WIKI YA SHERIA YAZINDULIWA WILAYANI TUNDURU..WANANCHI WAHIMIZWA KUTAFUTA MSAADA WA KISHERIA |Shamteeblog.


Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Wilaya Ya Tunduru Shughuli Mwampashe aliyevaa suti nyeusi akiongoza matembezi kwa watumishi na wadau mbalimbali wa Mahakama kabla ya uzinduzi wa wiki ya sheria Wilayani Tunduru

Watumishi na wadau mbalimbali wa Mahakama Wilayani Tunduru Mkoani Ruvuma wakielekea katika viwanja vya Baraza la Idd Wilayani humo kabla ya uzinduzi wa wiki ya sheria


Na Regina Ndumbaro Tunduru.

Watumishi wa Mahakama na wadau mbalimbali wilayani Tunduru, mkoani Ruvuma, wamefungua wiki ya Sheria kwa kufanya matembezi ya kilometa moja yaliyoongozwa na Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Wilaya, Shughuli Mwampashe. 

Matembezi hayo yalipokelewa rasmi na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tunduru, Milongo Sanga, katika viwanja vya Baraza la Idd mjini Tunduru.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Sanga amewahimiza wananchi kutumia wiki ya Sheria kutafuta msaada wa kisheria kupitia vituo saba vilivyotengwa maalum kwa huduma hiyo.

 Ameeleza kuwa wataalamu wa sheria, wakiwemo mahakimu, watakuwepo kwenye vituo hivyo kusaidia utatuzi wa changamoto mbalimbali zinazowakumba wananchi.


Vituo hivyo, vilivyotajwa na Sanga, ni Shule ya Sekondari Frank Weston, Mataka, Mgomba, Shule ya Msingi Mchangani, Shule ya Msingi Umoja, na Chuo cha Ufundi Mbesa. Pia, amebainisha kuwa huduma za kisheria zitatolewa kwa viongozi wa dini kupitia nyumba za ibada, ili kuwasaidia kuelewa taratibu za kisheria na kuzifikisha kwa waumini wao.


Sanga amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi zake za kuboresha huduma za Mahakama nchini, ikiwemo kuanzisha mfumo wa Mahakama Mtandao. Amesema mfumo huo umesaidia sana wananchi kupata elimu na taarifa za kisheria kwa urahisi. Pia, amewataka watumishi wa Mahakama kuhakikisha wanatenda haki kwa usawa bila kujali nafasi au cheo cha mtu.



Kwa upande wake, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi, Shughuli Mwampashe, amesema lengo la wiki ya Sheria ni kuwapa wananchi uelewa kuhusu mambo yanayofanywa na Mahakama na wadau wake. 



Amesisitiza umuhimu wa wananchi kutembelea vituo vya huduma za kisheria ili kupata elimu na msaada wa kisheria, hasa kutokana na kuongezeka kwa mashauri ya ubakaji na uhujumu uchumi katika wilaya hiyo.


Naye Mdau wa Sheria kutoka kituo cha msaada wa kisheria cha TUPASE, John Nginga, ameeleza kuwa changamoto kubwa inayoikumba jamii ni ukosefu wa uelewa kuhusu haki zao za msingi na taratibu sahihi za kuzidai. 


Ameonya kuwa watu wengi hujikuta wakivunja sheria bila kujua wakati wa kudai haki zao.


Amesisitiza kuwa msingi wa maendeleo na ustawi wa jamii ni amani, na amani haiwezi kupatikana bila haki.

 Amewaomba watumishi wa Mahakama kuendelea kutenda haki kwa uadilifu ili kuhakikisha wananchi wanajenga imani kwa mhimili huo muhimu wa nchi.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post