Na Said Mwishehe,Michuzi TV
WAZIRI Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama amewashauri watanzania hususan viongozi mbalimbali, kujenga utaratibu wa kusoma na kuandika vitabu kwa lugha ya Kiswahili ili kuchagiza utekelezaji wa mipango ya taifa, na kubadili fikra za watanzania.
Mhagama ametoa ushauri huo jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Maktaba ya UONGOZI na Utambulisho wa toleo la Kiswahili la kitabu cha aliyekuwa Rais wa Awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa cha 'Maisha yangu kusudio langu' kwa lengo la kusaidia watanzania wote wasioelewa lugha ya kingereza kupata fursa ya kukisoma.
Katika uzinduzi wa kitabu hicho pamoja na Maktaba ya Taasisi ya UONGOZI iliyopo Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere wageni waalikwa mbalimbali walihudhuria wakiwemo viongozi walioko kwenye utumishi pamoja na waliostaafu.Pia waliokuwepo wawakilishi wa mataiafa mengine kadhaa.
"Machapisho na vitabu vingi nchini vimeandikwa kwa lugha za kigeni, hivyo ili kuondoa dhana ya kuwa watanzania kukosa utaratibu wa kusoma vitabu kwa kigezo cha kutoelewa lugha, waandishi wa vitabu wanatakiwa kujikita zaidi kuandika vitabu vyao katika lugha ya Kiswahili kwa kuzingatia maadili natamduni za Mtanzania.
"Tukiwa na vitabu ambavyo vitaandikwa kwa lugha rafiki naamini wengi watapenda kusoma lakini tusiishie kuandika vitabu vyenye mambo magumu peke yake ,ni vema vikaandikwa na vitabu ambavyo vitafanya msomaji kutoona uvivu kukisoma,kitabu kinaweza kuandikwa katika historia ya kufurahisha na hivyo kuvuta wengi,"amesema Waziri Mhagama.
Aidha Waziri Mhagama ametoa Rai kwa Taasisi ya UONGOZI kuangalia namna ya kuhakikisha vitabu ambavyo ambavyo wanavyo kwenye maktaba yao kikiwemo kitabu cha Hayati Mkapa vikasambazwa kwenye shule za msingi, sekondari pamoja na vyuoni na hiyo itaongeza hamasa ya Watanzania kusoma vitabu.
"Nashauri kwa Taasisi ya UONGOZI hiki kitabu cha mzee wetu Benjamin Mkapa ni vema kikasambaza mashuleni wanafunzi wetu wasome, na wakianza kusoma wakiwa wadogo itafanya wawe na muamko wa kusoma vitabu."
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu na Mwenyekiti wa Bodi ya taasisi ya Uongozi, Balozi Ombeni Sefue, ameeleza kwamba viongozi na watanzania kwa ujumla wanapaswa kumtendea haki Hayati Rais Mkapa kwa kusoma kitabu hicho alichokiandika kwa ajili ya ila mtanzania.
Wakati Mbunge wa Jimbo la Ubungo jijini Dar es Salaam Profesa Kitila Mkumbuko amesema kuna kila sababu ya Serikali kuweka mazingira rafiki wananchi kuibu mijadala na hivyo itasababisha watu kuandika vitabu na kusoma." Kumekuwa na changamoto kwa sasa vijana vyuoni wanaogopa kuweka majukwaa ya majadiliano kwasababu wakionekana wanajadiliana wanaonekana wanafanya makosa.
"Enzi zetu tukio Chuo Kikuu mijadala ilikuwa inafanyika bila vikwazo, na kweye mijadala ndiko ambako watu wanalazimika kusoma vitabu ili kuwa na uelewa mpana wa mambo na kujenga hoja,"amesema na kuongeza kwamba bado kuna changamoto ya watu kupenda kusoma vitabu na matokeo yake hata viongozi wanapokosea hakuna wa kuhoji.
"Napenda sana kusoma vitabu tangu zamani na bahati nzuri nimewahi kuwa Waziri Kuna wakati unazungumza jambo na unapotafakari unaona kabisa sikuwa sahihi lakini hakuna aliyekuwa akihoji, lakini kama kungekuwa na utamaduni wa watu kusoma vitabu wangekuwa na uwezo wa kuhoji.Rai yangu ni lazima tujenge utamaduni wa kupenda kusoma vitabu,"amesema Profesa Mkumbuko.
