MAFANIKIO YA BoT KATIKA KUONGEZA AKIBA YA DHAHABU: HATUA MUHIMU KUIMARISHA UCHUMI |Shamteeblog.

Meneja Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha BoT, Dkt. Anna Lyimo akitoa mada kuhusu umuhimu wa Benki kuu kuwa na dhahabu kama sehemu ya akiba yake ya fedha za kigeni wakati wa semina kwa waandishi wa habari Kanda ya Ziwa

Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imepiga hatua kubwa katika kuongeza akiba yake ya fedha za kigeni kwa kutumia dhahabu kama rasilimali muhimu.

Hayo yamesemwa leo Jumatano Novemba 14, 2024 na Meneja Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha BoT, Dkt. Anna Lyimo, wakati akitoa mada kuhusu umuhimu wa Benki Kuu kuwa na dhahabu kama sehemu ya akiba yake ya fedha za kigeni wakati wa semina kwa waandishi wa habari Kanda ya Ziwa.

Dkt. Lyimo ameeleza kuwa akiba yake ya fedha za kigeni kwa kutumia dhahabu ni sehemu ya mpango wa kimkakati wa kuimarisha uchumi wa taifa, kupunguza utegemezi wa mikopo ya nje, na kuhakikisha usalama wa kifedha wa taifa.

Amebainisha kuwa katika kipindi cha Julai 2023 hadi Juni 2024, BoT ilinunua dhahabu yenye kilo 366.55 yenye thamani ya takribani $23 milioni na sasa kiasi hicho kiliongezeka thamani kwa $7 milioni na kufikia $30.32 milioni. 

Aidha, kufuatia marekebisho ya sheria yaliyofanywa mwezi Julai na utekelezaji wake kuanza Oktoba mwaka huu, katika kipindi cha mwezi Oktoba 2024 peke yake, BoT iliweza kununua 872.05 kg na kuchangia hifadhi ya fedha za kigeni kwa $74.04 milioni.

"Huu ni ushahidi wa mafanikio ya mpango wa kuimarisha akiba ya fedha za kigeni kwa kutumia dhahabu, ambao unalenga kuboresha hali ya kifedha ya taifa na kuunda mazingira mazuri ya kiuchumi," amesema Dkt. Lyimo.
Meneja Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha BoT, Dkt. Anna Lyimo.

Amesema mafanikio haya yanadhihirisha uwezo wa Tanzania katika kutumia rasilimali zake za asili kwa manufaa ya uchumi wake. Dhahabu ni mali ya thamani ambayo inatoa fursa ya kujenga akiba ya fedha za kigeni, na kuongeza usalama wa kifedha kunapotokea mitikisiko ya kiuchumi duniani.

Benki Kuu pia imefanikiwa kusaini mikataba miwili ya manunuzi ya dhahabu kutoka kwa wachimbaji na wauzaji wa dhahabu nchini Tanzania.

"Mikataba hii ni sehemu ya juhudi za BoT kuhakikisha kuwa nchi inapata dhahabu ya kutosha kwa ajili ya kujenga akiba ya fedha za kigeni, huku ikilenga kuongeza ushirikiano na makampuni ya uchimbaji na viwanda vya kuchenjulia dhahabu," ameeleza Dkt. Lyimo.

Ameongeza kuwa, kwa sasa, BoT inaendelea na mazungumzo na wachimbaji na wauzaji wa dhahabu ili kuhakikisha kuwa utaratibu wa ununuzi wa dhahabu unaendelea kuwa endelevu, na kwamba bidhaa zinazozalishwa nchini zinapatikana kwa urahisi ili kujenga akiba ya dhahabu ya kutosha.

"Mafanikio haya yana mchango mkubwa katika uchumi wa taifa, na kuleta matarajio chanya kwa Tanzania kwa sababu kadhaa ikiwemo kuimarisha Akiba ya fedha za kigeni, kupunguza utegemezi wa mikopo ya nje, kuvutia uwekezaji wa nje na kuonyesha ustahimilivu wa Sarafu ya Tanzania," amesisitiza.

Ameeleza kuwa Dhahabu ina uwezo wa kusaidia kulinda thamani ya sarafu ya Tanzania (Tsh) dhidi ya mabadiliko makubwa ya kiuchumi na mfumuko wa bei, na hivyo kuimarisha ustahimilivu wa sarafu ya nchi.
 Dkt. Anna Lyimo 

Benki Kuu inaendelea na jitihada za kuimarisha usimamizi wa rasilimali za dhahabu ili kuhakikisha kuwa nchi inapata manufaa makubwa kutokana na rasilimali hii ya kipekee. Huu ni mwanzo wa hatua kubwa za kiuchumi kwa Tanzania, ambazo zitasaidia kuboresha hali ya maisha ya wananchi na kuongeza maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Kwa mafanikio haya, Benki Kuu ya Tanzania inaonesha kwamba uwekezaji katika dhahabu ni suluhisho la kudumu katika kujenga akiba ya fedha za kigeni na kuimarisha uchumi wa taifa.

Hatua hii ni sehemu ya mpango wa kimkakati wa kuwa na uchumi thabiti na unaoegemea zaidi kwenye rasilimali za ndani, na inatoa mwanga wa matumaini kwa uchumi wa Tanzania katika siku zijazo.
Meneja Msaidizi kutoka Kurugenzi ya Masoko ya Fedha BoT, Dkt. Anna Lyimo akitoa mada kuhusu umuhimu wa Benki kuu kuwa na dhahabu kama sehemu ya akiba yake ya fedha za kigeni wakati wa semina kwa waandishi wa habari Kanda ya Ziwa


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post