IDARA YA WANAWAKE MASJID AKRAM YAADHIMISHA MAULID YA 16 YA MTUME MUHAMMAD S.W.A |Shamteeblog.

Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu Jaji. Imaan Aboud akizungumza wakati wa maadhimisho ya Maulid (Mazazi,) ya 16 ya Mtume Muhammad S.W.A iliyofanyika katika Masjid Akram Mbezi Beach na kuwahimiza wanawake kushika usukani katika malezi na maadili mema kwa watoto na vijana, Leo jijini Dar es Salaam.
 

 

WANAWAKE wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuimarisha malezi bora na kuwaongoza vyema katika maadili mema kuanzia ngazi ya familia ili kulinda maadili na hiyo ni pamoja na kuhakikisha watoto na vijana wanapata elimu ya dini na elimu dunia kwa manufaa ya jamii na Taifa kwa ujumla.

Hayo yameelezwa na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu Jaji. Imaan Aboud wakati wa maadhimisho ya Maulid (Mazazi,) ya 16 ya Mtume Muhammad S.W.A yaliyoandaliwa na Idara ya wanawake wa Akram Masjid na kufanyika katika Masjid Akram Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.

‘’Ninatoka katika Mahakama ya Afrika inayolinda na kutetea haki za binadamu na watu…na hakuna jambo jema kama kuhakikisha haki ya binadamu yeyote haivunjwi ni vyema tulinde amani kuanzia ngazi ya familia na tuhimize maadili mema, elimu ya dini na elimu dunia ili kuimarisha tunu za Taifa hasa amani, utulivu na uzalendo…..Tumche Mungu kwa kufuata tabia na mienendo kama Mtume Muhammad S.W.A anavyotuasa’’ Amesema.

Amesema, ni vyema wazazi hasa wanawake kushika usukani na kuwafundisha watoto kumcha Mungu tangu wakiwa wadogo ili kuwajenga vyema na kujenga kizazi bora cha sasa na hiyo ni pamoja na kuwa na mienendo na mazungumzo mema ambayo watoto na vijana wa watajifunza kutoka kwao.

Vilevile amewataka kuendeleza umoja na mshikamo bila kujali itikadi za kisiasa na tofauti za dini na kuleta maendeleo katika jamii na Taifa kwa ujumla pamoja na kuwasaidia wahitaji.

Pia Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanawake wa Kiislam Mkoa wa Dar es Salaam Mariam Mtambo aliwahimiza wanawake hao kuwa wanyenyekevu kwa kuwa uislam ni hekima na busara na kuwataka viongozi wa dini kukemea maadili yanayoporomoka.

‘’Tuombe kwa ajili ya watoto na vijana wetu wasitumbukie katika wimbi la maadili ambayo hali si nzuri tunasikia mambo ambayo hayamridhishi mwenyezi Mungu hata jamii…Tuwape watoto na vijana wetu elimu ya dini na elimu dunia ili waweze kujifahamu na kutenda matendo mema yanayompendeza Mungu.’’ Amesema.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Idara ya Wanawake Masjid Akram Mbezi Beach Mwajuma Kingwande amesema, hayo ni maadhimisho ya 16 ya mazazi (Maulid,) ya Mtume Muhammad S.A.W na wamekuwa wakikutana kumswalia pamoja na kupata masomo na mawaidha ya kuwajenga wanawake katika imani na dunia kwa ujumla.

Amesema katika Maulid hiyo suala la maadili limetiliwa mkazo kwa wanawake wa kiislamu na dini zote na kuwataka wanawake wote kuwa karibu na Mwenyezi Mungu pamoja na kuwaelekeza wanawake katika maadili mema na kuwahimiza kupata elimu ya dini na elimu dunia ili kujenga kizazi kinachoishi maisha yanayompendeza Mungu na kizazi chenye manufaa ya kiuchumi katika jamii na Taifa kwa ujumla.

Pia Makamu Mwenyekiti wa Idara ya Wanawake Masjid Akram Mbezi Beach Zainab Kasoro amesema kupitia Maulid ya Muhammad S.A.W inayofanyika kila mwaka wamekuwa wakipata elimu ya dini na elimu ya dunia ili kujifahamu zaidi katika imani na kumtii mwenyezi Mungu pamoja na elimu dunia mahsusi katika kuwajenga katika masuala ya uchumi pamoja na kuwasaidia mahitaji.

‘’Kupitia idara yetu hapa Mbezi Beach kwa kushirikiana na ndugu, marafiki na jamii tumekuwa tukisaidia wahitaji kutoka makundi mbalimbali wakiwemo wajane na Watoto yatima katika mahitaji na huduma mbalimbali ikiwemo kulipa bili za maji na umeme kupitia sadaka na kutekeleza kwa vitendo yanayofundishwa na Mtume Muhammad S.A.W..’’ Amesema.

Kupitia Maulid hiyo wanawake wa kiislamu walipewa mawaidha mbalimbali ikiwemo kuomba mwisho mwema, kuwasaidia wahitaji,malezi na maadili kwa vijana na watoto pamoja na kutunza tunu za Taifa za amani, mshikamano, undugu na umoja, uzalendo bila kujali dini wala itikadi za kisiasa.

 Mwenyekiti wa Idara ya Wanawake Masjid Akram Mbezi Beach Mwajuma Kingwande akizungumza wakati wa maadhimisho hayo na kueleza kuwa, hayo ni maadhimisho ya 16 ya mazazi (Maulid,) ya Mtume Muhammad S.A.W na wamekuwa wakikutana kumswalia pamoja na kupata masomo na mawaidha ya kuwajenga wanawake katika imani na dunia kwa ujumla.

Makamu Mwenyekiti wa Idara ya Wanawake Masjid Akram Mbezi Beach Zainab Kasoro akizungumza wakati wa maadhimisho hayo na kueleza kuwa  kupitia Maulid ya Muhammad S.A.W inayofanyika kila mwaka wamekuwa wakipata elimu ya dini na elimu ya dunia ili kujifahamu zaidi katika imani na kumtii mwenyezi Mungu pamoja na elimu dunia mahsusi katika kuwajenga katika masuala ya uchumi pamoja na kuwasaidia mahitaji.
 











Matukio mbalimbali wakati wa hafla ya Maulid hiyo.

 


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post