Kwa upande wa Mke wa Hayati Benjamin Mkapa, Mama Anna Mkapa akizungumza kwenye uzinduzi wa kitabu cha Hayati Mkapa ambacho kimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili amesema pamoja na kuzindua kitabu hicho kwa lugha ya Kingereza lakini kiu kubwa ya Mzee ilikuwa ni kuwa na kitabu chenye lugha ya Kiswahili kinachozungumzia maisha yake na sasa Taasisi ya Uongozi wametimiza hilo.
Zitto Kabwe yeye alipokuwa akizungumza kwenye uzinduzi huo amesema amekuwa na utamaduni wa kupenda kusoma vitabu huku akitumia nafasi hiyo kuwaomba viongozi kuandika vitabu vinavyozungumzia maisha yao pamoja na uzoefu wao kwenye masuala ya uongozi.
"Hiyo itasaidia Watanzania hasa vijana kutambua historia ya maisha ya viongozi akitoa mfano amemfahamu zaidi Benjamin Mkapa kupitia kitabu chake kwani wakati anamaliza uongozi wa nchi yeye( Zitto) ndio alikuwa anamaliza sekondari,"amesema Zitto.
Awali akizungumza kabla ya uzinduzi huo Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya UONGOZI Kadari Singo ameeleza tukio hilo limejumuisha utambulisho wa toleo la Kiswahili la tawasifu ya Rais wa tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Benjamin William Mkapa, “Maisha Yangu,
Kusudi Langu: Kumbukizi ya Rais wa Tanzania”.
Amesema awali kitabu hicho kiliandikwa kwa lugha ya Kiingereza na kuzinduliwa Novemba, 2019 na hayati John Pombe Magufuli, Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania." Wakati wa uzinduzi "Mheshimiwa Rais aliiagiza Taasisi ya UONGOZI itafsiri kitabu hicho kwenda kwenye lugha ya Kiswahili ili kuwafikia Watanzania wengi zaidi.
"Washiriki kwenye tukio hili ni pamoja na mke wa Rais Mstaafu Mkapa, Mama Anna Mkapa;
Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi ya UONGOZI; viongozi waandamizi kutoka kwenye sekta
za umma na binafsi; washirika wa maendeleo; na wanachama wa Maktaba hiyo. "
Maktaba ya Uongozi ilianzishwa mnamo mwaka 2012 kwa lengo la kuhamasisha
utamaduni wa kutoa maarifa na kujisomea nchini na Barani Afrika kwa ujumla na kwamba kupitia Maktaba hiyo, viongozi, watafiti, wanafunzi na jamii kwa ujumla, wanaweza kufikia machapisho ya masuala ya uongozi na maendeleo endelevu yanayoendana na
mabadiliko mbalimbali duniani. Maktaba ina vitabu na majarida zaidi ya 50,000, ikiwemo
vile vilivyochapishwa na katika mifumo ya kielektroniki.
Waziri Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama akiwa na Ofisa Mtendaji Mkuu Taasisi ya UONGOZI Kadari Singo wakiangalia vitabu vilivyopo kwenye maktaba hiyo.
Waziri Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama akiwa amekata utepe kuashiria kuzindua rasmi Maktaba ya UONGOZI iliyopo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Waziri Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama(wa nne kulia), Mke wa Hayati Rais Mstaafu Benjamin Mkapa,Mama Anna Mkapa ( wa tatu kushoto) wakiwa na viongozi wengine wakati wa uzinduzi wa Maktaba ya Uongozi na Utambulisho wa toleo la Kiswahili la kitabu cha Rais wa Awamu ya tatu, Hayati Benjamin Mkapa cha 'Maisha yangu kusudio langu' uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Mkuruenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communication Bakari Manchumu (katikati) akiongoza mdahalo ulioangazia yali ya usomaji wa vitabu nchini katika hafla hiyo. (wa pili kushoto), ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo Prof. Kitila Mkumbo, na (wa tatu kulia), ni Kiongozi Mkuu wa Chama cha Siasa cha ACT - Wazalendo Zitto KabweMatukio mbalimbali katika picha wakati wa tukio hilo
By Mpekuzi
Post a Comment