Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
NAIBU Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Khamis Hamza Chilo amesema amesikitishwa na kasi ya uharibu wa mazingira inayofanywa na baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali ikiwemo wilayani Mbarali mkoani Mbeya,ambapo kumefanyika uharibifu mkubwa na hali ya mazingira imekuwa mbaya huku akitoa rai kwa watanzania kutunza mazingira sambamba na kupanda miti.
Chilo ameyasema hayo Oktoba 24,2022 mbele ya wananchi wa Ubaruku wilayani Mbarali mkoani Mbeya ambapo Mawaziri Nane wakiongozwa na Mwenyekiti wao Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Angelina Mabula wanaendelea na ziara yao ya kwenda mikoa mbalimbali kushuhudia masuala mbalimbali yakiwemo ya uharibifu wa mazingira, vyanzo vya maji pamoja na migogoro ya ardhi.
“Ndugu wananchi leo tumefanya ziara katika mkoa huu ni moja ya muendelezo wa ziara zetu ambazo tumezianza kwenye mikoa mingine na leo tuko hapa, kabla ya kufika hapa tulifanya ziara ya kutembelea vijijini lakini tulipofika huko hali ya mazingira huko ni mbaya , hali ya mazingira tuliyoona huko mabondeni ni mbaya sana na mazingira yake yameharibiwa na binadamu kwa maana ya sisi wenyewe .
“Tumeshuhudia mambo mengi ambayo tukikaa kimya tusipoyasema taifa hili litakuwa linaelekea pabaya, cha kwanza ambacho tumekiona kule tumegundua kuna uharibu mkubwa wa mazingira, mazingira ya binadamu yanaharibiwa mpaka tunafika wakati tunasema huku hakuna watu wa kusimamia lakini mwisho wa siku wasimamiaji ni ninyi wenyewe.
“Watu wa Wilaya hii, watu wa vijiji hivi, watu wa maeneo haya tulichokiona kule ukataji mkubwa wa miti, watu wamekata na wamejengea lakini tumeshuhudia malundo ya kuni au miti imepangwa, sasa tukifika wakati miti yote tumeikata kuna siku tuja tusimamie chini ya miti tufanye vikao, lakini tutafika wakati tutakuwa tunaitaka mvua katika wilaya hii tutaisikia tu katika mikoa ya wenzetu hapa hatutaipata, sasa sijui tutalima vipi, sijui tutafuta vipi, sijui sisi kama binadamu tutaishi vipi , bila ya maji bila ya mvua.”
Chilo ameongeza katika ziara hiyo wameshuhudia vyanzo vya maji vimeharibiwa sana , maji yale ndio yanayosababishia watu kuishi.“Maji yale yale ndio yanayofanya kuweza kusukuma umeme ukapatikana, maji yale (Mto Ruaha) ndio hayo wengine wanayatumia kuishi, tumekwenda kwenye bonde tumeona hali mbaya, mifugo inaingizwa ndani ya vyanzo vya maji, maji yanaharibiwa.”
Aidha amesema kingine ambacho wamekishuhudia kuna baadhi ya watu wamekwenda kufanya makazi kwenye maeneo ambayo hayastahili watu kufanya makazi , tena wengine wanajenga nyumba za kudumu kabisa, sasa ile hali inasababisha mazingira ambayo si mazuri na inakuja kuwapa wakati mgumu Serikali , kwa hiyo amesisitiza kwamba mazingira ndio kila kitu na yasipoyatunzwa na mazingira nayo hayatawatunza.
Ametoa mwito watu wapande miti watu watunze vyanzo vya maji, mazingira watu waheshimu sheria na taratibu zote zinahusiana na mazingira.
By Mpekuzi
Post a Comment