TUNATAKA MUONGEZE MAPATO -WAZIRI BALOZI CHANA |Shamteeblog.

Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Pindi Chana, amesema miradi inayobuniwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ni njia sahihi ya kuongeza idadi ya watalii na kufikia lengo la Serikali la kuwa na milioni tano.

Waziri huyo pia amesema kubuniwa kwa miradi hiyo kutasaidia kuongeza mapato ya dola 6 bilioni kufikia mwaka 2025.
 

Amezungumza hayo wakati akizindua Bodi ya tatu ya Wakurugenzi ya TAWA mjini Morogoro leo Ijumaa Oktoba 12, 2022.

Ameongeza kuwa idadi ya watalii na mapato yameongezeka na hivyo kuashiria njia nzuri ya uhifadhi, ambapo mwaka 2021 hadi 2022 idadi ya wageni waliotembelea vivutio vya TAWA ni 158,000 wakiingiza Sh49.5 bilioni ikilinganishwa na watalii 38,000 ambao walileta mapato ya Sh25.7 milioni.

Aidha amesema katika kuhakikisha wanadhibiti uharibifu unaofanywa na wanyamapori Wizara inajiandaa kuwafunga GPS Tembo hasa Tembo kiongezi ili kujua mahali alipo kwa lengo la kuwasaidia kufuatilia wanapopata taarifa za uvamizi.

Waziri huyo ametoa rai kwa wananchi wanaozunguka maeneo ya hifadhi kutoa ushirikiano katika kuhifadhi mazingira kwa sababu maeneo ya hifadhi sio maeneo ya kulishia mifugo bali ni maeneo yaliotengwa kwa manufaa ya watanzania wote.

“Ukiingiza mifugo hifadhini utakausha vyanzo vya maji na kuharibu uoto wa asili, tushirikiane bega kwa bega katika kuhifadhi na kutumia vyanzo vingine katika kulishia mifugo yetu,” alisema Waziri Chana

Mwenyekiti mpya wa Bodi ya wakurugenzi TAWA Meja Jenerali Mstaafu Hamisi Semfuko alimpongeza Rais Samia Suluhu Hassani kwa kuboresha shughuli za utalii kwa kuzindua Royal Tour ambayo imesaidia katika sekta ya utalii na kufanya asilimia 60 ya wawindaji kutoka nchi za kigeni ikiwemo Marekani kuingia nchini.

Bodi mpya ya wakurugenzi iliyozinduliwa ni Mwenyekiti Meja Jenerali Mstaafu Hamisi Semfuko, Katibu Mabula Misungwi Nyanda na wajumbe wa bodi ambao ni Dk Jafari Kiegesho, Dk Simon Mduma, Profesa Suzan Augustino, Beatrice Kimoleta, Naibu Kamishina wa polisi Simon Thobias na Dk Vales Msuha.

Naye Kamishna wa Uhifadhi TAWA Mabula Misungwi alimshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapatia mradi wa ujenzi wa vituo 16 vya askari kwa ajili ya kukabiliana na matukio ya wanyamapori wakali na waharibifu ambapo aliahidi kuusimamia vyema na kuhakikisha shughuli iliyokusudiwa inatekelezwa vyema.

Aidha Misungwi pia aliipongeza Serikali kupitia mradi wa maendeleo na ustawi wa Taifa na mapambano dhidi ya Uviko-19 kwa kuwapatia magari na mitambo mbalimbali ili kutekeleza vyema shughuli za uhifadhi katika mapori ya akiba yaliyopo.




 

By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post