Binti atupa kichanga chooni hospitalini akihofia kuachika |Shamteeblog.




Katavi. Rehema Erick (19) mkazi wa Kijiji cha Mtapenda Halmashauri ya Nsimbo ametupa mtoto chake kichanga cha siku moja chini ya sinki la kunawia mikono kwenye choo cha hospitali ya Nsimbo muda mfupi baada ya kujifungua, akihofia kuachwa na mume wake.

Akisimulia kisa hicho leo, Alhamisi Januari18, 2024 Kaimu Mganga Mfawidhi wa hospitali ya halmashauri hiyo, Glory Solo amesema Rehema alifika hospitalini hapo akilalamika anasumbuliwa na maumivu ya tumbo.

Amesema daktari aliyemuona alimwandikia baadhi ya vipimo na baadaye Rehema alitoweka pasipo kufahamu alikoelekea jambo lililomfanya ndugu yake aliyempeleka hospitalini hapo naye kuanza kumtafuta.

"Kumbe aliingia chooni akawa amejifungua huyu mtoto na kisha alitoa kondo la nyuma na akamfunika mtoto kwenye kanga aliyokuwa nayo na kumsukumia nyuma ya sinki.

"Sisi tumegundua baada ya kumuona anatoka chooni akiwa anavuja damu nyingi, tulianza kumhudumia bila kujua baadaye watu walimleta mtoto wakadai ametupwa chooni, tulimuuliza akakana siyo wake," amesema Glory na kuongeza:

“Baadaye tulipoangalia mazingira yake ikiwemo kumhoji kwa kuwashirikisha Ustawi wa Jamii na vyombo vya sheria alikubali mtoto ni wake”.

Amesema madhara aliyopata mtoto kutokana na kuzaliwa katika mazingira hatarishi ni michubuko na amevunjika miguu yote miwili sehemu za mapaja.


Hata hivyo amesema mama na mtoto wote wanaendelea vizuri na matibabu huku mtoto akinyonya vizuri.

Rehema Erick anayedaiwa kuhusika na tukio hilo, alipoulizwa kwa nini amefanya kitendo hicho amesema amemtupa mtoto huyo kwa kuwa anahofia kuvunja ndoa yake kwakuwa aliolewa akiwa mjamzito.

"Nikuja kutibiwa juzi kabla ya kupimwa nilimuuliza muuguzi chooni ni wapi akanionyesha nikaenda nikakifungua nikamuacha mtoto kwa sababu niliolewa nikiwa na mimba na mme wangu angenifukuza," amesema Rehema.

Mume wa Rehema, Ramadhan Mrisho amesema baada ya kupata taarifa za tukio hilo ameshangaa uamuzi uliochukuliwa na mkewe kwani hakujua kama ni mjamzito.

"Ni miezi miwili tu tangu nimuoe akitokea Dar es Salaam, nikamchukua sijafunga naye ndoa alinificha maana mimba ilikuwa haionekani na baada ya kumuoa alisema yupo kipindi hatari anaweza kupata ujauzito.

"Nimejitambulisha kwao hatua ya kwanza, maandalizi ya kuchukua mahari yalikuwa yanaendelea, uamuzi wangu kwa sasa nitalea mtoto japo amenisikitisha sana kwa kumtupa," amesema Mrisho.

Ameongeza kuwa baada ya kufika hospitalini hapo hajamkaripia mkewe isipokuwa amemuuliza kama mtoto ananyonya na alijibiwa kuwa anasumbua.

Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Jamila Yussuf amelaani  kitendo hicho  na akitoa onyo kwa wengine kuacha tabia hiyo ya ukatili.


"Serikali haitavumilia kamwe ukaliti wa aina hii, Jeshi la Polisi Mpanda nawaagiza kuchukua hatua kali za kisheria kwa binti huyu na wengine wanaoendekeza vitendo vya kikatili," amesema Jamila.



from Author

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post