![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEgzCabNekIXc_EQEzpVtnda3HtfvPCsfD-0s219XSFW0V48PCckxirqShnA1YS2gbXaOKfb92hZ2u-LegeoY80fURtSjFhhe7UHhDbPGI3zXBoM13BrVWlpKhGJFm-32spHcYU2vgxhqpCmNdEcfQK8Dvv8xrxFXtafTdH7z2f-W3a9sCVHDcrQBlJVDG4Y/w640-h424/1001991611.jpg)
![](https://blogger.googleusercontent.com/img/b/R29vZ2xl/AVvXsEihdhv9X5igPachmAE6HNS0HTKcQ9OEE4pw2S0xWwxee_yq-E7JHj4ps84q8gwHL5jM7fpvc57i-qbM4z7Y0sxJjC918eCYTuGnxBpelkoJGHfNhQbIEOJWK3wfNmulHC7md9IDXyQK_NROPgWhfb41vLrssN7DpL_Gd2A_yAXyAHYnBNDrPsb1j-ICFnI5/w640-h348/1001991616.jpg)
Baadhi ya Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga Mkoani Ruvuma wakiwa kwenye kikao
Na Regina Ndumbaro - Mbinga.
Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, mkoani Ruvuma, limewasimamisha kazi Watendaji saba wa vijiji kwa tuhuma za ubadhirifu wa Shilingi 28,236,400/=.
Fedha hizo zilipatikana kutoka vyanzo mbalimbali vya mapato vya Halmashauri kupitia mashine za POS lakini hazikupelekwa benki kama inavyotakiwa.
Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Desderius Haule, ametoa maamuzi hayo Januari 31,2025 baada ya Baraza kugeuka kuwa kamati maalum ya kujadili suala hilo.
Amesema uchunguzi uliofanywa na tume maalum ulibaini kuwa Watendaji hao walitumia fedha hizo bila kufuata taratibu za kisheria ikiwa ni pamoja na kushindwa kuomba idhini ya kubadili matumizi au kuhamisha fedha kutoka kifungu kimoja kwenda kingine.
Haule ameeleza kuwa Watendaji hao walifikishwa kwenye Kamati ya Maadili, ambapo Madiwani waliunga mkono mapendekezo ya tume ya uchunguzi na timu iliyoundwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya kuwachukulia hatuanapia kupewa agizo la kurejesha fedha walizochukua.
Kwa upande wake, Afisa Rasilimali Watu wa Halmashauri hiyo, Festo Mwangalika, amewataja Watendaji waliohusika pamoja na kiasi cha fedha walizoshindwa kupeleka benki.
Watendaji hao ni Festho Komba (Sh. 7,527,100), Mwajuma Matily (Sh. 580,000), Shaban Mkongo (Sh. 582,000), Fotnatus Ngongi (Sh. 2,626,000), Keneth Moyo (Sh. 10,448,000), Sotely Kawhili (Sh. 2,734,300) na Gaston Mbunda (Sh. 3,739,000).
Katika hatua nyingine, Baraza la Madiwani limemsimamisha Diwani wa Kata ya Mapera, Betram Komba, kutohudhuria vikao vitatu kwa tuhuma za kukiuka maadili ya kikanuni, kutoa lugha isiyo staha, na kufanya vurugu kwenye kikao cha Baraza.
Haule amewapongeza Madiwani na Watumishi wa Halmashauri kwa kazi nzuri ya kusimamia ukusanyaji wa mapato, hali iliyoiwezesha Halmashauri hiyo kuwa kinara wa makusanyo kati ya Halmashauri nane za Mkoa wa Ruvuma.
Amesisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa yeyote atakayekiuka taratibu za ukusanyaji na usimamizi wa fedha za umma.
By Mpekuzi
Post a Comment