Kocha Mkuu wa US Monastir ya Tunisia Darko Novic amesema wapo tayari kuikabili Young Africans kwenye mchezo wa Mzunguuko wa Kwanza wa Kundi D, Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
US Monastir itaanzia nyumbani Stade Hammadi Agrebi, mjini Tunis, Februari 12 majira ya saa kumi na moja jioni kwa saa za Tunisia.
Kocha Novic amesema dhamira yao kuu ni kuhakikisha wanaanza vizuri michuano hiyo kwa kuifunga Young Africans, ambayo amekiri ina kikosi kizuri chenye uwezo wa kucheza popote Barani Afrika.
Amesema wanajiandaa kuelekea mchezo huo na wameifuatilia Young Africans kwa ukaribu na kubaini baadhi ya mbinu wanazotumia wanapokua nje na ndani ya Uwanja, hivyo itakua rahisi kwao kukabiliana nayo wakiwa nyumbani kwao Tunisia.
“Tunahitaji kuanza vizuri Kombe la Shirikisho Barani Afrika Hatua ya Makundi, tunaanzia nyumbani na tutahitaji kushinda mchezo huo dhidi ya Young Africans,”
“Tunafahamu Young Africans ina kikosi kizuri na inaweza kupambana popote Afrika, ndio maana tumeanza kujiandaa kukabiliana nayo, tunaamini tutaweza kujipanga na kupata ushindi tukiwa nyumbani.”
“Tunawafuatilia kwa ukaribu na kuona baadhi ya mbinu zao wanazozitumia katika michezo yao, siwezi kusema tunatumia mbinu gani kuwafuatilia, lakini naamini hata wao wanatufuatilia ili watufahamu kabla hatujakutana.” amesema Kocha Darko Novic
Young Africans ilijihakikishia kucheza Hatua ya Makundi Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kuifunga Club Africain ya Tunisia 1-0 mjini Tunis-Tunisia.
Kundi D la michuano hiyo lina timu za TP Mazembe (DR Congo), Real Bamako (Mali), US Monastir (Tunisia) na Young Africans (Tanzania).
from Author
Post a Comment