TUMIENI VYAKULA VYA ASILI ILI KUDHIBITI UDUMAVU |Shamteeblog.



Na mwandishi wetu Muleba

Wadau wa lishe Wilayani Muleba Mkoani Kagera wametakiwa kushirikiana na Serikali kuhamasisha wananchi kula vyakula vya asili ambavyo vipo kwenye maeneo yao ili kuweza kudhibiti udumavu dhidi ya watoto katika Wilaya hiyo.

Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Bi. Edina Kabyazi ametoa  kauli hiyo  kwenye kikao cha kamati jumuishi ya lishe ngazi ya Wilaya cha robo ya pili ya Oktoba hadi Desemba mwaka 2024/2025 ambacho kimefanyika Februari 25, 2025  katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muleba.

Bi. Edna Kabyazi amesema kuwa jukumu la uhamasishaji wa ulaji wa vyakula vyenye lishe sio la Watalaam wa afya pekee bali ni jukumu la kila mdau wa maendeleo kwani panahitajika nguvu ya ziada na kutokata tamaa lengo likiwa ni kuhakikisha kila kaya inakuwa na lishe bora.

Awali akiwasilisha taarifa ya lishe Afisa lishe Wilaya ya Muleba Dkt. Robson Tigererwa amesema kuwa wameweza kufanya kampeni ya ugawaji wa matone ya vitamin A na dawa za minyoo ambapo walilenga kuwapatia watoto 119,737 na wameweza kuwapatia watoto 119,440 sawa na asilimia 99.

Dkt. Tigererwa amesema kuwa pia pamefanyika upimaji wa hali ya lishe kwa watoto 53,881 wenye umri wa miezi sita hadi 59 ambapo watoto wenye hali nzuri ya lishe ni 50,649 sawa na asilimia 94, wenye hali hafifu ya lishe ni 3,017 sawa na asilimia 5.6 huku watoto wenye hali mbaya ya lishe wakiwa ni 216 sawa na asilimia 0.4.

Aidha amesema kuwa bado kuna changamoto ya baadhi ya wazazi kugoma kuwapeleka watoto kwenye zoezi la chakula dawa pamoja na ushiriki mdogo wa wanaume kwenye masuala ya lishe hasa kwenye mafunzo na mikutano.

Nao baadhi ya washiriki ambao ni Johanes Mtoka na Gaudini Gration wameshauri kuwepo kwa mashamba darasa kwenye shule za msingi na Sekondari ili kuondoa changamto ya  wa uhaba wa chakula shuleni ambao umekuwa ukipelekea baadhi ya wanafunzi kuwa na udumavu kutokana na kushinda njaa siku nzima.






By Mpekuzi

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post