WAHANDISI 40 GGML WAFANYA ZIARA YA MAFUNZO DARAJA LA KIGOGO- BUSISI |Shamteeblog.

 Na Mwandishi Wetu

WAHANDISI 40 kutoka Kampuni ya Geita Gold Mining Limited (GGML) wametembelea daraja la Kigongo-Busisi linalounganisha mikoa ya Mwanza na Geita kwa lengo la kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu mambo mapya kuhusu sayansi, teknolojia na uvumbuzi unaotumika sasa dunia kwenye sekta ya ujenzi.

Ziara hiyo ambayo ni sehemu ya mipango ya Kampuni ya GGML kuendeleza wafanyakazi wake kupitia ziara mbalimbali za kimafunzo kwenye miradi mikubwa ya kihandisi, imefanyika mwishoni mwa wiki.

Akitoa maelezo kwa wahandishi hao kutoka GGML, Mhandisi Abdukarim Majuto kutoka kundi la Makampuni ya Ushauri wa mradi wa ujenzi wa daraja hilo la Kigongo – Busisi alisema mradi huo umetumia teknolojia ya hali ya juu inayotumiwa na wahandisi duniani kote.

Alisema teknolojia inayotumika katika ujenzi wa miradi mikubwa chini ya maji ni moja ya kivutio cha kutembelea eneo la Daraja la Kigongo Busisi.

“Daraja lina urefu wa kilometa 3.2 katika Ghuba ya Mwanza na kuunganisha Kigongo mkoani Mwanza na Busisi mkoani Geita, ni moja ya maeneo ya kuvutia zaidi nchini,” alisema.

Ziara hiyo iliyohudhuriwa na vikundi vya mafundi wakiwemo wahandisi wa mitambo, umeme na viwanda, wasimamizi wa miradi, mafundi mekanika na wakuchomelea vyuma.

Aidha, Meneja wa Miundombinu wa GGML, Eliakim Kagimbo, alifichua kuwa Kampuni inapenda kutumia daraja hilo kama jukwaa la kujifunzia ili kupata maarifa ya kina juu ya vipengele vya kiufundi vya mradi mzima.

“Tunafuraha kuona daraja hili linajengwa karibu na tunakofanyia shughuli zetu. Kama unavyojua, GGML imetekeleza miradi kadhaa ya uhandisi kwa miaka mingi na daraja hili linatoa fursa kwetu kuboresha ujuzi wetu,” alisema.

Kwa upande wake Msimamizi wa Ujenzi wa TANROAD katika daraja hilo Mhandisi William Sanga, alikaribisha ziara hiyo ya mafunzo na kubainisha kuwa kukamilika kwa daraja hilo ni suala muhimu katika utekelezaji wa programu ya maendeleo ya nchi.

“Daraja la Kigongo–Busisi litakuwa kiungo muhimu kati ya Mwanza na mikoa ya jirani pamoja na nchi jirani. Kwa hivyo lina uwezo wa kuchochea ukuaji wa uchumi katika eneo hilo. Daraja hili litapunguza kiasi kikubwa cha foleni katika njia hii na pia kuboresha usalama wa watumiaji katika kivuko cha ziwa hili," alisema.

Tangu kuanzishwa kwake, GGML imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na mamlaka za serikali za mitaa kusaidia miradi kadhaa ya jamii katika mkoa wa Geita kupitia Ubia kati ya Sekta ya Umma na Sekta Binafsi pamoja na programu za kitaifa.Mhandisi Abdukarim Majuto kutoka kundi la Makampuni ya Ushauri wa mradi wa ujenzi wa daraja hilo la Kigongo – Busisi, akitoa maelezo ya mradi huo kwa Wahandisi na watalaam mbalimbali kutoka GGML.






By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post