ZAIDI YA BILIONI 23 KUTUMIKA KUSAMBAZA UMEME KILIMANJARO VIJIJINI |Shamteeblog.


-VIJIJI 506 VIMEUNGANISHWA NA UMEME KATI YA VIJIJI 519 SAWA NA 97.49%

SERIKALI kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) imejipanga kuhakikisha ifikapo Desemba 2024 vijiji vyote 519 Mkoani Kilimanjaro viwe vimeunganishwa na umeme.

Mkurugenzi wa Umeme Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu amebainisha hayo mbele ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa Julai 29 Mkoani Kilimanjaro wakati wa utambulisho wa Wakandarasi walioshinda tenda ya kusambaza umeme katika vijiji 13 vilivyokuwa vimesalia.

"Hadi sasa tumeunganisha umeme katika vijiji 506 kati ya vijiji 519 ambayo ni sawa na asilimia 97.49 Mkoani hapa; na leo hii tupo hapa kutambulisha Wakandarasi watakaotekeleza miradi katika vijiji hivi vilivyosalia," amebainisha Mhandisi Olotu.

Mhandisi Olutu amebainisha kuwa kwa Mkoa wa Kilimanjaro REA inatekeleza jumla ya miradi mikubwa mitatu ambayo ni mradi wa shilingi bilioni 13.1 wa kusambaza umeme vijijini, mradi wa bilioni 8.8 wa kusambaza umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo na mradi wa bilioni 1. 7 wa kusambaza umeme katika vituo vya afya na visima vya maji.

"Tumefika hapa kwa lengo la kutambulisha Wakandarasi watakokamilisha kazi iliyobaki Mkoani hapa sambamba na kutambulisha wasimamizi wake kwa upande wa REA ambao miongoni mwa majukumu walionayo ni kuwasilisha kwako taarifa za mara kwa mara za maendedeleo na hatua za utekelezaji," amefafanua Mhandisi Olotu.

Akizungumza wakati wa utambulisho wa wakandarasi hao; Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro, Kiseo Nzowa ameipongeza REA kwa kuendelea kufanikisha dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuwaletea maendeleo wananchi wake kupitia umeme.

"Umeme ni injini ya uchumi wa taifa lolote duniani na kwakutambua hilo, Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewekeza fedha nyingi katika Sekta ya Nishati na kwa bahati nzuri REA mmetambua vyema dhamira ya Rais na mnatekeleza kwa vitendo," amepongeza Nzowa.

Aidha, amewataka Wakandarasi waliopewa jukumu hilo la kufikisha umeme katika vijiji vilivyosalia kufanya kazi kwa weledi na kwa kasi ili kukamilisha na kukabidhi mradi ndani ya muda uliopangwa.

"Wote mliopewa jukumu ni wazawa; hatutarajii kuona kazi ikikwama; kukitokea changamoto yoyote Ofisi ya Mkuu wa Mkoa ipo wazi kuwasikiliza na kusonga mbele," amesisitiza Nzowa.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Wakandarasi hao waliahidi kufanya kazi kwa weledi, ubunifu na kasi ili kutimiza dhamira ya Serikali.

"Serikali imetuamini kwa kutupa kazi, nasi tunaahidi kuhakikisha hatufanyi makosa; tutatekeleza kazi hii kwa uzalendo ili sote kwa pamoja tutimize dhamira ya Rais wetu," amesema Mhandisi Cuthbert Shirima, Mkandarasi kutoka Kampuni ya Transpower Limited.

Kampuni zilizopewa jukumu la kukamilisha vijiji 13 vilivyosalia Mkoani humo ni Northern Engineering works Ltd (Wilaya ya Hai), Radi Services Ltd (Wilaya ya Hai na Moshi), Transpower Ltd (Wilaya ya Same) na Octupus Engineering Ltd (Wilaya ya Mwanga).



By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post