DKT. SAMIA AMWAGA MABILIONI KUINUA FURSA ZA UCHUMI WA BULUU |Shamteeblog.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (wa nne kushoto) akiwa kwenye boti ya uvuvi iliyopewa jina la Mv. Blue Economy na kubainisha mambo kadhaa juu ya uwekezaji wa serikali kwenye Uchumi wa Buluu, mara baada ya kutembelea kikundi cha ushirika cha Mchukuuni kilichopo jijini Tanga ambacho kinajishughulisha na kilimo cha mwani na ufugaji tango bahari ama jina lingine la zamani jongoo bahari.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (wa kwanza kushoto) akiwa kwenye kikundi cha ushirika cha unenepeshaji kaa kiitwacho Jifute kilichopo Wilaya ya Pangani, Mkoani Tanga kujionea namna wanavyojishughulisha na unenepeshaji wa kaa hao pamoja na vizimba vilivyojengwa mahsusi kwa ajili ya kufuga kaa 600 kwa wakati mmoja

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb), (aliyesimama) akiwa kwenye mazungumzo mara baada ya kufika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba (aliyekaa), kabla ya Naibu Waziri Ulega kuanza ziara ya kikazi mkoani humo.

Na. Edward Kondela
Serikali imeendelea kutekeleza bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 katika uwekezaji wa uchumi wa buluu kupitia maji ya Bahari ya Hindi, maziwa na mito ikiwemo kuhamasisha ufugaji wa viumbe maji.

Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amebainisha hayo (15.02.2023) wakati akiwa kwenye ziara ya kikazi Mkoani Tanga ambapo katika siku ya kwanza ya ziara hiyo, kwenye Sekta ya Uvuvi ametembelea vikundi vya ushirika vya ukuzaji viumbe maji vya Jifute kinachonenepesha kaa pamoja na Mondura na Mchukuuni vinavyojishughulisha na ufugaji wa tango bahari ama kwa jina lingine la zamani jongoo bahari pamoja na ukulima wa mwani.

Ili kukuza uchumi wa buluu, Naibu Waziri Ulega amesema serikali imeweka Shilingi Bilioni 2.5 kwa ajili ya kuendeleza zao la mwani ambapo tayari Shilingi Milioni 447 zimeshatolewa kwa vikundi mbalimbali, Shilingi Bilioni 11.5 zimetengwa kwa ajili ya kutengeneza boti za kisasa za uvuvi na Shilingi Bilioni 20 kwa ajili ya ujenzi wa vizimba vya kufugia samaki aina ya sato kwenye Ziwa Victoria.

Mhe. Ulega amesema serikali inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejizatiti kuinua uchumi wa buluu kwa kutenga fedha nyingi huku wadau mbalimbali wa sekta hiyo wakikaribishwa kuunga mkono juhudi za Rais Dkt. Samia kuweka mazingira mazuri ya ukuzaji viumbe maji.

Aidha, amewataka wadau wa Sekta ya Uvuvi hususan vikundi vya ushirika vya wavuvi kuchangamkia fursa ambayo serikali imetoa fedha ili kuongeza mahitaji ya ukuzaji viumbe maji kutokana na masoko yaliyopo ndani na nje ya nchi.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Pangani Mhe. Zainabu Abdallah amesema anafurahishwa na namna Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inavyoweka juhudi za kuwasaidia vijana katika uwekezaji kwenye viumbe maji kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kutaka uwekezaji wa kisasa kwa kuongeza mnyoyoro wa thamani, huku akibainisha kuwa wilaya yake iko tayari kutenga maeneo mengi zaidi kwa ajili ya shughuli za ukuzaji viumbe maji.

Akisoma risala ya kikundi cha ushirika cha kilimo cha mwani na ufugaji tango bahari cha Mchukuuni kilichopo jijini Tanga, Bw. Abdallah Mtondo amelalamikia kitendo cha baadhi ya watu ambao siyo waaminifu kuiba matango bahari katika mashamba yao hususan nyakati ambapo maji yamefunika mashamba hayo.

Kutokana na hali hiyo wameiomba serikali kuwachukulia hatua za kisheria watu hao ambao wamekuwa wakiwarudisha nyuma katika shughuli za ufugaji ili kujiongezea tija jambo ambalo Naibu Waziri Ulega amelitolea kauli kali na kutaka mamlaka husika kuingilia kati jambo hilo huku akisisitiza wanunuzi wa mwani na tango bahari kununua mazao hayo kwenye vikundi vinavyotambulika na kusajiliwa.

Awali kabla ya kuanza ziara ya kikazi Mkoani Tanga, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega (Mb) amefika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga Mhe. Omary Mgumba na kufanya naye mazungumzo juu ya namna serikali kupitia wizara hiyo inavyofanya jitihda mbalimbali za kufungua fursa kwa wadau wa sekta za mifugo na uvuvi kwa kufuga na kuuza mazao yanayotoka katika sekta hizo.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post