Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mwaka wa fedha wa 2023/2024 imetoa fedha kwa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi kiasi cha Shilingi bilioni 11.34 kwa ajili ya matengenezo na Shilingi bilioni 2.84 kwa ajili ya miradi ya maendeleo kwa barabara za mikoa.
Kiasi hicho cha takribani shilingi Bilioni 14.18 kilitolewa na Rais Samia kwa TANROADS Mkoa wa Lindi kufanya kazi katika mtandao wa barabara wenye jumla ya urefu wa kilomita 1,289.49 na jumla ya madaraja 367 ambazo zinahudumiwa na TANROADS.
Akizungumzia utekelezaji wa miradi hiyo mara baada ya kutembelea na kukagua maendeleo yake Msimamizi wa Kitengo cha Mipango wa Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Lindi Mhandisi Jastas Mpenihaka amesema kuwa Utekelezaji wa matengenezo ya barabara umekamilika na matengenezo yalifanyika Barabara kuu na barabara za mkoa.
Amesema matengenezo ya kawaida yamefanyika kwa urefu wa kilomita 347.97 kwa gharama ya jumla Shilingi bilioni 3.835, Matengenezo ya muda maalum kilomita 6 kwa gharama ya jumla Shilingi bilioni 2.174, na Matengenezo ya kawaida ya madaraja 30 kwa gharama jumla Shilingi milioni 138.400.
Pia ameseam kuwa katika Barabara za Mkoa Matengenezo ya kawaida yamefanywa katika barabara za lami urefu wa kilomita 48.13 kwa gharama ya jumla Shilingi milioni 274.677 pia Matengenezo ya kawaida yamefanywa katika barabara za changarawe zenye urefu wa kilomita 836.28 kwa gharama ya jumla Shilingi bilioni 2.682.
Mhandisi Mpenihaka ametaja miradi mingine iliyofanyiwa Matengenezo ya muda maalum kwa barabara za changarawe kilomita 100 kwa gharama ya jumla Shilingi bilioni 2.151, Matengenezo ya kawaida ya madaraja 25 kwa gharama jumla ya Shilingi milioni 85.409 na Ukarabati miradi ya maendeleo kwa barabara za mkoa kilomita 32.3 unaendelea kwa gharama ya Shilingi bilioni 2.84.
Kwa upande wake Msimamizi wa Kitengo cha Miradi ya Maendeleo TANROADS Mkoani Lindi Mhandisi Fred Sanga amesema kuwa mvua za El-Nino pamoja na kimbunga Hidaya ziliathiri maeneo mengi katika barabara za mkoa wa lindi ambapo athari kubwa zaidi ilikuwa katika barabara za mikoa na barabara kuu hususani maeneo ya Somanga-Mtama, Mikereng’ende, Mbwemkulu, na Kipwata.
Ameyataja maeneo yaliyoathirika katika barabara za mikoa kuwa ni pamoja na Liwale-Nachingwea, Kiranjeranje-Namchiga pamoja na Tingi-Kipatimo ambapo serikali ilichukua hatua za haraka kurejesha mawasiliano kwa kutoa Bilioni 13 katika urejeshaji wa miundombinu katika maeneo yaliyoathirika katika barabara kuu huku katika barabara za mikoa zikitolewa Bilioni 6.
Kuhusu barabara ya mchepuko ambayo imekamilika kwa kujengwa kwa kiwango cha lami katika eneo la Mbwemkulu barabara kuu ya Lindi-Dar es salaam limewekewa alama zote muhimu ili kuruhusu wakati wa ujenzi wa daraja kusiwe na changamoto kwa wasafiri na wasafirishaji.
By Mpekuzi
Post a Comment