HIFADHI YA TAIFA ZIWA MANYARA YAWAVUTIA WAZAWA, WAMIMINIKA KUITEMBELEA |Shamteeblog.

Na Seif Mangwangi, Arusha

HIFADHI ya Taifa ya ziwa Manyara imeelezwa kuvutia mamia ya watanzania ambao wamekuwa wakitembelea hifadhi hiyo katika kipindi cha siku kuu za mwisho wa mwaka kufuatia kufikika kwa urahisi tofauti na hifadhi zingine.

Akizungumza na waandishi wa habari wanachama wa klabu ya waandishi wa habari Arusha, waliotembelea hifadhi yao kwa lengo la kujionea vivutio vilivyopo na kuvitangaza, Mhifadhi utalii katika hifadhi hiyo Ahmed Nassoro amesema idadi kubwa ya watanzania wameanza kufika katika hifadhi ya Manyara.

Amesema wingi wa watanzania unatokana na ukaribu uliopo hifadhi hiyo na vivutio vingi vilivyomo ikiwemo simba wanaopanda miti, ziwa Manyara, Maji moto yanayotiririka kutoka chini ya miamba ambayo huweza kuchemsha mayai kwa muda mfupi kufuatia kuwa na joto kali.

"Hifadhi ya Ziwa Manyara ni hifadhi inayofikika kwa urahisi sana, hapa kuna simba wanaopanda miti, kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo msitu uliofunga hivyo hulazimika kupanda juu ili waone mawindo vizuri lakini pia hapa kuna chemchem ya maji moto yanayoivisha hadi mayai, ukifika utajiona mwenyewe maajabu haya," amesema.

Nassor amesema hifadhi ya Manyara pia ina kivutio cha cha daraja la kamba lenye urefu wa mita400 juu ya miti ambapo watalii wengi wanaotembelea katika hifadhi hiyo wamekuwa wakivutiwa nalo.

Wakati huo huo, Kaimu Kamishna wa Utalii hifadhi ya ziwa Manyara, Neema Mollel amewataka Watanzania kutumia likizo ya siku kuu ya christmass na mwaka mpya kutembelea hifadhi za Taifa na kujionea wenyewe maajabu na vivutio vilivyopo katika hifadhi hizo.

Ametoa mwito huo alipokuwa akifungua Mkutano Mkuu Maalum wa waandishi wa habari wanachama wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Arusha (APC).

Amesema maeneo ya hifadhi ni urithi ambao watanzania wamepewa bure na Mungu hivyo ni wakati muafaka kwa watanzania kutumia likizo ya mwaka kutembelea hifadhi hizo na kupata mapumziko sahihi.

Amesema hifadhi ya ziwa Manyara ni miongoni mwa hifadhi zenye vivutio vingi ambavyo watanzania wanapaswa kuviona badala ya kuachia wageni pekee waweze kutembelea hifadhi hizo.

" Hifadhi ya Manyara ni moja ya hifadhi rahisi sana kufikika, ukiwa Arusha mjini ni kilometa chache sana unaweza kutumia hadi kufika katika hifadhi yetu na gharama zetu ni ndogo sana,"amesema.

Awali akimkaribisha Mhifadhi wa Manyara, Mwenyekiti wa APC, Claud Gwandu amesema waandishi wa habari ni miongoni mwa wadau wakubwa wanaopaswa kutembelea hifadhi za Taifa na kuzitangaza.

Amesema Waandishi wa habari ni miongoni mwa waandishi ambao wamekuwa wakitoa kipaumbele kutangaza hifadhi za Taifa na kwamba mbali ya kufanyika kwa mkutano huo pia wamepata fursa ya kutembelea hifadhi ya ziwa manyara na lengo ni kutangaza vivutio vilivyopo.

" Mhifadhi napenda kukuhakikishia kuwa mara baada ya mkutano huu tumejipanga kutangaza hifadhi ya Manyara kupitia vyombo mbalimbali vya habari, hapa tuko waandishi zaidi ya 40 kwa hiyo tegemea kuona habari nyingi katika vyombo nyetu vya habari,"amesema.
Mhifadhi utalii Hifadhi ya Ziwa Manyara Ahmed Nassoro akizungumza na waandishi wa habari wanachama wa klabu ya waandishi wa habari Arusha waliotembelea hifadhi hiyo
Kaimu Kamishna wa uhifadhi hifadhi ya Taifa Ziwa Manyara, Neema Mollel akiwa katika picha ya pamoja na waandishi wa habari wanachama wa klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Arusha
Waandishi wa habari wanachama wa klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Arusha wakiwa pembezoni mwa ufukwe wa hifadhi ya ziwa Manyara
Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Arusha Claud Gwandu akihutubia waandishi wa habari kwenye mkutano wa mabadiliko ya katiba katika mkutano uliofanyika ndani ya hifadhi ya Taifa ya ziwa Manyara
Mratibu wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Arusha Seif Mangwangi akiwasilisha maeneo ya katiba  yanayopendekezwa kufanyiwa mabadiliko kwenye mkutano mkuu maalum uliofanyika katika hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara




By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post