Na Muhidin Amri, Tunduru
WAKALA wa barabara za mijini na vijijini Tanzania(Tarura)wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,imeanza kufungua barabara mpya zinazounganisha vijiji vya pembezoni na mji wa Tunduru ili kuwawezesha wananchi kusafiri na wakulima kusafirisha mazao yao kwa urahisi kutoka shambani hadi sokoni.
Barabara hizo zinatajwa zinakwenda kuhamasisha uzalishaji,kuongeza thamani ya mazao na kipato kwa wakulima na kuchochea kukua kwa uchumi wa wilaya ya Tunduru,mkoa wa Ruvuma na Taifa.
Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Tarura wilayani Tunduru Msola Julius,wakati akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara mpya yenye urefu wa km 3.5 inayounganisha kijiji cha Kidugalo kata ya Mchangani na katikati ya mji wa Tunduru.
Alisema kwa mwaka wa fedha 2022/2023 Tarura imetenga shilingi milioni 100 kutoka mfuko wa barabara kwa ajili ya kuifungua barabara hiyo ambayo awali haikuweza kupitika kwa urahisi kutokana na kuwa na makorongo na mabonde.
Alisema,kwa muda mrefu wananchi wa Kidugalo hawakuwa na mawasiliano ya barabara ya uhakika,lakini sasa serikali kupitia wakala wa barabara za mjini na vijijini(Tarura)imeanza mpango wa kufungua barabara mpya na kufanya matengenezo barabara za zamani ili kutoa fursa kwa wananchi wazitumie katika shughuli zao za kila siku.
Aidha alisema,kwa muda mrefu wilaya ya Tunduru ilikuwa na changamoto ya barabara za uhakika ,lakini baada ya kuanzishwa kwa Tarura miaka minne iliyopita na tangu Rais Dkt Samia Suluhu Hassan alipoingia madarasani barabara nyingi katika wilaya hiyo zimefunguliwa na kutengenezwa.
Mwenyekiti wa kitongoji B cha Mchangani kata ya Mchangani Hausi Bilal alieleza kuwa,awali barabara hiyo haikuweza kupitika kwa urahisi kutokana na ubovu,badala yake wananchi walilazimika kutumia usafiri wa baiskeli tu na wakulima kubeba mazao kichwani.
Alisema,hali hiyo ilisababisha wananchi hasa wa kijiji cha Kidugalo kusafiri kwa shida kwenda maeneo mengine ya wilaya ya Tunduru kufuata huduma mbalimbali za kijamii na wakulima kushindwa kupeleka mazao yao sokoni kwa wakati.
Baadhi ya wananchi wa kijiji cha Kidugalo hususani wakulima, wameishukuru Tarura kuanza matengenezo ya barabara hiyo ambayo ni tegemeo kubwa kwao kwa ajili ya kusafirisha mazao kufika sokoni.
Dastan Msilasi mkazi wa mtaa wa Mkwanda alisema,matengenezo ya barabara ya Mchangani-Kidugalo imemaliza kilio cha muda mrefu cha mawasiliano ya uhakika na kuipongeza serikali kuitengea Tarura fedha za kutosha kwa ajili ya matengenezo barabara hiyo.
Ali Yusufu alisema,mawasiliano kati ya kijiji cha Kidugalo na maeneo mengine ya mji wa Tunduru hayakuwepo baada ya kukatika kwa barabara,lakini tangu Tarura ilipoanza matengenezo takribani siku tatu zilizopita wananchi wameanza kunufika na wakulima wataitumia barabara hiyo kuuza na kusafirisha mazao yao kwa wakati muafaka.
MWISHO.
Muonekano wa barabara mpya ya Kidugalo-Mchangani yenye urefu wa kilomita 3.5 inayotekelezwa na wakala wa Barabara za mijini na vijijini Tanzania(Tarura) kwa gharama ya shilingi milioni 100,Barabara hiyo imeanza kurudisha mawasiliano kwa wananchi wa Kidugali na maeneo mengine ya mji wa Tunduru.
Katapila likiendelea na matengenezo ya barabara mpya ya Kidugalo-Mchangani kata ya Mchangani Halmashauri ya wilaya Tunduru ili kurudisha mawasiliano ya wananchi wa kijiji cha Kidugalo na mji wa Tunduru.
By Mpekuzi
Post a Comment