Rais aliyeondoka madarakani Uhuru kenyatta na mrithi wake William Ruto
Siku chache tu baada ya rais William Ruto kula kiapo cha kuwa rais , alianza kazi ya kurekebisha kile ambacho mtangulizi wake Uhuru Kenyatta anadai alikosea wakat wa Uongozi wake.
Na ili kudhihirisha kwamba uhasama uliokuwepo kati yake na mtangulizi wake haukuwa jambo la mzaha, kiongozi huyo alipangua baadhi ya maagizo yaliofanywa na mtangulizi wake .
Miongoni mwao ni suala la usajili wa majaji sita wa mahakama kuu ambao rais Uhuru Kenyatta alikataa kuwateua akidai walikuwa hawana maadili.
Pamoja na suala hilo haya hapa maagizo saba ya Uhuru Kenyatta yaliobadilishwa na mrithi wake Rais William Ruto.
1. Kuondolewa kwa ruzuku ya mafuta na Unga
Hatua ya rais William Ruto ya kuondoa ruzuku ya mafuta na ile ya chakula ilipokelewa na hisia tofauti nchini Kenya kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha kote duniani.
Licha ya kwamba ruzuku hizo zilelanga kuwapeusha wakenya wa kipato cha chini dhidi ya makali ya kupanda kwa bei za bidhaa ulimwenguni , Rais William Ruto alitofautiana.
Rais Ruto alisema kwamba ruzuku ya mafuta pamoja na ile ya chakula haijawasaidia Wakenya , akiongezea kwamba ruzuku ya mafuta pekee imemgharimu mlipa kodi ksh. 144b, huku ksh.7b zikitumika katika kipindi cha miezi minne iliopita kabla ya serikali yake kuchukua madaraka.
Ruzuku hizo ziliwekwa na rais Uhuru Kenyatta wakati wa utawala wake huku kukabiliana na bei za juu za mafuta na unga wa mahindi huku akitafuta suluhu ya kudumu kwa tatizo hilo.
Hatahivyo ,Ruto alisema kwamba mbali na kuwa ghali , ruzuku hiyo ilikuwa ikitumiwa vibaya , imefnya uharibifu wa soko na imekuwa ikitumika kutengeneza uhaba bandia wa bidhaa hiyo.
2. Kuuangazia upya mfumo wa elimu wa CBC
Serikali ilipoamua kubadilisha mtaala wa 8-4-4 na kuweka mtaala unaozingatia Umahiri (CBC), habari hizo zilipokelewa kwa mitazamo tofauti.
Wadau wakuu, kama vile Tume ya Utumishi wa Walimu, Taasisi ya Ukuzaji Mitaala, Vyuo vya Ualimu, Wakuu wa Shule na walimu walishiriki kwa kiasi kikubwa katika uzinduzi, uanzishaji na utekelezaji endelevu wa CBC.
Wote waliruhusiwa kueleza wasiwasi wao na kushiriki michango katika kufanikisha mtaala.
Ni kutokana na manung'uniko hayo ambayo yalimshinikiza Rais William Ruto kuanzisha jopo ambalo litsaidia katika kuwauliza Wakenya iwapo mfumo huo wanadhania unapaswa kuendelea kuhudumu na maeneo yapi yalipaswa kurekebishwa .
Rais pia aliahidi kutatua suala la mpito la wanafunzi wa darasa la nane chini ya mfumo wa 8-4-4 na Gredi ya sita chini ya mfumo wa CBC hadi katika shule ya upili mwezi Januari.
KIongozi huyo amsema kwamba kuna mazungumzo ya kiwango cha juu yanayoendelea nchini hususan katika kuidhinisha CBC.
3. Kupakua na kuondoa mizigo bandarini Mombasa
Kufuatia hatua ya serikali iliopita kutangaza kwamba ilikuwa inafungua bandari ndogo ya nchi kavu katika eneo la Naivasha na kwamba baadhi ya huduma za badanri ya Mombasa zingeathiriwa kulikuwa na hisia kali mjini humo huku baadhi ya wafanyabiashara wakiamua kufanya maandamano.
Hatahivyo utawala ulioondoka haukuridi nyuma katika uamuzi wake huo , na kilichotokea ni kwamba raia wengi wa eneo la pwani walipoteza ajira zao huku wale wa Naivasha wakipata ajira hizo.
Hatahivyo wakati wa kampeni za uchaguzi uliopita rais William Ruto aliapa kurudisha huduma za bandari hiyo Mombasa, ili wakaazi wanedelea kufaidika nazo. Na muda mfupi tu baada ya kuapishwa Rais Ruto alitoa agizo la mara moja la kurudishwa kwa huduma hizo kinyue na mtangulizi wake rais Uhuru Kenyatta.
Huduma hizo ni pamoja na upakuzi wa shehena kutoka bandarini humo ambalo litaruhusu kuondolewa kwa bidhaa zote na masuala mengine ya kiutendaji kurejea katika bandari ya Mombasa, hivyo basi kubatilisha agizo la awali la aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta. Hii, alisema, itarejesha maelfu ya kazi katika jiji la Mombasa.
4. Komesha Kufungiwa kwa wenye mikopo CRB
Zaidi ya watu milioni nne waliokosa mikopo wataondolewa kwenye orodha zisizoruhusiwa za Credit Reference Bureau (CRB) chini ya mipango iliyopendekezwa na Rais William Ruto ya kurekebisha soko la mikopo nchini.
Rais aliagiza Benki Kuu ya Kenya (CBK) kukomesha kuorodhesha wakopaji na badala yake iwe na mbinu ya kupata alama ambapo wanaokiuka watapata alama za chini badala ya kufungiwa nje ya mfumo wa kifedha.
