Na Abdullatif Yunus - Michuzi Blog Kagera
Kituo cha kulelea Watoto Wadogo cha Ntoma Orphanage kinachosimamiwa na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Dayosisi ya Kaskazini Magharibi, kimetimiza Miaka Sabini ya Huduma huku Taarifa zikionesha kuwa Watoto 290 wamelelewa Kituoni hapo.
Akisoma Risala mbele ya Wageni na Mgeni Rasmi Mkuu wa Kituo hicho katika Tukio la Kubwa la Unyonyeshaji Watoto hao, ambalo limeratibiwa na Kamati iliyoongozwa na Mbunge wa Jimbo la Bukoba Vijijini Dkt. Samson Jasson Rweikiza, Bi Penina Kaimukirwa (Mtawa) Amesema Kituo hicho Mwaka huu kimetimiza Miaka 70 ya Huduma hiyo ya kulea Watoto Wadogo ambao huletwa hapo kufuatia Matukio mbalimbali katika Jamii husika, zikiwemo Changamoto za Kifamilia, huku akitaja changamoto mbalimbali kubwa ikiwa ni chakula cha Watoto hao.
Awali akiongoza Ibada Maalum ya kuombea Kituo hicho Mchungaji Dkt. Elimerek Kigembe amewakumbusha Wageni na waumini waliohudhuria, juu ya umuhimu wa kuendelea kuwalea Watoto hao, huku akisisitiza Maneno matakatifu Yanayosema kuwa "Dini Safi ni Ile inayojali Mayatima na Wajane katika Dhiki zao.."
Kwa upande Dkt. Samson Rweikiza ambaye Ni Mwenyekiti wa Kamati ya Shughuli hiyo ya Unyonyeshaji, ameendelea kuwaomba Wananchi kuguswa Mara kwa Mara na kutembelea Kituo hicho bila kujali Dini Wala itikadi, licha ya kuwa Kituo kipo chini ya Kanisa, lakini hata Watoto wenye Madhehebu na Dini nyingine wamekuwa wakilelewa hapo.
Katika Tukio hilo lililoambatana na Harambee ya Kuchangia Kituo hicho, Zaidi ya Milioni 30 zimechangwa ikiwemo ahadi na Pesa Taslimu, Harambee iliyoongozwa na Mhe. Charles Mwijage Mbunge.
By Mpekuzi
Post a Comment