MBUNGE wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina ameitaka serikali kubadili mfumo kwa baadhi ya ajira za viongozi ikiwamo Mawaziri zinazopatikana kwa uteuzi ziwe za ushindani ili kupata viongozi wasiotiliwa shaka.
MBUNGE wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina.
Akiuliza maswali ya nyongeza bungeni jana, Mpina alihoji: "Kwanini serikali isiachane na baadhi ya ajira kupatikana kwa uteuzi badala yake ajira zote zipatikane kwa ushindani ajira za viongozi, ajira za watendaji, mawaziri, makatibu wakuu, wakurugenzi ili kuiwezesha serikali kupata viongozi wenye uwezo usiotiliwa shaka katika nafasi mbalimbali za serikali."
Pia alihoji mkakati wa dharura wa serikali kudhibiti biashara holela, uingiaji wa mikataba mibovu na usimamizi hafifu wa sheria kutokana na kusababisha ajira nyingi za Watanzania kupotea.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi - Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Patrobas Katambi alisema kwa sasa Katiba ya mwaka 1977 inaeleza namna ya mfumo na uendeshaji wa serikali na inatambua kuwapo ajira zinazopatikana kwa ushindani na uteuzi.
Alisema serikali kupitia vyombo vyake imekuwa ikichukua hatua katika kuimarisha vyombo vinavyosimamia sheria ikiwamo mahakama, polisi, TAKUKURU na kuchukua hatua kwa wanaoingiza serikali kwenye mikataba mibovu.
"Serikali ina mahakama maalum ya kuchukua hatua kwenye makosa ya kiuchumi na moja wapo ni kudhibiti mambo haya," alisema.
Katika swali la msingi, Mpina alihoji ni vijana wangapi hawana ajira nchini na serikali imewaandaaje kushindana katika soko la ajira ndani na nje ya nchi.
Akijibu swali hilo, Katambi alisema utafiti wa watu wenye uwezo wa kufanya kazi wa mwaka 2021 unaonyesha vijana wenye umri wa miaka 15-35 ambao wana ukosefu wa ajira ni 1,732,509.
"Idadi hiyo ni sawa na asilimia 12.2 ya nguvu kazi ya vijana 14,219,191 wenye uwezo wa kufanya kazi kwa maana ya vijana walio katika umri huo na hawapo katika mafunzo au hawana ulemavu unaosababisha wasijishughulishe na shughuli za kiuchumi," alisema.
Katambi alisema katika kuhakikisha vijana wanaandaliwa ipasavyo kushindana katika soko la ajira la ndani na nje, serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Kukuza Ujuzi wa Miaka 10 (2016/2017–2025/2026).
Alisema kupitia mkakati huo, serikali imefanya maboresho ya miundombinu na mitaala katika ngazi za Elimu ya Juu, Elimu ya Kati na Mafunzo ya Ufundi Stadi.
"Sambamba na maboresho hayo, serikali inatoa mafunzo ya kuwezesha vijana walio nje ya mfumo rasmi wa mafunzo ili kumudu ushindani katika soko la ajira yakiwamo mafunzo ya uanagenzi," alisema.
Pia alisema yanatolewa mafunzo ya uzoefu wa kazi kwa wahitimu, mafunzo ya urasimishaji ujuzi uliopatikana nje ya mfumo rasmi wa elimu na mafunzo na mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya vitalu nyumba.
from Author
Post a Comment