VETA KIHONDA YASISITIZA MAFUNZO YA UJASIRIAMALI KWA WAHITIMU ILI KUJIAJIRI |Shamteeblog.


-Mkurugenzi VETA Kanda ya Mashariki ahimiza ujasiriamali kwa vitendo

Mkurugenzi wa Kanda ya Mashariki, John Mwanja ameelekeza vyuo vya VETA Kanda ya Mashariki kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa vitendo kuwasaidia vijana kujiajiri baada ya kuhitimu mafunzo yao.

John Mwanja, ameyasema hayo alipokuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 36 ya wanafunzi wa ngazi ya II katika chuo cha VETA Kihonda, yaliyofanyika katika viwanja vya chuo hicho, tarehe 21 Novemba 2024.

Amewataka walimu na menejimenti za vyuo vya kuwasaidia na kuwasimamia wanafunzi kuanzisha vikundi, kupanga na kutekeleza mawazo ya kuanzisha makampuni madogo madogo wakiwa darasani, ili kuwazoesha kuungana na kufanya kazi kwa pamoja, kujiajiri na kutafuta soko la bidhaa zao.

“Hivyo, ni jukumu la menejimenti kuwasaidia wanafunzi waliojiunga kwenye vikundi vidogo vidogo kwa fani mbalimbali, kurasimisha vikundi hivyo ili bidhaa zitakazozalishwa ziweze kuingia sokoni,” Mwanja amesema

Mkurugenzi huyo, amesisitiza menejimenti kutoa mafunzo ya ujuzi yenye tija yanayolenga kuzalisha bidhaa zenye ubora kukidhi ushindani na kutafuta soko ili kupata marejesho ya bidhaa hizo kupitia fedha za mauzo.

Aidha, Mwanja ametaka bidhaa zinazotengenezwa na wanafunzi wakati wa mazoezi ya vitendo zitafutiwe soko na kama inashindikana kupata soko zitolewe kwa watu wenye mahitaji maalum badala ya kurundikana katika karakana.

Mkuu wa Chuo cha VETA Kihonda, Dkt. Salumu Ulimwengu, amewapongeza wahitimu na kuwataka Kwenda kutumia ujuzi katika kuwaendeshea maisha yao na kuwa mfano wa kuigwa na jamii itakayowazunguka.

“Nendeni mkawe mabalozi wazuri, mkatumie elimu ya ufundi stadi mliyoipata kuwaletea kipato,” Dkt.Ulimwengu amesema

Mahafali hayo yalijumuisha wahitimu 230 wa ngazi ya II wakiwemo wasichana 62 na wakiume 168 katika fani za Zana za Kilimo (wahitimu 25), Umeme wa magari (23), umeme majumbani (42), Bomba (37), Useremala (11), Uashi (21), Majokofu na Viyoyozi (32), Ushonaji (16), Ufundi magari (21), na Mitambo na Ukerezaji (16). Pia wanafunzi 132 wa udereva na kozi za muda mfupi wamehitimu


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post