Zimwi la ajali lilivyomaliza watu Mbeya mwaka 2022 |Shamteeblog.



AJALI haina kinga, wahenga walisema. Lakini kinachotokea kwenye mteremko wa Inyala, milima ya Iwambi, Nyoka, Igawilo na Uwanja wa Ndege yanafikirisha pale unaporejea msemo huu.

Maeneo hayo ni machache kwa kuyataja lakini yamejaa matukio ya ajali mbaya ambazo zimegharimu maisha ya watu na mali zao katika Mkoa wa Mbeya.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Jeshi la Polisi, zaidi ya watu 40 walipoteza maisha katika kipindi cha miezi sita iliyopita na wengine zaidi ya 120 walipata majeraha kutokana na ajali katika kipindi kama hicho.

Kwa mujibu wa Jeshi la Polisi, sababu  za ajali katika maeneo hayo zimetokana nani mwendo kasi, uzembe wa madereva, ulevi, ubovu wa miundombinu na ufinyu wa barabara.

ENEO LA INYALA

Wakati eneo la Inyala likiongoza kwa ajali, maeneo mengine, Mlima Nyoka, Iwambi, Igawilo na Kawetere  yanafuatia, takwimu zinaonyesha kwamba  maeneo hayo kwa ujumla wake kumetokea ajali zaidi ya 120  zilizosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Benjamini Kuzaga anasema kuanzia  Juni mpaka Septemba mwaka 2022, eneo la Inyala pekee limesababisha vifo vya watu zaidi ya 30 kutokana na ajali za barabarani zilizotokea katika eneo hilo.

Anasema ajali nne mfululizo zilizotokea katika mteremko huo uliopo katika Kijiji cha Shamwengo, Kata ya Inyala wilayani Mbeya ikiwamo ajali iliyoikumba gari la Serikali lililokuwa limembeba Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Igunga mkoani Tabora, Fatuma Omary na dereva wake ambao walifariki dunia papo hapo.

Kuzaga anasema kuwa ajali ya pili ilitokea katika eneo hilo la Inyala ni ile iliyohusisha magari matatu likiwamo la abiria likitokea jijini Mbeya kuelekea Mbarali  liliparamiwa na lori la mizigo lililokuwa limebeba mahindi na kusababisha vifo vya watu watano papo hapo na wengine zaidi ya 10  kujeruhiwa.


“Katika eneo hilo la Inyala pekee tumepoteza Watanzania wetu zaidi ya 30 kutokana na ajali za barabarani., Ajali hizo zilitokea kutokana na sababu mbalimbali, ikiwemo ubovu wa vyombo vyetu vya usafiri, ufinyu na ubovu wa miundombinu ya barabara katika eneo hilo na madereva kutozingatia sheria za usalama barabarani,” anasema ACP Kuzaga.

Anasema chanzo kingine cha ajali ni mwendo kasi kasi, na kwamba Jeshi la Polisi limechukua hatua mbalimbali kwa lengo la kupunguza au kumaliza kabisa ajali katika eneo hilo.

Anasema miongoni mwa hatua ambazo zimechukuliwa naPolisi ni kuanzisha utaratibu wa kupitisha magari eneo hilo kwa awamu ikiwa ni mkakati wa muda mfupi wakati Serikali ikiendelea na utekelezaji wa hatua za muda mrefu wa kuboresha miundombinu ya barabara katika eneo hilo.

Anasema Polisi pia liliishauri Serikali kuhusu umuhimu wa kuwepo kwa njia mbadala ya kupitisha magari katika eneo hilo ili kupunguza madhara.


Anasema ushauri huo ulizingatiwa na Serikali kupitiakwa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) ambao ulijenga barabara ya mchepuko katika eneo hilo kupitisha magari madogo pamoja na mabasi ili yasiongozane namalori ambayo yamekuwa na matukio ya kushindwa kupanda mlima na kurudi nyuma kugonga magari mengine na kusababisha ajali.

Meneja wa TANROAD Mkoa wa Mbeya, Mhandisi  Matari Masige anasema katika kukabiliana na ajali eneo la Shamwengo serikali imetoa sh bilioni mbili kwa ajili ya ujenzi barabara ya mchepuko.

Anasema lengo la kujenga barabara kupitisha magarimadogo na ya abiria ili kupunguza msongamano na kuepusha ajali zinazosababishwa na kufeli breki na hitilafu nyingine barabarani.

“Barabara hii ina urefu wa kilomita  2.8  tayari matengenezo yameanza kwenye barabara hii ya mchepuko  magari madogo na ya  abiria yatapita wakati tukiendelea kuboresha zaidi  kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama na kuleta utulivu kwa wasafiri na madereva wa vyombo vya moto wanapopita eneo hili,” anasema Mhandisi Masige.


ENEO LA IWAMBI

Novemba 9 majira ya saa moja asubuhi watoto wawili wa familia moja walifariki dunia  papo hapo na watu wengine watatu kujeruhiwa katika ajali ambayo ilihusisha basi dogo la abiria linalofanya safari zake kati ya Mbeya na Sumbawanga ambalo limefeli breki na kuyangoga magari mengine matatu kwenye mteremko wa Iwambi, barabara kuu ya Tanzania na Zambia (TANZAM),  eneo la Mbalizi nje kidogo ya Jiji la Mbeya.

