📌 Watanzania milioni 13.5 kusambaziwa umeme ifikapo 2030 kutoka milioni 5.2 ya sasa
📌 Asema Mkutano wa Mission 300 umekuwa kivutio duniani; Taasisi za Kimataifa zaonesha nia ya kushiriki
📌 Ataja sababu za mkutano wa M300 kufanyika Tanzania
Na Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe.Dkt.Doto Biteko amesema kuwa maandalizi ya Mkutano wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika wenye lengo la kuharakisha upatikanaji umeme kwa Waafrika milioni 300 ifikapo 2030 (Mission 300) utakaofanyika tarehe 27 na 28 Januari jijini Dar es Salaam yamefikia asilimia 95.
Dkt.Biteko amesema hayo tarehe 15 Januari 2025 mara baada ya kukagua maandalizi ya Mkutano huo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Julius Nyerere (JNICC) Jijini Dar es Salaam akiwa ameambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Amesema Wakuu wa Nchi 54 kutoka Bara la Afrika wanatarajiwa kushiriki pamoja na viongozi wengine ambao ni Mawaziri wa Fedha na Nishati kutoka barani Afrika, Marais wa Benki ya Dunia (WB) na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB), pamoja viongozi kutoka Jumuiya ya Ulaya na Jumuiya ya Umoja wa Afrika ambapo kazi zinazoendelea kwa sasa ni pamoja na kukamilisha ukarabati wa ukumbi wa JNICC.
“Kazi nyingine zinazoendelea ni pamoja na usajili na uthibitisho wa wageni ambao watakuja kwa ajili ya ushiriki na ukarabati wa maeneo mengine yatakayotumika kwenye mkutano huu, nichukue nafasi hii kuupongeza uongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa hatua iliyofikiwa na kuliweka jiji kwenye mandhari ya kuvutia.” Amesema Dkt.Biteko
Ameongeza kuwa, Mkutano wa M300 umekuwa kivutio ambacho kimewashawishi Wakuu wa Taasisi nyingi za Kimataifa kuonesha nia ya kushiriki mkutano huo mkubwa katika Sekta ya Nishati.
Ameeleza kuwa, Tanzania kuwa mwenyeji wa mkutano huo kumetokana na Diplomasia nzuri ya Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo imezidi kuimarisha uhusiano wa Tanzania kimataifa na kupelekea WB na AfDB kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa Mkutano.
Ametaja sababu nyingine ya Tanzania kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo muhimu ni mafanikio yaliyofikiwa katika sekta ya Nishati huku akitoa mfano wa mafanikio katika usambazaji wa nishati vijijini.
Amesema vijiji vyote nchini 12,318 vimesambaziwa umeme na Vitongoji 34,000 kati ya 64,274 vilivyopo nchini, tayari vimesambaziwa umeme.
Ametaja baadhi ya faida za mkutano huo kuwa ni pamoja na kuongezeka idadi ya Watanzania watakaounganishwa na umeme ifikapo mwaka 2030 hadi kufikia milioni 13.5 kutoka milioni 5.2 ya sasa.
Ameongeza kuwa, katika mkutano huo nchi zitasaini mikakati ya kuharakisha kusambaza umeme kwa wananchi ambayo itaeleza kwa kina hatua gani zitachukuliwa chini ya mwavuli wa WB na AfDB.
Ameongeza kuwa, faida nyingine zitakazotokana na mkutano wa M300 ni kuongezeka kwa fursa za uwekezaji, kuimarisha biashara na kuongeza heshima ya nchi katika Duru za kimataifa na Tanzania kuwa Taifa linalopigiwa mfano kwenye nyanja mbalimbali.
Dkt. Biteko ametoa wito kwa Watanzania kuupokea kwa mikono miwili mkutano huo ambao kwa kiasi kikubwa unazidi kumheshimisha Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan na Watanzania kwa ujumla.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kuendelea na hali ya amani na utulivu kuelekea katika mkutano huo wa kihistoria kutoka nchi ipige hatua kwenye Sekta ya Nishati kwani ni Mkutano Mkubwa wa kwanza kufanyika.
Vilevile ametoa wito kwa Waandishi wa Habari kuutangaza Mkutano huo kwa Watanzania ili waufahamu kwa kina na kufahamu fursa zilizopo.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila amesema maandalizi ya kupokea ugeni huo yako katika hatua za mwisho.
Amesema ili kufanikisha mkutano huo, baadhi ya mitaa itafungwa ili kuwezesha maonesho na utalii wa ndani ikiwa ni pamoja na utalii wa tiba.
By Mpekuzi
Post a Comment