📌Kunufaisha Kaya 2,970 kutoka katika Vitongoji 90 ndani ya Wilaya Tatu
📌RC Macha asema Umeme ni kipaumbele cha Rais Samia
Na Mwandishi wetu - Shinyanga
Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) inatekeleza mradi wa Shilingi Bilioni 11.18 wa kusambaza umeme katika vitongoji 90 utakaonufaisha Kaya 2,970 Mkoani Shinyanga.
Msimamizi wa Miradi ya REA Kanda ya Magharibi, Mhandisi Robert Dulle amebainisha hayo Novemba 05, 2024 Mkoani Shinyanga mbele ya Mkuu wa Mkoa huo, Mhe. Anamringi Macha wakati wa kumtambulisha Mkandarasi aliyeshinda Zabuni ya kutekeleza mradi huo Kampuni ya wazawa ya Derm Group (T) Limited ya Jijini Dar es Salaam.
“Tunamshukuru Rais wetu Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia kiasi cha shilingi 11,184,759,397.2 kitumike kusambaza umeme katika vitongoji 90 Mkoani hapa, leo hii tumefika hapa kumtambulisha Mkandarasi na tayari maandalizi ya awali ya kutekeleza mradi yameanza,” amesema Mhandisi Dulle.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi wa kufikisha umeme katika vitongoji Mkoani Shinyanga, Mhandisi Dulle amesema kati ya vitongoji 2,703 vilivyopo mkoani humo, vitongoji 930 vimefikishiwa umeme na kwamba vitongoji 90 vitakavyopata umeme awamu hii vitaongeza idadi ya vitongoji vitakavyokuwa na umeme Mkoani Shinyanga.
Amesema mradi unatekelezwa kwa kipindi cha miezi 24 ambapo utekelezwaji wa mradi ulianza tarehe 3 Septemba, 2024 na utakamilika ifikapo tarehe 19 Agosti 2026 na kwamba vitongoji vitakavyobaki vitaendelea kusambaziwa umeme kulingana na upatikanaji wa fedha.
Mhandisi Dulle amebainisha kuwa mradi unatekelezwa katika majimbo sita kutoka katika Wilaya za Shinyanga, Kahama na Kishapu na kwamba kila jimbo vitongoji 15 vitanufaika.
“Mradi huu unalenga kupeleka umeme katika majimbo ya Shinyanga, Solwa, Kishapu, Msalala, Ushetu na Kahama,” amesema Mhandisi Dulle.
Aidha, Mhadisi Dulle ameainisha hali ya upatikanaji wa umeme maeneo ya vijijini Mkoani Shinyanga sambamba na miradi iliyokamilika na inayoendelea kutekelezwa ambapo amesema kati ya vijiji 506 vilivyopo mkoani humo, vijiji 485 vimefikishiwa umeme ambayo ni sawa na asilimia 96 na kwamba vijiji 21 vilivyobaki vipo katika hatua mbalimbali za utekelezaji wa mradi wa REA awamu ya tatu mzunguko wa pili (REA3R2) chini ya Mkandarasi Tontan Project Technology LTD JV Group Six International.
Amesema vijiji hivyo vipo katika Wilaya ya Kahama na kwamba Mkandarasi anatarajiwa kukamilisha hivi karibuni.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha ameipongeza REA kwa kutekeleza majukumu yake kwa uwazi na kwa utaratibu iliyojiwekea wa kutambulisha wakandarasi kwa viongozi wa Mkoa na Wilaya kote nchini.
“Ujio wenu hapa ni habari njema sana kwa mustakabali mzima wa maendeleo ya Mkoa wetu; pamoja na huduma zingine za jamii huduma ya umeme imepewa kipaumbele kikubwa na Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan, umeme ni injini ya uchumi hili halina ubishi na sasa matumizi ya umeme yameongezeka, mahitaji kwa ajii ya majumbani na pia kiuchumi,” amesema Mhe. Macha.
Amesema Mkoa wa Shinyanga unaendelea kukua kwa kasi na kwamba kwa sasa shughuli za kiuchumi zimeongezeka ikiwemo uwepo wa viwanda vidogo na vikubwa ambavyo vyote vinahitaji umeme.
“Hapa Shinyanga mbali na Madini pia tunashughulika na kilimo cha mpunga na tungependa kuona mkulima akiongeza thamani ya mazao yake hukohuko unapozalishwa mpunga kwa kukoboa na kupata mchele na hapa faida itaongezeka sambamba na kuandaa ajira na fursa zingine vijijini,” amesema Mhe. Macha.
Aidha, amemtaka Mkandarasi kuhakikisha anatekeleza mradi kwa ubora na anakamilisha kwa wakati kwani tayari miundombinu ipo hivyo hakuna changamoto yoyote itakayokwamisha utekelezaji wa mradi.
“Tunafuraha kuona zipo kampuni za Kitanzania zenye uwezo wa kutekeleza miradi mbalimbali ikiwemo hii ya umeme ikiwemo kampuni hii ya Derm, tunatoa wito pia kutumia huduma na watoa huduma kwenye maeneo ya mradi, tutoe kipaumbele kwenye kazi zisizohitaji ujuzi mkubwa kwa wananchi wa maeneo ya mradi,” amesema.
Meneja wa Mradi kutoka Kampuni ya Derm Group (T) Limited Mhandisi Justinus Mutalemwa amesema wamejipanga kikamilifu kutekeleza mradi ambapo kwa sasa wamekamilisha hatua muhimu za awali za mradi, ikiwemo ukaguzi wa eneo na kukagua nguzo kiwandani, na tayari nguzo zimeanza kufika kwenye maeneo ya mradi.
“Tunatarajia kumaliza mradi huu ndani ya muda uliopangwa wa miezi 24. Kazi hii haitakuwa kubwa sana kwa sababu ya umbali wa kilomita 164 tu, tutamaliza kabla ya wakati uliopangwa, kikubwa tunaomba ushirikiano kutoka kwa TANESCO, REA na Serikali ili kuhakikisha utekelezaji wa mradi unafanikiwa kama ilivyopangwa”,amesema Mhandisi Mutalemwa.Mhandisi Anthony Tarimo
Naye Mhandisi Mwandamizi kutoka TANESCO Mkoa wa Shinyanga Anthony Tarimo akizungumza kwa niaba ya Meneja wa TANESCO Mkoa wa Shinyanga amesema vitongoji 90 vilivyopendekezwa ni vya umuhimu mkubwa, kwa kuwa vilikuwa na uhitaji mkubwa wa huduma ya umeme, na utekelezaji wa mradi huu utaondoa malalamiko ya wananchi kuhusu ukosefu wa huduma hiyo.
By Mpekuzi
Post a Comment