NHC YAAGIZWA KUTOA GAWIO LA BILIONI 10 KWA SERIKALI |Shamteeblog.

 


 ****

Na Mwandishi wetu 

Msajili wa Hazina, Nehemiah Mchechu, amelitaka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuweka lengo la kutoa gawio serikalini la bilioni 10 kwa mwaka Ujao wa fedha. 

Kauli hiyo ameitoa katika kikao cha baraza la wafanyakazi wa NHC kilichofanyika mkoani Pwani mapema leo.

Akizungumza katika kikao hicho, Mchechu awakumbusha wafanyakazi wa NHC kuwa umoja, upendo, na mshikamano katika utendaji wao wa kazi ni muhimu kwa maendeleo ya taasisi hiyo. 

Amesema kuwa, bila kushirikiana, taasisi hiyo itakuwa ngumu kufikia malengo yake ya kiuchumi.

"Miradi inayotekelezwa na NHC katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mtwara, Lindi, na Iringa inakaribia kukamilika, na italeta manufaa makubwa kwa taifa. Hivyo, ni muhimu wafanyakazi wa NHC kufanya kazi kwa bidii, kwa uwajibikaji na kwa umoja ili kufanikisha malengo haya," amesema Mchechu.

Mchechu ameongeza kuwa, wafanyakazi wa NHC wanapaswa kutokuwepo na majivuno na kutokuwa na utovu wa nidhamu katika kazi. 

Amesema kuwa maisha ni mafupi, na hivyo ni vyema wafanyakazi wa NHC kupendana na kufanya kazi kwa kujituma ili taasisi iweze kufikia malengo yake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Ahmad Abdallah, amewakumbusha wafanyakazi kuhusu umuhimu wa kufanya kazi kwa uwadilifu na katika muda uliotakiwa. 

Amesisitiza kuwa, ili taasisi iweze kufikia malengo ya kifedha yaliyowekwa, kila mfanyakazi anapaswa kuchangia kwa kiwango cha juu.

NHC imejipanga kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa nyumba na miundombinu katika mikoa mbalimbali, na Mchechu amesema kuwa, kama miradi hii itafanikiwa, itachangia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya kiuchumi ya taifa.










By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post