MAKOCHA wawili mahiri waliowahi kuifundisha Yanga wameshtushwa na kiwango cha beki wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’, Ibrahim Bacca kwenye michuano ya Afcon. Na wameshangaa kuona kwanini bado anacheza ligi ya ndani.
Kocha Mbelgiji anayeinoa Gambia kwenye Afcon, Tom Saintfiet katika wachezaji wote wa Stars amemuelewa zaidi Bacca kwenye eneo la ulinzi na kutabiri kwamba muda wowote staa huyo atapata ofa Ulaya kwa vile ameonyesha utofauti mkubwa licha ya matokeo ya timu.
Saintfiet ambaye aliinoa Yanga mwaka 2012 kwa muda mfupi, alisema Bacca ni beki anayecheza jihadi wakati wote wa mchezo na kwamba kiwango chake kinastahili awe anajiunga na Stars akitokea klabu kubwa Ulaya au nje ya Afrika.
Saintfiet ambaye jana usiku timu yake ilikuwa inacheza na Cameroon kukamilisha ratiba kwenye Afcon, amekumbusha kiwango cha beki wa zamani wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ lakini akakiri mkongwe huyo amezidiwa na Bacca.
“Nilikuwa nahesabu wachezaji ambao wanatoka nje ya Tanzania, nilipofika kwa yule mwenye jezi namba nne nilishangaa kuona anacheza Yanga, naiheshimu Yanga ni klabu kubwa Tanzania na timu yangu ya zamani lakini huyu beki anatakiwa kucheza nje ya Tanzania hata Ulaya,” alisema Saintfiet.
“Ana tachi nzuri ya mpira lakini muda wote akili yake iko uwanjani kuzuia. Angalia anavyoteleza kuzuia mipira ni beki wa kisasa kabisa ambaye klabu nyingi zingependa kuwa naye,” aliongeza kocha huyo ambaye kabla ya jana usiku timu yake ilikuwa haina pointi hata moja.
Wakati Saintfiet akiyasema hayo kocha Mzambia George Lwandamina ambaye kwa sasa anainoa Zesco, alisema Bacca kucheza na Yanga ni suala la bahati kubwa kwa klabu hiyo.
Lwandamina alisema beki huyo kama angesimama na mshambuliaji Patson Daka aliyeisawazishia Zambia bao asingefunga kirahisi.
“Ni beki ambaye mshambuliaji yoyote hawezi kuwa huru kufanya kazi kwa akili yake, makocha wengi wanapenda kufanya kazi na mabeki wa aina hii, ni bahati sana kwamba bado yupo hapo Yanga lakini alitakiwa kuwa Ulaya.
“Nimemuangalia anatumia miguu yote vizuri hiyo ni faida kubwa kwa beki wa kati hasa anapokuwa mzuri kuruka na kutumia miguu yote inamfanya kuwa tayari kutoa msaada kwa pande zote za pembeni,” alisema Lwandamina ambaye aliikochi Yanga kuanzia 2016-2018.
Huu ni msimu wa pili kwa Bacca Yanga ambaye alijiunga na Yanga akitokea KMKM ya Zanzibar. Mchezaji huyo amekuwa tegemeo kwenye kikosi cha Taifa Stars licha ya kwamba imekuwa na matokeo ya kusuasua baada ya kupoteza dhidi ya Morocco na kutoa sare na Zambia.
from Author
Post a Comment