BINGWA Mtetezi, Timu ya taifa ya Morocco imejitoa kwenye Michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika, kwa Wachezaji wanaocheza Ligi za nyumbani (CHAN 2023) baada ya Waandaji wa Michuano hiyo kukataa Ndege iliyokuwa inasafirisha timu hiyo kutua moja kwa moja kwenye mji wa Constantine, Algeria kutokea mjini Rabat.
Imeelezwa kuwa, Algeria wamekataa kuruhusu Ndege hiyo ya Morocco kufika moja kwa moja kwenye mji wa Constantine ambapo timu hiyo imepangwa kucheza huko katika Kundi C, sababu kubwa ikitajwa kuwa ni hali ya uhusiano wa Kisiasa uliopo baina ya nchi hizo mbili.
Desemba mwaka jana, Morocco walitishia kujitoa kwenye Michuano hiyo endapo wangekataliwa ombi lao na walipeleka maombi kwenye Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) kuomba Shirika lao la Ndege la ‘Royal Air Maroc (RAM)’ kuwasafirisha moja kwa moja hadi Constantine, lakini Mamlaka za nchini Algeria zilikataa ombi hilo.
Nchi hizo mbili zilivunja uhusiano wa Kidiplomasia mnamo Agosti, 2021 na hivyo kupelekea kufunga Anga na safari zote za moja kwa moja za Ndege kati yao kusimamishwa. Katika Michuano hiyo, ambayo inaanza Junuari 13, 2023, Algeria itamenyana na Libya katika mchezo wa ufunguzi, huku Morocco ikitarajiwa kuanza kutetea taji lao Jumapili dhidi ya Sudan lakini Shirikisho la Soka la Morocco (FMRF) limesema hilo halitawezekana.
“Sisi tuliarifiwa mnamo Desemba 22 na CAF, kwamba idhini kimsingi imepatikana, kwa bahati mbaya upataji wa idhini ya mwisho haujathibitishwa na CAF,” imeeleza taarifa ya Shirikisho la Soka nchini Morocco (FMRF).
Hata hivyo, FRMF imewasilisha maelezo ya mpango wa Ndege na kuratibu ili kupata idhini ya mwisho ya safari ya Shirika la Ndege nchini humo (RAM) kutoka Rabat na kuendelea na maandalizi ya safari na ushiriki wao katika Michuano ya CHAN 2023.
Morocco maarufu kwa jina la Simba ya Atlas walipangwa Kundi C pamoja na timu za taifa za Ghana, Madagascar na Sudan, hatua ya kujitoa kwenye Michuano hiyo kutaleta ugumu kwa CAF ambao watalazimika kufanya mashindano bila timu moja kwenye Michuano hiyo.
Morocco walitwaa ubingwa wa Michuano hiyo, Februari 7, 2021 baada ya ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mali kwenye mchezo wa Fainali ya Michuano hiyo uliopigwa katika dimba la Ahmadou Ahidjo nchini Cameroon.
Hata hivyo, Morocco walikuwa tayari wamefanya maandalizi kwa ajili ya Michuano hiyo wakiwa tayari wamecheza michezo miwili ya kirafiki dhidi ya Ethiopia.
Je, timu hiyo kutoka Afrika Kaskazini huenda wakakabiliwa na vikwazo kutoka kwa Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kufuatia kujiondoa kwao kwenye Michuano hiyo…???

By Mpekuzi
Post a Comment