NGEZE AMSHUKURU RAIS SAMIA KWA KUPAMBANIA AFYA YAKE |Shamteeblog.



Na Lydia Lugakila - Bukoba

Mwenyekiti wa Alat Taifa,Diwani wa kata ya Rukoma Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera Mhe, Murshid Hashimu Ngeze amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu hassan kwa namna alivyosimama katika kugharamia matibabu  yake alipopata ajali Mwaka 2022 iliyopelekea kukatwa mguu wake mmoja.

Mhe, Ngeze ametoa kauli hiyo katika dua Maalum ya Kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumnusuru katika ajali mbaya ambayo imeenda sambamba kuliombea taifa hasa katika kipindi hiki cha uchaguzi mkuu ujao iliyofanyika kata Rukoma Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Mkoani Kagera  ikiongozwa na viongozi mbali mbali wa dini na madhehebu.

"Namshukuru Rais Samia pamoja na wasaidizi wake kwa juhudi zao za kugharamia matibu yangu ndani na nje ya Nchi tangu nilipopata ajali iliyopelekea kuvunjika mguu  mmoja hadi kupelekea kukatwa" ,amesema Mwenyekiti  Alat Taifa.

Ngeze amesema Rais Samia ana upendo anajali anasikiliza na sio kwamba anaangalia miradi tu bali anaangalia Afya za Watanzania.

Ngeze amesema kupona kwake kuliimarika siku tatu alipokuja Makamu wa Rais wa Tanzania kumuona Hospitalini kwa maelekezo ya Rais Samia aliyemtaka aeleze nini anataka kufanyiwa ili Afya ikae sawa.

Aidha kiongozi huyo amewashukuru Madaktari waliohusika katika kutoa huduma ya matibabu bila kuchoka, Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya Taifa na Mkoa, taasisi za kifedha viongozi mbali mbali wa kiserikali pamoja na mtu mmoja mmoja ikiwemo familia yake  kwa namna walivyoshirikiana kutoa huduma mbali mbali katika kipindi hicho kigumu.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba Privatus Mwoleka,  akizungumza kwa niaba ya Madiwani wa Halmashauri hiyo amesema wanamshukuru Mungu kwa uhai wa kiongozi huyo lakini pia wanampongeza Rais Samia kwa matibabu aliyoyapata nje na ndani ya Nchi kwani Rais Samia amegharamikia matibabu ya Ngeze kwa  asilimia 80.

Mkuu wa Wilaya Bukoba Erasto Sima aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa Kagera, Hajjat Fatma Mwassa amesema Kata ya Rukoma imekuwa mfano katika shughuli mbalimbali za maendeleo kupitia Mwenyekiti Ngeze, ambaye amekuwa chachu ya kusimamia miradi inatekelezwa kwenye halmashauri hiyo yenye vijiji 94 kata 29.

Baadhi ya Viongozi wa dini waliongoza dua hiyo ni pamoja na Mchungaji Mathias Buberwa wa Kanisa la KKKT Dayosisi Kaskazini Magharibi, Padre Achileus Rugemalia wa Poroko Ichwandimi pamoja na Sheikh Twahir Said wa Wilaya Bukoba.

Kwa pamoja wameliombea Taifa la Tanzania liendelee kuwa na amani umoja na mshikamano, ili viongozi wake wajaliwe rehema na busara katika kutekeleza majukumu yao kuanzia vitongoji hadi taifa na kuliepusha na migogoro mbalimbali.


By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post