MAMLAKA ya Elimu Tanzania(TEA) kwa kushirikiana na Kituo cha utangazaji EATV leo tarehe 25 Agosti 2024 wameongoza matembezi ya hisani kwa ajili kuhamasisha umma kushiriki katika kampeni ya Namthamini inayolenga kuweka mazingira rafiki kwa wanafunzi wa kike mashuleni.
Matembezi hayo yameanzia Makao Makuu ya EATV Dar es Salaam na kupita maeneo ya Bamaga, Sayansi, Makumbusho na Morocco kisha kurejea tena Makao Makuu ya EATV.
Akizungumza katika kampeni hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa TEA, Bi. Mwanahamisi Chambega amesema TEA inashiriki kampeni hiyo muhimu kwa vile lengo la kampeni linaendana na majukumu ya Mfuko wa Elimu wa Taifa ambao TEA inausimamia.
“ Jukumu la Mfuko wa Elimu wa Taifa ni kukusanya raslimali kutoka sehemu mbali mbali kisha kuzitumia raslimali hizo kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia, ndio maana TEA leo tunashiriki katika kampeni hii inayolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia ya wanafunzi wa kike “ amesema Bi. Chambega.
Kaimu Mkurugenzi huyo wa Huduma za Taasisi wa TEA ametumia fursa hiyo kuhamasisha wadau kuchangia kampeni ya Namthamini akiongeza kuwa watapata faida mbali mbali ikiwa ni pamoja na kupata Hati ya Utambuzi wa Uchangiaji wa Elimu (Certificate of Educational Appreciation- CEA) kwa mujibu wa Kifungu cha 12 cha Sheria ya Mfuko wa Elimu ya mwaka 2001.
Mdau anaweza kutumia hati ya CEA kuombea nafuu ya kodi kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa mujibu wa Kifungu cha 16 (1) cha Sheria ya Kodi ya Mapato Sura 332 marejeo ya mwaka 2019.
Faida nyingine ni mdau kutangazwa na kutambuliwa kitaifa, ambapo mchangiaji huandikwa katika rejesta ya kudumu ya wachangiaji wa elimu
Awali Balozi wa Kampeni ya Bi. Namthamini Najma Paul alisema kampeni hiyo ambayo imeendeshwa kwa miaka saba na kituo cha utangazaji cha EATV imeweza kufikia Mikoa 20 nchini ambapo wanafunzi elfu 20 wamepatiwa huduma ya Taulo za Kike kwa kipindi cha mwaka mzima.
Katika matembezi hayo wadau muhimu wa TEA wameshiriki ambapo mwakilishi wa Total Energy Bi. Faith Mfugale ameahidi kuwa shirika lake litachangia taulo za kike katika baadhi ya shule wakati mwakilishi wa Shirika la Sayari Safi Bi. Veronica Ussiri ameahidi kuwa shirika lake litaweka miundombinu ya kusafishia maji katika baadhi ya shule zitakazonufaika na kampeni ya Namthamini.
By Mpekuzi
Post a Comment