Rais Ruto alisema serikali inaunga mkono utaratibu wa kutoa mikopo lakini inataka mfumo ambapo wakopaji wanaweza kufuzu kutoka mkopaji wa kiwango cha chini hadi bora zaidi, ambapo wataruhusu kukopa kulingana na hatari.
Rais alisema utawala wake utahamisha mfumo wa Bodi ya Mikopo (CRB) kutoka kwa utaratibu wake wa sasa wa kuwaorodhesha wakopaji kiholela kwa lengo la kuwanyima mikopo.
5. Majaji sita waliokataliwa, ufadhili wa Mahakama
Katika hatua ambayo iliwashangaza wakenya wengi wakati wa utawala wa Rais Uhuru Kenyatta, kiongozi huyo alikataa katakata kuwaapisha majaji sita ambao walikuwa wameteuliwa na tume ya huduma za mahakama ili kuhudumu kama majaji.
Taarifa kutoka Ikulu ilisema kuwa Rais alikataa uteuzi wa Majaji wa Mahakama ya Juu Joel Ngugi, George Odunga, Aggrey Muchelule na Weldon Korir kwa mahakama ya Rufaa "kwa kukosa kuafikia kiwango kinachohitajika".
Wengine ambão pia walikosa kuorodheshwa ni Msajili wa Mahakama Kuu Judith Omange na Hakimu Mkuu Evans Makori, ambaye alikuwa ameteuliwa katika Mahakama ya Mazingira na Ardhi.
Lakini katika kampeni za uchaguzi mkuu uliopita rais Ruto aliahidi kubadili uamuzi huo na kuamua kuwaapisha punde atakapochukua madaraka.
Na ili kudhihirisha zaidi kujitolea kwake kwa uhuru wa Idara ya Mahakama, Rais Ruto aliwateua majaji hao sita na kuwaapisha mara moja
Zaidi ya hayo, alisema utawala wake utaongeza mgao wa bajeti kwa Idara ya Mahakama hadi bilioni 3 kila mwaka kwa miaka mitano ijayo.
Rasilimali hizi, alisema, zitasaidia kuongeza kiwango cha chini cha haki kwa kuongeza idadi ya mahakama ndogo kutoka 25 za sasa hadi 100.
6. Kuondolewa Wizara ya Ugatuzi
Wakati huohuo Rais William Ruto aliiondoa wizara moja - wizara ya ugatuzi - ambayo ilikuwa katika baraza la mawaziri la mtangulizi wake, Rais Uhuru Kenyatta.
Kuondolewa kwa wizara ya ugatuzi kuliibu mijadala ya umma kuhusu iwapo Kenya itaafikia malengo ya ugatuzi ipasavyo, jinsi inavyotazamiwa katika katiba ya 2010.
Aliyekuwa Waziri wa Ugatuzi Eugene Wamalwa alikashifu uamuzi huo akishangaa kwa nini Ruto hakuuona kama kipaumbele.
Hatahivyuo baadhi ya raia walisema kwamba ilikuwa ni Wizara ambayo ilihusishwa na serikali ya kitaifa ikisisitiza kung'ang'ania baadhi ya majukumu ambayo yalipaswa kugatuliwa.
Raia hao walisema kwamba shughuli zote ambazo zimegatuliwa zinafaa kwenda kaunti kwa hivyo hakuna sababu ya kuwa na wizara kama hiyo.
Baadhi ya ‘sababu za ushindi wa William Ruto dhidi ya Raila Odinga katika uchaguzi wa urais’19 Agosti 2022
William Ruto: Muuza kuku aliyepanda ngazi hadi kuwa rais wa Kenya12 Agosti 2021
Je, rais anayeondoka wa Kenya atakumbukwa vipi?12 Septemba 2022
7. Kuongezeka kwa Malipo ya NHIF
Rais William Ruto ameunga mkono msukumo wa kutaka matajiri walipe michango ya juu zaidi ya kila mwezi kwa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF), miezi kadhaa baada ya pendekezo sawia kutupiliwa mbali na Bunge.
Bw Ruto alisema kuwa michango ya NHIF itaegemezwa kwenye malipo ya kila mwezi ya wafanyikazi, katika azma ya kuongeza ufadhili wa mpango huo.
NHIF mapema mwaka huu ilipendekeza kwamba michango ya wafanyikazi wanaopata zaidi ya Sh100,000 inapaswa kuhesabiwa kuwa asilimia 1.7 ya malipo yao. Lakini hii ilikataliwa na Bunge lililopita , na kulazimisha bima hiyo kutafuta mbinu mbadala.
Hatua ya Dkt Ruto, ambaye sasa anaungwa mkono na wabunge wengi kuunga mkono pendekezo la NHIF, inajiri kama afueni kuu kwa bima ya kitaifa ambayo imekuwa ikitafuta mbinu za kuongeza ufadhili wake kutekeleza mpango wa afya kwa wote.
Rais Ruto alitangaza kuwa michango iliyotolewa na Wakenya kwa Hazina ya Kitaifa ya Bima ya Hospitali (NHIF) sasa itategemea mapato ya mtu binafsi.
Hii ni habari njema kwa watu wa kipato cha chini kwani ina maana sasa wanaweza kulipa kidogo.
Kwa sasa, wafanyakazi wanaopata zaidi ya Sh100,000 watalipa mchango uliopangwa wa kila mwezi wa Sh1,700 huku wafanyakazi wanaolipwa chini kabisa wakichangia Sh150.
VISIT WEBSITE
from Author
Post a Comment