Katika kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya sita katika kuhudumia wananchi, Wafanyakazi wa benki ya NMB kutoka matawi ya Chato na Sengerema wametoa msaada wa magodoro 50 katika gereza la wilaya ya Chato pamoja na kompyuta moja na UPS kwa gereza la Kasungamile wilayani Sengerema .
Akizungumza wakati wa hafla fupi ya makabidhiano hayo yaliyofanyika katika gereza la Kasungumile wilayani Sengerema, Meneja wa benki ya NMB - Stanley Betty alisema benki ya NMB tawi la Sengerema ilipokea ombi la hitaji ya kompyuta kutoka uongozi wa gereza la Kasungamile na benki yao ikaona ifanikishe ombi hilo.
"Benki yetu ya NMB itaendelea na juhudi mbali mbali za kuunga mkono Serikali ya awamu ya sita katika kuleta maendeleo" alisema Betty.
Amepongeza watumishi wa gereza la Kasungamile kwa kuendelea kutumia huduma za benki ya NMB.
Naye Kaimu Mkuu wa Gereza la Kasungamile - Hiyari Mwaijombe alishukuru sana benki ya NMB kwa msaada wao.
"Kompyuta tuliyopewa itaturahishia katika kazi zetu za kila siku ikiwemo kuwaandalia wafungwa rufaa pamoja na mahitaji yao mengine mbali mbali" alisema Mwaijombe.
Aliongezea kuwa inawaomba benki ya NMB iweze kuwasaidia uhitaji wa matenki mawili yenye ujazo wa lita 5000 kwajili ya kutunzia maji katika gereza lao na upatikanaji wa taulo za kike kwa wafungwa sita wanawake waliopo katika gereza la Kasungamile.
Naye, Meneja wa benki ya NMB Wilaya ya Chato - Baraka Nyagwaswa ameshukuru uongozi wa gereza la Chato kwa kupokea msaada wa magodoro 50 kutoka benki ya NMB.
"Kwa hapa Chato sisi ni wenyeji sana na tunajiona wenyeji zaidi kwa kutambua kuwa tunatambulika na kushirikishwa katika masuala muhimu kwa maendeleo,ushirikiano huu ndio unatafanya kuwa benki yenye kujali umuhimu wa masuala ya jamii" alisema Nyagwaswa.
Aliahidi kuwa benki ya NMB itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau wake wakubwa katika kuhakikisha kuwa changamoto za jamii zinapatiwa ufumbuzi katika kujenga afya na elimu bora kwa jamii ya Tanzania.
Aidha, Mkuu wa Gereza la Wilaya ya Chato, Raphael Magesa ameishukuru benki ya NMB na kuwaomba pia Wadau wengine iwasaidie magodoro mengine zaidi, vyakula na sabuni kwani wafungwa na mahabusu wanauhitaji huo.
By Mpekuzi
Post a Comment