Na Kadama Malunde - Malunde 1 blog
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga, Mhandisi James Jumbe Wiswa, amechangia mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika Kituo cha Afya Kambarage Manispaa ya Shinyanga.
Mchango huu unalenga kuimarisha usalama wa wagonjwa na watoto wachanga waliozaliwa katika kituo hicho.
Mhandisi Jumbe amekabidhi mifuko hiyo ya saruji leo, Jumamosi, Februari 22, 2025, wakati wa ziara ya Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, ambapo wamekagua maendeleo katika Kituo cha Afya Kambarage na ujenzi wa barabara ya Kenyatta-Karena.
Ziara hiyo pia imejumuisha mazungumzo na wanachama wa CCM kutoka Kata ya Kambarage, Lubaga na Mjini.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya mifuko ya saruji, Mhandisi Jumbe amesema, "Nimeamua kutimiza ahadi yangu kutoa mifuko hii ya saruji ili kuimarisha ulinzi katika Kituo cha Afya Kambarage. Kamati ya Kituo hiki iliniletea ombi la ujenzi wa uzio na mimi nimelijibu kwa vitendo. Kituo hiki kipo kwa ajili ya akina mama na watoto, na tunahitaji kuwalinda kwa kila hali."
Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga, Mhandisi James Jumbe Wiswa (kushoto), na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko wakikabidhi mifuko ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio katika kituo cha afya Kambarage
“Niipongeze kamati ya Kituo cha Afya Kambarage kwa juhudi zao za kutoa michango mbalimbali. Mwenyekiti wa Kamati aliniandikia barua tangu mwaka jana akaniambia kuhusu ujenzi wa uzio wa kituo hiki, na mimi nikaahidi kumsaidia kama alivyoeleza. Ingawa zoezi hili lilikuwa likichelewa mara kwa mara, katika hatua ya mwisho nilimwambia kuwa, kama mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Wazazi, na kwa kutambua kuwa Kituo hiki cha Afya kinahudumia kwa kiasi kikubwa akina mama na wazazi, ni muhimu tuungane ili kuhakikisha linakuwa salama,” amesema Mhandisi Jumbe.
Mhandisi James Jumbe Wiswa
“Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejitahidi sana kuboresha sekta ya afya. Ameleta vifaa tiba vya kisasa, ameunda majengo ya kisasa, na ametunza vifaa vya gharama kubwa ambavyo vilikuwa vigumu kupata kwenye sekta binafsi. Mama Samia ni mama mwenye watoto, anajua changamoto zinazowakumba akina mama. Sisi kama wadau wa maendeleo, na mimi pia ni mfanyabiashara, tunapaswa kujitolea kwa ajili ya jamii yetu,” ameongeza Mhandisi Jumbe.
Amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameonesha jitihada kubwa kuboresha sekta ya afya nchini, na yeye kama mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji Jumuiya ya Wazazi, ameamua kuunga mkono juhudi hizo kwa kuchangia katika ujenzi wa uzio akisema "Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan amejitahidi kuboresha sekta ya afya, ametoa vifaa vya kisasa na kujenga majengo bora.
“Kwa hiyo, nimeona ni vyema kumuunga mkono Rais Samia kwa juhudi zake kubwa. Kama wadau, ametufanyia mazingira rafiki ya kufanya shughuli zetu na tumeweza kulipa kodi bila shida. Hivyo, tunahitaji kutoa kile tunachopata kusaidia jamii yetu. Na nawaasa wafanyabiashara wa Shinyanga, tunao wengi, wajitolee kusaidia. Mchango huu ni kidogo, lakini kama wote tungeungana, uzio huu utakuwa ni ishara ya kulinda uhai wa mwanadamu aliyetunukiwa na Mwenyezi Mungu. Hatupaswi kuweka mazingira hatarishi kwa akina mama wanaokuja kupata huduma, lazima tuwajibike na kuwalinda,” amesema Mhandisi Jumbe.
“Leo, tumekabidhi mifuko 100 ya saruji kwa ajili ya ujenzi wa uzio, lakini pia Jumuiya ya Wazazi CCM Shinyanga Mjini tumechangia matofali 2000 kwa mradi huu, na tutachangia mchanga wa kutosha. Tutaendelea kutekeleza matendo ya msaada, kumuunga mkono Rais Samia, na Mungu akipenda, tutawatia moyo watumishi wa afya. Mchango huu ni zawadi kutoka kwa watu wa Shinyanga, na pia ni ishara ya kuunga mkono azimio la Mkutano Mkuu CCM kumteua Rais Samia kugombea tena urais. Tunamuonesha Rais wetu upendo na msaada kwa vitendo. Mchango huu ni zawadi kwa Rais Samia na pia ni ishara ya kumpongeza kwa juhudi zake” ,ameeleza Mhandisi Jumbe.
Katika ziara hiyo, akiwa katika kata za Kambarage, Mjini na Lubaga Mhandisi Jumbe amewahamasisha wanachama wa CCM kutangaza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
"Kazi yetu kama makada wa CCM ni kuyasemea mambo mazuri yaliyofanywa na Rais Samia. Tunataka Rais Samia apate ushindi mkubwa katika uchaguzi Mkuu mwaka huu, ni mama mwenye huruma na ameimarisha amani, umoja, na mshikamano",amesema Jumbe.
Viongozi wa Kituo cha Afya Kambarage, Mwenyekiti wa Bodi Adolf Nzwanzungwanko na Mganga Mfawidhi Dkt. Ernest Magula, walimshukuru Mhandisi Jumbe kwa mchango wake na kusema kuwa uzio huo utasaidia kuimarisha usalama hasa wakati wa usiku, hivyo kurahisisha huduma za afya kwa wananchi.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Fue Mrindoko, amesisitiza kuwa chama kinapaswa kuungwa mkono kwa sababu kimeendelea kuwaletea maendeleo wananchi wa Shinyanga.


By Mpekuzi
Post a Comment