Na Mwandishi wetu Dodoma
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 tarehe 31 Oktoba, 2022 katika uwanja wa michezo wa Jamhuri jijini Dodoma.
Akitoa taarifa kwa Umma kupitia Vyombo habari hii leo Oktoba 21,2022 Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amesema kuwa Maandalizi ya uzinduzi huo yanaendelea vizuri na Serikali imejiandaa kuhakikisha kuwa wananchi wote wanapata fursa kufahamu matokeo ya Sensa.
Senyamule amesema kwa mujibu wa Mpango wa Utekelezaji na Usimamizi wa Sensa ya Watu na Makazi, mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhesabu watu, kazi zinazotakiwa kufanyika ni kuchakata taarifa zilizokusanywa ili kupata matokeo yake na hatimae kutangazwa rasmi kwa umma matokeo ya mwanzo.
"Mara baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhesabu watu tarehe 5 Septemba, 2022 wataalamu wetu walianza zoezi hilo la uchakataji wa taarifa. Hadi sasa matokeo ya mwanzo yako tayari kwa uzinduzi,"Amesema Senyamule
Na Kuongeza kuwa "Ninayo furaha kutangaza kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan atazindua Matokeo ya Mwanzo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 tarehe 31 Oktoba, 2022 katika uwanja wa michezo wa Jamhuri jijini Dodoma,"Senyamule
Mkuu huyo wa Mkoa ametolea mifano Sensa zilizopita ikiwemo ile ya mwaka 2002na 2012 ambazo zilitumia teknolojia ya usomaji wa vivuli (Scanning Technology), matokeo ya Sensa hizo yalizinduliwa rasmi miezi mitatu baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhesabu watu ,wakati Sensa ya mwaka 2022 matokeo yake yanazinduliwa mwezi mmoja baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhesabu watu na makazi.
"Kwa Sensa ya mwaka huu, matokeo yake kama mnavyoona yatatoka ndani ya kipindi cha mwezi mmoja baada ya kukamilika kwa zoezi la kuhesabu watu ,ambapo ni mafanikio makubwa katika utekelezaji wa Sensa nchini kwetu na yamewezekana kutokana na matumizi makubwa ya tekinolojia za kisasa hasa matumizi ya vishikwambi katika awamu zote za utekelezaji wake na utashi wa Siasa katika kusimamia zoezi hilo kuanzia maandalizi hadi leo," Amesema Senyamule
Wakati huohuo RC Senyamule ametumia nafasi hiyo kupitia vyombo vya habari kutoa wito kwa wananchi wote Mkoa wa Dodoma, Taasisi zote, Watumishi wa Umma wote na wa Sekta binafsi Mkoani Dodoma, Makundi mbalimbali katika jamii (wafanya biashara, Dini, Walemavu, Bodaboda, Machinga, Wazee n.k) na wananchi kutoka Mikoa yote jirani kumuenzi Rais kwa kujitokeza kwa wingi tarehe 31 Oktoba, 2022 kwenye viwanja vya Jamhuri kujumuika katika katika tukio hilo.
Ikumbukwe kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ilikamilisha rasmi zoezi la Kuhesabu Watu, Kuhesabu Majengo, na Kuhesabu Anwani za Makazi kupitia mfumo wa utekelezaji wa Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022 tarehe 05 Septemba, 2022.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule
By Mpekuzi
Post a Comment