
Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog
Wajumbe na wanachama wa Chama cha Mapinduzi jimbo la Shinyanga Mjini wametakiwa kutetea na kuyasemea mazuri yanayofanywa na viongozi wa chama chao ili waweze kuendelea kutekeleza ilani ya chama hicho.
Hayo yamebainishwa leo Februari 23, 2025 wakati wa ziara ya kata kwa kata ya Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi yenye lengo la kukijenga chama na kusikiliza kero za wananchi ndani ya jimbo hilo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Katibu wa Chama cha Mapinduzi CCM wilaya ya Shinyanga Mjini Hamisa Chacha amewahimiza wajumbe hao kuendelea kuhamasisha wananchi kujiunga na Chama Cha Mapinduzi na kuwakumbusha wajibu wao katika kuyasema mazuri yaliyofanywa na viongozi wa chama hicho na kuwatetea kwenye majukwaa dhidi ya watu wanaowakashifu.
"Tuendelee kuwahamasisha wasio wanachama kujiunga na chama chetu ili ifikapo Oktoba tuweze kujitokeza kwa wingi kushiriki katika uchaguzi wa kuwachagua viongozi wetu, lakini pia twendeni tukayaseme yale waliyofanya viongozi wetu ikiwemo wabunge, madiwani na Rais wetu kupitia majukwaa mbalimbali. Yanayosemwa juu ya viongozi wetu tuwe mstari wa mbele kuwatetea ili kuwapa moyo wa kuendelea kukitumikia", amesema Hamisa Chacha.
Diwani wa kata ya Kizumbi Mhe. Ruben Kitinya ameeleza ukuaji wa kasi wa kata hiyo kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, umeme na maji na kumshukuru Mbunge Katambi kwa kuwapigania wananchi na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa kipindi cha miaka minne huku akimuomba Mheshimiwa Mbunge kuwashika mkono katika ukamilishaji wa jengo la zahanati ya Bugayambelele ambalo ujenzi wake umeanzishwa na wananchi.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na watu wenye ulemavu ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe. Patrobas Katambi amesema kwa sasa Shinyanga imepiga hatua kubwa katika maendeleo sambamba na ukusanyaji wa mapato kupitia vyanzo vyake vya mapato na kufikia bilioni 5 hadi 6 na kuweka wazi miradi iliyotekelezwa kwa kipindi cha miaka 4 ndani ya jimbo la Shinyanga kwenye sekta zote.
"Ahadi nyingi zilizoahidiwa na ilani ya Chama Cha Mapindizi zimeendelea kutekelezwa, tumejenga shule mpya 10 za msingi na sekondari ndani ya miaka 4 lengo ni kutoa elimu ya uhakika, fursa na ajira kwa vijana, lakini pia ujenzi wa vyuo vikuu na vya kati, uhimalishaji wa huduma za afya nao pia umeendelea kuimarishwa",
"Ni lazima tuwe na miundombinu bora ili kufanya manispaa ya Shinyanga kuwa Jiji, tunazidi kuiba serikali kufanya ukarabati wa miundombinu yetu iliyoharibiwa na mvua, dhamira yetu ni kusambaza mtandao wa barabara za lami utakaounganisha kata zetu sambamba na ujenzi wa uwanja wa ndege lengo ni kuongeza mapato na shughuli za uzalishaji ndani ya manispaa ya Shinyanga ili kupiga hatua na kuwa Jiji na haya yote yanafanywa na serikali ya awamu ya sita kupitia Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan ", ameongeza Katambi.
Nao baadhi ya wananchi walimpongeza Mbunge Katambi kwa kazi kubwa ambayo ameifanya, huku akimuomba awatatulie changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara ambayo iliharibiwa na mvua,kufikisha umeme kwenye maeneo ambayo bado, pamoja na umaliziaji wa maboma ya Zahanati yaliyosalia.
Mganga Mkuu wa Manispaa ya Shinyanga Dk. Elisha Robert akijibu swali la ukamilishaji wa Zahanati kwenye Mkutano wa hadhara kata ya Kizumbi amesema kwanza anamshukuru Mheshimiwa Rais Samia pamoja na Mbunge Katambi, kwa kupunguza idadi ya maboma ya vituo na zahanati ambayo yalikuwa bado hayajakamilika kuliwa na Maboma 16,lakini 6 yamekamilishwa na yanatoa huduma, huku Zahanati mbili ya Mwagala na Mwamagunguli zipo hatua za mwisho za ukamilishaji.
Mheshimiwa Mbunge Patrobas Katambi Februari 24,2025 anaendelea na ziara yake Katika Kata ya Mwamalili na Oldshinyanga ambapo leo ameanza ziara hiyo kwenye kata ya Kizumbi na Ibinzamata,







By Mpekuzi
Post a Comment