Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akijibu maswali ya wabunge, wakati wa kipindi cha maswali na majibu, Bungeni jijini Dodoma, Februari 10, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu) Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Mbunge wa Makete Festo Sanga, Bungeni jijini Dodoma, Februari 10, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri wa Katiba na Sheria Geofrey Pinda (kushoto) katikati ni Mbunge wa Viti Maalum wa Chama cha Mapinduzi Sylvia Sigula, Bungeni jijini Dodoma, Februari 10, 2022. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
***************************
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema unahitajika umakini mkubwa sana kama itaonekana kuna haja ya kuligawa Shirika la Umeme nchini (TANESCO).
“Shirika letu la umeme nchini linafanya kazi kubwa. Linazalisha, linasafirisha na linagawa umeme kwenye maeneo mbalimbali nchini. Unapotaka kufanya jukumu la aina hii inabidi tuangalie sana usalama wa Taifa letu.”
“Inabidi tuangalie kwa makini hasa katika kugawa haya makampuni ya kuzalisha, kusafirisha na kugawa umeme kwenye maeneo mbalimbali nchini. Inaweza kutokea mahali mnahitaji umeme mwingi kwa kazi fulani lakini kampuni moja ikagoma kupeleka kwa sababu zake,” amesema.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Februari 10, 2022) Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Kinondoni, Bw. Abbas Tarimba kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Bw. Tarimba aliuliza ni kwa nini Serikali haioni haja ya kuigawa TANESCO katika makampuni matatu ya kuzalisha, kusafirisha na kugawa umeme kwa vile Shirika hilo hivi sasa limelemewa na kusababisha matatizo ya umeme kila mara.
Akifafanua suala hilo, Waziri Mkuu amesema: “Kutokana na mvua zinazonyesha hivi sasa, maji yako ya kutosha na uzalishaji unaendelea, kwenye gesi uzalishaji unaendelea na hata maeneo mengine kama mafuta, uzalishaji nako pia unaendelea. Changamoto ni miundombinu iliyopo kwenye maeneo haya ya uzalishaji. Tumewapa kazi wafanye utafiti na waone nani atafanya nini.”
Akielezea kuhusu usambazaji wa umeme vijijini, Waziri Mkuu amesema mkakati wa Serikali ya awamu ya sita ni kuhakikisha inapeleka umeme kwenye vijiji vyote ifikapo Desemba, mwaka huu. “Tunataka ikifika Desemba vijiji vyote viwe na umeme na kwenye eneo la uzalishaji hatuna tatizo kwa sababu umeme utakuwepo wa kutosha,” amesema.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inaendelea kulipa mafao ya wastaafu na itahakikisha lengo la kulipa wastaafu kwa wakati linafikiwa.
“Mabadiliko ya sheria yapo na kanuni zilishatengenezwa. Kwa sasa tunaangalia kama kanuni hizi zitatuwezesha kulipa mafao ya wastaafu kwa wakati. Malengo yetu ni kulipa wastaafu wote kwa wakati na hatua hii tutaifikia,” amesisitiza.
Alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Bi. Esther Bulaya ambaye alitaka kujua ni lini Serikali itapeleka Bungeni Sheria ya Mifuko ya Jamii ili ifanyiwe tena mabadiliko na wastaafu waweze kupata amani kuhusu mafao yao na wasipate usumbufu.
Waziri Mkuu amesema mifuko hiyo ilikuwa mingi na Serikali iliamua kuiunganisha ili ibakie michache ambapo kwa sasa kuna NSSF unaoshughulika na sekta ya binafsi na PSSSF ambao unashughulika na watumishi wa umma.
Amesema baada ya kuunganisha mifuko hiyo Serikali ilikuta kunamadeni madeni mengi. “Sasa hivi tunataka tukamilishe ulipaji wa haya madeni ili tuanze kutoa mafao kwa wakati. Serikali iliwahi kutoa fedha ili kuiongezea nguvu mifuko ya hifadhi ili ikamilishe malipo yake kwa wastaafu.”
By Mpekuzi
Post a Comment