Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesisitiza kwamba hali ya usalama na haki za binadamu katika sekta ya madini hususani katika mgodi wa North Mara hapa nchini ni shwari na hiyo iimethibitiswa na ripoti iliyotolewa na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (THBUB) hivi karibuni kuhusu hali ya usalama na haki za binadamu kwenye mgodi huo unaomilikwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga.
Akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya DW ,Waziri Mavunde, alisema Tanzania ina vyombo vyake vya ufuatiliaji wa utekelezaji wa haki za binadamu hapa nchini na Tume ipo kisheria pamoja kwamba katiba na sheria zetu zinaruhusu kwa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) ndani na nje ya nchini kufanya utafiti na kutoa ripoti zao kwa uwazi.
Alipoulizwa kuhusu taarifa iliyotolewa hivi karibuni na shirika lisilo la kiserikali la nchini Canada (Canada Mining Watch) kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki za Binadamu wakati wa upanuzi wa shughuli za mgodi katika vijiji vya Komolela na Kewacha katika wilaya ya Tarime kata ya Nyamongo ,alisema Serikali tayari ilishayafanyia kazi kupitia vyombo vyake na kubaini ukweli juu ya suala hilo kama ambavyo Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (CHRAGG) ilifanya uchunguzi wa kina dhidi ya tuhuma hizo na kutoa ripoti yake.
"Bahati nzuri Tanzania hatuishi kisiwani na sisi tuna vyombo vya kuangalia , kufuatilia na kuzingatia haki za binadamu na vyombo vyetu vimekuwa mstari wa mbele kwa jambo lolote kama linakwenda kinyume hatua zitachukuliwa kikamilifu", alisema Waziri Mavunde.
Aliendelea kusisitiza “Hoja kubwa za wananchi wanazouliza wanaozunguka maeneo ya migodi ni jinsi ya kupata maeneo ya kuchimba, kushiriki kwenye uchumi , huduma za kijamii na uwajibikaji wa wamiliki wa migodi kwa wananchi wa maeneo husika.
“ Hizo ndio hoja kubwa ambazo mimi mwenyewe nimezisikia masikio mwangu nilipoenda na kuzungumza na wananchi wa maeneo husika haya unayoniuliza sio hoja za wananchi,” alisema Mavunde.
Mnayoniuliza sio malalamiko ya wananchi mie mwenyewe nimekwenda na kufanya mikutano na wananchi wa maeneo hayo ni kilio chao zaidi ni ajira , kupata maeneo ya kuchimba na uwajibikaji wa wamiliki wa migodi kwa wananchi wanaozunguka migodi husika hicho ndio takwa la wanakijiji,” alisisitiza Waziri Mavunde.
Alisema katika juhudi za kuendelea kuvutia uwekezaji hapa nchini na kutoa ufafanuzi wa taasisi za nje ambazo zimekuwa zikitoa taarifa potovu za kufifisha uwekezaji nchini,Serikali itaendelea kushiriki katika mikutano ya kimataifa na kikanda na kuhakikisha kwamba taarifa zote zinatokana katika vyombo rasmi vya Serikali na Jeshi la Polisi litaendelea kutoa taarifa sahihi mara kwa mara ili kuondoa huu upotoshaji unaondelea ili kuendelea kuvutia wawekezaji kwenye sekta ya madini hapa nchini.
Awali akizungumza hali katika sekta ya madini alisema sekta hiyo inaendelea kukua siku hadi siku kwa kuongeza ajira, tozo , kodi ya serikali na pato la taifa na katika pato la taifa sekta hiyo inachangia asilimia 9.0 na 2021 na 2022 ilichangia asilimia 7.2 la pato la taifa.
“Sekta hii ya madini itaendelea kutegemewa hapa nchini katika kupunguza tatizo la ajira na kuchangia pato la taifa kwa maendeleo ya nchini yetu,” alisisitiza.
Aliongeza kwamba mabadiliko ya sheria ya madini ya mwaka 2017 , kwenye maudhui ya ndani (Local content) uwajibikaji kwa jamii (Corporate Social Responsibility- CSR) imechangia kwa kiasi kikubwa kuleta maendeleo ya wananchi kupitia sekta husika.
“Hapo awali wenye leseni ya uchimbaji wa madini wao ndio walikuwa wanaamua kwamba mradi huu tusaidie kuchimba na kujenga matundu ya vyoo au zahanati ila baada ya mabadiliko ya sheria , mradi unaanza kuibuliwa kutoka kwa wananchi wenyewe ngazi ya kitongoji , kata mpaka juu ndio wananchi wanaamua nini wafanyiwe na wenye leseni ya uchimbaji wa madini,” alisisitiza .
Hivi karibuni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania (THBUB) kupitia Mwenyekiti wake (Jaji Mstaafu) Mathew Mwaimu ilitoa taarifa baada ya uchunguzi wa tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu katika mgodi wa North Mara zilizotolewa na taasisi ya Canada Mining Watch na kubainisha kuwa taratibu za kisheria na taratibu za nchi zilifuatwa na ulifanyika kwa uwazi na ushirikishwaji wakati wa mgodi huo kupanua shughuli zake za uchimbaji katika vijiji tajwa vya Komarera na Kewanja
Mgodi wa North Mara unamikiwa na kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga.
By Mpekuzi
Post a Comment