Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed akizungumza na watumishi wa sekta mbalimbali ikiwemo Afya waliokuja kwenye kikao hicho cha mpango harakishi na shirikishi wa tathmini ya mpango wa bajeti ya lishe
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Dkt. Louis Chomboko akiwasilisha mpango harakishi na shirikishi wa kupunguza udumavu na utafiti wa hali ya udumavu na viashiria vyake
Afisa lishe Mkoa Joyce Cosmas Kamanga akitoa taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa Lishe kwa kipindi cha Julai hadi Disemba 2024
Baadhi ya Watumishi wa serikali kutoka sekta za afya na viongozi wa serikali wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma pichani hayupo kwenye kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa Lishe kwa kipindi cha Julai-Disemba 2024.
Na Regina Ndumbaro - Songea Ruvuma.
Kikao cha tathmini ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2024 kimefanyika katika Ukumbi wa Chandamali, Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma.
Kikao hicho kimeongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas, ambaye alithibitisha ajenda za kikao hicho.
Lengo kuu la mkutano huo lilikuwa ni kutathmini hali ya lishe katika mkoa huo, hususan kwa watu wanaokabiliwa na tatizo la udumavu, na kuweka mikakati ya kupunguza changamoto hiyo.
Katika kikao hicho, takwimu za hali ya lishe ziliwasilishwa kwa kila wilaya ya mkoa wa Ruvuma.
Mkoa huu una jumla ya wilaya tano, zikiwemo Manispaa ya Songea, Tunduru, Mbinga, Nyasa, na Namtumbo.
Takwimu hizo zimeonyesha kuwa Manispaa ya Songea ina mashine tatu za usindikaji wa lishe, viwanda 34, na shule mbili za sekondari—Songea Girls na Songea Boys.
Halmashauri ya Tunduru ina mashine moja, Madaba mashine moja, wakati Mbinga Mji na Nyasa hazina mashine za usindikaji wa lishe na Wilaya ya Namtumbo, ambayo awali haikuwa na mashine, sasa ina mashine tatu.
Sababu mbalimbali zinazoathiri lishe na kusababisha udumavu katika mkoa wa Ruvuma zilijadiliwa.
Ili kukabiliana na hali hiyo, kikao kilielekeza juhudi za kufanya tafiti za kina katika kila wilaya ili kubaini chanzo halisi cha tatizo.
Matokeo ya tafiti hizo yatasaidia kuweka mikakati thabiti ya kuimarisha hali ya lishe na kupunguza udumavu katika jamii.
Afisa Lishe wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Joyce Cosmas Kamanga, amewasilisha taarifa ya utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa kipindi cha Julai hadi Desemba 2024.
Taarifa hiyo ilihusisha tathmini ya hatua zilizochukuliwa katika kuimarisha lishe pamoja na changamoto zilizopo.
Amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi, na wadau wa maendeleo katika kupambana na tatizo la udumavu.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Dkt. Louis Chomboko, amewasilisha mpango harakishi na shirikishi wa kupunguza udumavu katika mkoa huo.
Pia, amewasilisha utafiti wa hali ya udumavu na viashiria vyake, akibainisha maeneo yanayohitaji uingiliaji wa haraka ili kuboresha hali ya lishe kwa watoto na makundi mengine yaliyo hatarini.
Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa, Victory Nyenza, amewasilisha taarifa ya Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM).
Programu hiyo imelenga kuhakikisha kuwa watoto wanapata lishe bora na malezi sahihi tangu utotoni ili kudhibiti tatizo la udumavu na madhara yake ya muda mrefu.
Kikao kilihitimishwa kwa majadiliano kati ya washiriki, ambapo maswali yaliulizwa na kujibiwa na wataalamu wa lishe, afya, na ustawi wa jamii.
Hatimaye, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas, alifunga rasmi kikao hicho huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kutekeleza mipango ya lishe kwa maendeleo ya jamii na afya bora ya wananchi.
By Mpekuzi
Post a Comment