 95 yaliyojengwa chini ya mpango wa maendeleo kwa ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya UVIKO 19. “Kituo nilichotoka nimetengua wakurugenzi wanne kutokana na ubadhilifu na matumizi mabaya ya fedha, kwako sijasikia kwahiyo endelea kuchapa kazi Mkurugenzi” aliongeza Rais Samia.
Akiongelea suala la ufanyaji wa biashara ndogondogo, Rais Samia amewataka wafanyabiashara wadogo maeneo ya Lamadi na Sehemu nyinginezo kuwa wavumilivu kwani Serikali ina mpango mzuri juu yao ya kutenga maeneo ya kufanya shughuli zao za biashara. “Serikali ina mpango mzuri, tukifanikiwa Tanzania itakuwa na maeneo mengi ya kufanyia biashara kwa muda wa masaa ishirini na nne” alisema Rais Samia. Rais Samia Suluhu Hassan anaeleka mkoani Mara kwa ziara ya siku nne, pamoja na mambo mengine atashiriki kilele cha maadhimisho ya miaka 45 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambayo kitaifa yanafanyika tarehe 05/02/2022 mkoani humo.
By Author
Post a Comment