Ajali hiyo imetokea baada ya basi hilo mali ya kampuni ya Mangare lenye namba za usajili T 601 DXC kuyagonga magari mengine matatu na kusababsha vifo vya watoto hao.

Waliopoteza maisha katika ajali hiyo ni wanafunzi wa kidato cha pili ambao ni  Maria Alute (15), mwanafunzi wa Shule ya Sekondari St. Francis na Halima Mwaijumba (14) mwanafunzi  wa Shule ya Sekondari Pandahill zote za Mkoa wa Mbeya.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Benjamin Kuzaga anasema chanzo cha ajali hiyo ni mwendo kasi wa dereva wa basi.

Anasema bsi hilo likiwa kwenye mteremko wa Iwambi liligonga gari lingine dogo lenye namba za usajili T 452 DHD aina ya Toyota Raum ambamo kulikuwa na watu watano.


WADAU WAZUNGUMZA

Mkurugenzi wa Mabalozi wa Usalama Barabarani Tanzania (RSA),Augustus  Fungo anasema moja ya mikakati ya kupunguza ajali za mara kwa mara ni kufanyika  mabadiliko ya Sheria  ya Usalama Barabarani  ya mwaka 2021.

Anasema mbalimbali zimeanza kuchukuliwa kama vile kufanya uchechemuzi, ushawishi wa kuainisha mapungufu na uhitaji wa sheria imara ambayo itaongeza uwajibikaji kwa wahusika.

Miongoni mwa dosari za katika sheria hiyo ni  adhabu ndogo kwa anayesababisha ajali na vifo kwa sasa dereva anayesababisha kifo na kujisalimisha polisi hulazimika kulipa faini ya sh 30,000.

Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mbeya, wanasema ili kukabiliana na ajali za mara kwa mara eneo la Inyala, Serikali ijenge barabara imara ambazo zitawezesha magari kupita bila vikwazo.

Joyce Baltazary anaiomba Serikali kuharakisha upanuzi wa barabara katika eneo hilo ili kuepusha ajali za mara kwa mara ambazo zimekuwa zinagharimu maisha ya watu.

Anasema licha ya kuanzisha ujenzi wa barabara ya mchepuko ambayo imepangwa kupitisha magari madogo na abiria lakini  sio ufumbuzi wa kudumu kwani barabara iliyopo ambayo inapitisha malori kwa sasa inahitaji kufumuliwa na kujengwa upya.

“Tatizo lililopo eneo hilo ni kwamba mteremko ni mkali na barabara ni nyembamba hali ambayo inasababisha  malori yanayofeli breki yashindwe kupita bila kusababisha madhara,” anasema Samwel.

“Tatizo lililopo eneo hilo ni kwamba mteremko ni mkali na barabara ni nyembamba hali ambayo inasababisha  malori yanayofeli breki yashindwe kupita bila kusababisha madhara,” anasema Samwel.

Atupakisye Mbumi  anasema pamoja na kuboresha miundombinu ya barabara, pia mchakato wa mafunzo ya udereva na utoaji wa leseni upitiwe upya ili kuwapata madereva wenye weledi, waadilifu na maarifa ya kutosha wawapo na vyombo vya moto barabarani.

“Nadhani hata utaratibu wa kuwapata madereva unapaswa kuangaliwa upya, mafunzo yaboreshwe na pia utoaji wa leseni uwekewe vigezo ambavyo vinamlazimisha dereva yeyote kutii sheria za barabarani nadhani hili nalo litasaidia kupunguza ajali,” anasema Atupakisye.

Mwalyego, anahusisha  ajali zilizotokea eneo la Shamwengo na imani za kishirikiana akidai kuwa yeye ni dereva wa muda mrefu na amepita maeneo mbalimbali nchini hayo ya  ubovu wa barabara au ufinyu haviwezi kuwa chanzo cha ajali eneo hilo.

Anasema kuna kazi ya ziada kufanya eneo hilo ilikumaliza kabisa ajali ikiwemo kufanya maombi kwa Mungu au matambiko kwa imani za watu kukabiliana na ajili eneo la Inyala.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Ramadhan Ng’anzi, kipindi cha kuanzia  Januari mpaka  Novemba mwaka huu Watanzania 886 wamepoteza maisha kutokana na ajali za barabarani.

 Watu 573 wamepata majeraha na ulemavu wa kudumu  kwenye ajali  1,422 zilizoripotiwa Jeshi la Polisi, ambazo ni sawa na ongezeko la ajali 11 zilizoripotiwa mwaka 2021 ambapo zilikuwa ajali 1,411 zilizoua watu 1,008 na kujeruhi 1496.

“Wajibu wetu ni kusimamia sheria za usalama barabarani na kutenda haki na kuzingatia maadili  ya kazi zetu, tuna kazi ya kutazama upya  baadhi ya sheria ambazo zinakwamisha jitihada za kukabiliana na ajali, naamini itatusaidia,” anasema Ng’anzi.

Mwisho.




from Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post