Baraza la Umoja wa Vijana CCM
Mkoa wa Shinyanga limemteua Arnold Bweichum kuwa Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi wa Mkoa wa Shinyanga. Uteuzi huu umetangazwa rasmi chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa Baraza hilo, Bernard Benson Werema, ambaye amempongeza Bweichum kwa kuteuliwa katika nafasi hiyo muhimu.
Akizungumza baada ya uteuzi, Bweichum amewashukuru viongozi wa Baraza la Umoja wa Vijana CCM Mkoa wa Shinyanga kwa kumjumuisha katika nafasi hiyo ya heshima, huku akieleza kuwa anafahamu majukumu
makubwa yanayomkabili. Amesisitiza kwamba anajua matarajio ya vijana wa Shinyanga na atajitahidi kufanya kazi kwa bidii ili kuleta mabadiliko chanya.
“Nawashukuru kwa dhati kwa imani mliyonionyesha. Nafahamu ukubwa wa jukumu hili na matarajio ya vijana wa Shinyanga. Najiandaa kufanya kazi kwa moyo wa kujituma, uaminifu na dhamira ya dhati ili kuleta maendeleo kwa vijana wa mkoa wetu,” amesema Bweichum.
Aidha, Bweichum amewahakikishia vijana wa Shinyanga kuwa atahakikisha kuwa umoja na mshikamano kati yao unakuwa imara, huku akisisitiza umuhimu wa vijana kushirikiana kwa pamoja katika kuleta mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
“Tutafanya kazi kwa bidii ili kuleta mafanikio makubwa kwa vijana wa Shinyanga. Maneno kidogo, kazi zitaongea. Tukutane site!” ameongeza.
Viongozi na wanachama wa Umoja wa Vijana CCM Mkoa wa Shinyanga wamepongeza uteuzi wa Bweichum, wakisema kuwa wanatarajia kuwa chini ya uongozi wake, vijana wa Shinyanga wataweza kupata fursa nyingi za maendeleo na kujitengenezea maisha bora.
Kwa upande mwingine, Bweichum ameahidi kutoa kipaumbele katika masuala ya uhamasishaji, maendeleo ya vijana na kutafuta njia bora za kuwainua vijana kiuchumi na kijamii.
Uteuzi wa Anord Bweichum kama Katibu wa Uhamasishaji na Chipukizi Mkoa wa Shinyanga ni ishara ya mabadiliko na matumaini mapya kwa vijana wa mkoa huo, huku viongozi wakiwa na matumaini makubwa ya mafanikio ya utawala wake.
By Mpekuzi
Post a Comment