BENKI ya Equity Tanzania imesaini mkataba na Taasisi ya ADC Tanzania, washauri wabobezi wa biashara, kuashiria kuanza kwa utekelezaji wa mradi maalum wa kuwawezesha wanawake kiuchumi.
Meneja Mkuu wa Biashara wa benki hiyo, Leah Ayoub amesema mradi huo unafanyika kwa ushirikiano na Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa ya African Guarantee Fund(AFAWA).
Amesema lengo kuu la mradi huo ni kuwajengea wanawake uwezo katika biashara zao waweze kufikia vigezo vya kupata huduma mbalimbali za kifedha, ikiwemo mikopo inayotolewa na benki hiyo kuboresha maisha yao kijamii na kiuchumi.
Leah amesema hatua hiyo ni sehemu ya mpango mkakati wa beki hiyo kuongeza wigo wa huduma kwa wateja wadogo na wa kati (MSMEs), kwa lengo la kufikia asilimia 65 ya mikopo yote ifikapo mwaka 2030.
“Tunakuwa na dhamira ya kuwawezesha wanawake katika biashara, ushirikiano huu ni hatua muhimu ya kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wanawake wajasiriamali na kuwawezesha kufikia ukuaji wa kiuchumi endelevu,” amesema Leah.
Mradi huu unalenga kuwawezesha zaidi wanawake nchini kwa kuwapatia mafunzo ya elimu ya fedha, mikopo nafuu, na ushauri maalum wa biashara.
Kwa hatua hiyo, Benki ya Equity Tanzania inaendelea kujitolea kuimarisha uimara wa kiuchumi na ujumuishi wa kijamii nchini.
Naye Ofisa Biashara wa ADC, Laura Vedasto amesema wanatarajia kuja na programu isemayo ‘Jifunze utoke’ itakayowasaidia wanawake kujua mbinu zitakazowawezesha kupata biashara na kukua.
By Mpekuzi
Post a Comment