Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam
RAIA wa Somalia ameshukuru kwa huduma ya upasuaji wa kuziba tundu la moyo aliofanyiwa mtoto wake mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI).
Shukrani hizo amezitoa leo jijini Dar es Salaam wakati akiongea na mwandishi wa habari hizi mara baada ya mtoto huyo kuruhusiwa kutoka wodini ambako alikuwa anapatiwa matibabu.
Hirs Ally ambaye ni baba mdogo wa mtoto alisema baba wa mtoto huyo aliyeko nchini Somalia alipata taarifa ya kupatikana kwa huduma ya upasuaji wa moyo JKCI na hivyo kumtuma mtoto huyo aliyeambatana na bibi yake kuja hapa nchini kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
“Tunashukuru huduma tuliyoipata ni nzuri kuna vifaa vya kutosha pia madaktari na wauguzi ni marafiki kila unachowauliza wanakujibu na wanakwambia kila kitu ambacho mtoto anaenda kufanyiwa,”.
“Tuliamua kumleta mtoto wetu JKCI kwani gharama za matibabu ni ndogo ukilinganisha na nchini Somalia pia kuna wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu na vifaa viko vya kutosha, ninawasihi wazazi wenye watoto ambao wanamatatizo ya moyo wawalete hapa kwa ajili ya matibabu,”alisema Hirs.
Kwa upande wake daktari bingwa wa magonjwa ya moyo kwa watoto wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Evelyn Furumbe alisema walimpokea mtoto huyo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili tarehe 10/10/2022 na baada ya kumfanyia vipimo waligundua moyo wake una tundu.
Dkt. Evelyn alisema tarehe 11/10/2022 mtoto alifanyiwa upasuaji wa kuziba tundu hilo ambapo hadi sasa anaendelea vizuri na leo hii ameruhusiwa na atarudi kwa ajili ya kliniki baada ya wiki mbili ili kuangalia maendeleo yake.
“Mtoto alikuwa na tundu ambalo linakuwa kati ya mshipa wa kupeleka damu kwenye mwili (Aorta) na wa kupeleka damu kwenye mapafu (Pulmonary) hili tundu mtoto akizaliwa huwa linafunga lakini la kwake halikufunga na lilikuwa na ukubwa wa milimita 6. Pia alikuwa na nyama chini ya Valvu ambayo ilikuwa inasababisha damu kupita kwa kasi katika Aorta na kusababisha mlango wa Aorta kuharibika na kuanza kuvuja damu hivyo basi tiba yake ilikuwa ni kukata nyama na kuziba tundu,”.
“Watoto wenye shida kama hizi huwa tunawapokea mara kwa mara na wanafanyiwa upasuaji na kupona na kuendelea na maisha kama watoto wengine,” alisema Dkt. Evelyn.
By Mpekuzi
Post a Comment