MIFUMO YA KIDIJITALI KULETA UFANISI SERIKALI, KUFANIKISHA SENSA ZIJAZO |Shamteeblog.

KUNA kila dalili Tanzania kwamba sensa ijayo ya watu na makazi itakuwa rahisi zaidi kuliko ya mwaka huu kutokana na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA).

Kasi ya ukuaji wa TEHAMA na kuchukuliwa kwake kwa matumizi ni kubwa; na kutakuwa na fursa nyingi za kiteknolojia wakati huo kuliko sasa. Hata ukilinganisha na sensa ya mwisho kufanyika nchini mwezi Agosti 2002; ya mwaka huu itakuwa na ufanisi mkubwa kutokana na teknolojia, kuanzia kwenye ukusanyaji wa data hadi kwenye uwasilishaji na uchambuzi.

Tumeona namna ambavyo madodoso ya karatasi yamebadilishwa na kuwa ya kidijitali, kwa kutumia vishkwambi. Karani wa sensa akiingiza taarifa za anayehesabiwa ni rahisi hizo kuingia kwenye mifumo ya kidijitali moja kwa moja kutoka popote alipo.

Teknolojia zilizopo ulimwenguni hivi sasa na ambazo zimeingia Tanzania, na zile zitakazojitokezwa zitakuwa zimeboreshwa. Mfano wa teknolojia zilizopo ni pamoja na zile zinazowezesha seti kubwa za data zinazoweza kuchambuliwa ili kuonyesha mwelekeo, hasa kuhusiana na vitendo vya binadamu. Hizi zinaitwa big data.

Teknolojia hii inatweza kutumia kuainisha masuala ambapo takwimu zitakusanywa takwimu wakati wa sense zijazo.

Kuna teknolojia zinazowezesha vitu kuunganishwa na kuwasiliana kwenye mtandao wa intaneti. Hivi vinaitwa internet of things, au kwa kifupi IoT. Huu ni mtandao wa vifaa na vyombo vinavyotumia mifumo ya kielektroniki kuwasiliana vyenyewe na kubadilishana data bila kumhusisha binadamu; isipokuwa tu kwenye hatua za awali za kuviwasha na kuvipa maelekezo.

Teknolojia ya IoT inatumika kwenye sekta nyingi, zikiwemo kilimo,usafirishaji na afya. Kipindi cha kuenea kwa kasi kwa homa kali ya mapafu itokanayo ya virusi vya corona – UVIKO 19, teknolojia hii ilitumika kufuatilia wagonjwa na kusambaza madawa na vifaa vingine.

Kifaa kilichofungwa kwa mgonjwa kuangalia mabadiliko yake kiafya vinaweza kuwasiliana na daktarin au mtoa huduma za tiba kupitia simu yak ya mkononi ambaye anaweza kuchukua hatua stahiki.

Kuna teknolojia inayohusisha mifumo ya kompyuta inayoweza kufanya kazi ambazo kwa kawaida zinahitaji akili na utashi wa binadamu, yaani akili bandia au Artificial intelligence.

Zipo zinazowezesha uundaji wa kitu kutokana na usanifu unaoonyesha sehemu zake tatu, yaani three dimension, au 3D printing). Mfano wa faida za teknolojia hii ni kwenye afya ambamo madaktari wataweza kuona sehemu za mwili wa wagonjwa wanazotaka kuzifanyia upasuaji. Pia zinasaidia katika kutengeneza vifaa saidizi vya watu wenye ulemavu.

Teknokolojia nyingine in ile ya mawasiliano ya intaneti ya kasi, yaani uzao watanio, au 5G, ambayo Tanzania inaisubiri kwa hamu na itatumiwa na wengi. Hii itaongeza kasi ya mawasiliano na fursa zake.

Kasi ya 5G itakuwa zaidi ya mara 20 ya ile ya teknolojia ya 4G ambayo inatumiwa na wengi Tanzania wenye simu zenye uwezo mkubwa (simu janja) kwa huduma za intaneti. Itakuwa na kasi ya GB 20 (ishirini) kwa sekunde, ukilinganisha na GB moja (1) ya 4G LTE.

Mipango inayotekelezwa na serikali kwenye sekta ya TEHAMA inaweka misingi ya matumizi ya teknolojia hizi.

