MAPINDUZI CUP 2023: YANGA, SIMBA HAKUNA KUCHEKANA… |Shamteeblog.
Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
WATANI wa jadi, Yanga na Simba hawatachekana baada ya wote kutupwa nje ya mashindano ya Kombe la Mapinduzi 2023 wakiwa katika makundi tofauti ya mashindano yote yanayoendelea visiwani Zanzibar.
Bingwa mtetezi, Simba SC alikuwa wa kwanza kutupwa nje ya mashindano hayo akiwa katika Kundi C lenye timu za Mlandege na KVZ, Simba SC alitupwa nje ya mashindano hayo baada ya kufungwa mchezo wa kwanza dhidi ya Mlandege, Mnyama alifungwa bao 1-0 kwenye dimba la Amaan.
Mchezo wa pili na wa mwisho wa mashindano hayo kwa Simba SC, ulikuwa mchezo wa kukamilisha ratiba licha ya Mnyama kushinda bao 1-0 kwenye uwanja huo huo wa Amaan, bao la Simba SC lilifungwa na Mshambuliaji kinda Michael Joseph.
Simba SC walikusanya alama tatu pekee kwenye Kundi C huku KVZ akiwa na alama moja pekee na Mlandege amepata faida ya kufuzu hatua ya Nusu Fainali ya mashindano hayo kwa alama zao nne walizokusanya kwenye michezo miwili.
Kwa upande wa Yanga SC wameaga mashindano hayo ya Kombe la Mapinduzi 2023 licha ya kuwa alama sawa na Singida Big Stars katika Kundi B, mchezo wa kwanza Yanga SC walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya KMKM, bao la Wananchi lilifungwa na Mshambuliaji Dickson Ambundo dakika za lala salama.
Mchezo wa pili dhidi ya Singida Big Stars, Wananchi wamepata sare ya bao 1-1, hivyo Singida BS wamepata faida ya kufuzu hatua ya Nusu Fainali kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa. Singida BS wamepata alama nne na Yanga SC wamepata alama nne. KMKM wamekosa alama yoyote.
Nusu ya kwanza ya mashindano hayo, Azam FC watakabiliana na Singida Big Stars kwenye dimba la Amaan, Januari 8, 2023 huku Namungo FC watakuwa na kibarua dhidi ya Mlandege kwenye Nusu Fainali ya pili itakayofanyika kwenye uwanja huo huo wa Amaan, Januari 9, 2023.
By Mpekuzi
Post a Comment