Kupitia mradi wa Tanzania ya kidijitali, serikali wa Tanzania itaboresha na kukuza maunganisho ya ndani na ya kimataifa ili kufikisha huduma za mawasiliano pamoja na utoaji wa huduma mbalimbali za Serikali kwa Wananchi.

Mradi huu una mikakati ya kuifanya Tanzania kuwa na uchumi wa kidjitali ndani ya miaka 10 ijayo. Inategemew kwamba shughuli zote za kiuchumi, uendeshaji wa sekta ya umma na utawala zitaendeshwa kidijitali.

Baadhi ya maeneo ambao mradi wa Tanzania ya kidijitali utaleta mabadiliko ni mawasiliano vijijini na Kuimarisha mitandao ya intaneto katika hospitali za wilaya kwenye maeneo ya vijijini na kuimarisha huduma za afya ya msingi.

Vilevile upo mpango wa kuboresha elimu ngazi ya sekondari, Matumizi ya TEHAMA shuleni na mradi wa elimu na Kuongeza stadi za TEHAMA kwa wavumbuzi na wajasiriamali. Lengo ni kuwaeezesha kuzalisha, kutengeneza na kuuza bidhaa kidijitali

Mingine ni matumizi ya TEHAMA kutekeleza miradi ya maji, kuongeza usalama katika mifumo ya malipo na kuwezesha wananchi kuwasilisha kero na malalamiko yao kwa serikali. Tayari kuna sehemu kwenye tovuti kuu ya serikali kwa ajili ya suala hili, inayoitwa e-mrejesho.

Mradi unatambua umuhimu wa kuongeza uelewa wa watanzania kwa ujumla kuhusu masuala ya TEHAMA. Uelewa huo ni katika matumizi ya vifaa na vyombo vya mawasiliano na katika huduma zinazotolewa.

Tanzania itavutia taasisi za kimataifa zinazojihusisha na uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma katika sekta ya TEHAMA ili kutekeleza malengo yake ya kuibadilisha nchi kuwa ya kidijitali.

Kama sehemu ya hatua za kuvutia wawekezaji na kuwezesha makampuni ya Tanzania kuwekeza nje ya nchi, serikali inakusudia kutunga sheria ya ulinzi wa wa taarifa binafsi za watu na taasisi. Hili ni sharti muhimu kwa mujibu wa Kanuni za Ulinzi wa Taarifa Binafsi za Umoja wa Ulaya katika kuvutia uwekezaji kwenye uchumi wa kidijitali.

Waraka wa majadiliano uliotolewa na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya habari hivi karibuni unasisitiza kwamba uwepo wa sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi utaweka mazingira wezeshi kwa nchi kuelekea uchumi wa kidijitali.

“Mwelekeo wa kiuchumi duniani unaonesha uwekezaji kwenye maeneo mbalimbali unategemea TEHAMA kama nyenzo muhimu katika shughuli za kiuchumi. Pamoja na mambo mengine yanayozingatiwa katika uwekezaji, wawekezaji makini hupendelea kuwekeza kwenye nchi ambazo zina mfumo wa kisheria na kitaasisi wa ulinzi wa taarifa binafsi”, inasomeka sehemu ya waraka huo.

Kwa mfano kampuni za TEHAMA za Ulaya na Marekani zinapotaka kuwekeza, huenda kwenye nchi ambazo tayari zina sheria za Ulinzi wa taarifa binafsi.

Wakati kampuni ya mtandao wa kijamii ya Twitter ya nchini Marekani ilifungua tawi nchini Ghana mwezi Aprili mwaka 2021, iliweka sharti ya kuwepo kwa sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi katika nchi hiyo kama kigezo cha msingi cha kufanya tatmini ya uwekezaji kule.

Hili pia lilitokea Kenya, ambao kampuni za Cisco, Facebook, Microsoft na Amazon zilifungua matawi nchini humo baada ya kuwepo sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi mwaka 2019.
Walimu wa shule ya sekondari ya Ukombozi, Urambo, Tabora wakibadilishana taarifa za elimu kupitia simu za mkononi. Mradi wa Tanzania ya Kidijitali unalenga kuimarisha matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa elimu



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post