Waandishi wa habari wametakiwa kuendelea kuwaelimisha wanawake kuhusu umuhimu wa kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi ili kuleta mabadiliko chanya katika jamii.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Tanzania upande wa Zanzibar TAMWA-ZNZ, Dkt. Mzuri Issa, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Redio Duniani yaliyofanyika huko Tunguu.
Dkt. Mzuri amesema kuwa licha ya waandishi wa habari kufanya kazi kubwa ya kuelezea changamoto zinazowakumba wanawake kwenye kuwania nafasi za uongozi pamona na kueleza umuhimu wa kuwa na uwiano sawa katika nafasi za uongozi, bado kuna kazi ya ziada ya kuwaelimisha wanawake ili waongeze ujasiri wa kujitokeza kugombea nafasi za uongozi katika vyama vya siasa.
"Wanawake wengi wana uwezo wa kuongoza, lakini tatizo kubwa ni ukosefu wa kujiamini. Hili ni jambo ambalo waandishi wa habari wanapaswa kulifanyia kazi kwa kuandaa vipindi vinavyoelimisha na kuwahamasisha wanawake," alisema Dkt. Mzuri.
Ameongeza kuwa redio zimekuwa zikiifanya kazi kubwa katika kutangaza mambo yanayohusu jamii, hivyo waandishi wanapaswa kuendelea kuandaa vipindi vyenye tija vinavyohamasisha ushiriki wa wanawake katika siasa na uongozi.
Aidha, akizungumzia kaulimbiu ya Siku ya Redio Duniani kwa mwaka huu inayosema “Redio na Mabadiliko ya Tabianchi”, Dkt. Mzuri amebainiaha kuwa vyombo vya habari vina jukumu muhimu katika kuelimisha jamii kuhusu athari za uharibifu wa mazingira na jinsi ya kupambana na ongezeko la joto duniani.
Kwa upande wao, waandishi wa habari waliohudhuria maadhimisho hayo wamesema kuwa redio nyingi kwa sasa zimejikita zaidi kwenye masuala ya kibiashara badala ya kutoa maudhui yanayolenga maendeleo ya jamii.
Wameeleza kuwa baadhi ya vipindi vya redio vimegeuka kuwa sehemu za ushabiki, hasa kwenye michezo, ambapo mijadala mingi inajikita kwenye timu za Simba na Yanga badala ya kuzungumzia changamoto za msingi zinazoikumba jamii.
Waandishi hao wamependekeza kuwa redio zirudi kwenye misingi yake ya awali kwa kuhakikisha zinatoa vipindi vinavyolenga maendeleo ya jamii, hususan katika kuwawezesha wanawake kushiriki kikamilifu katika siasa na uongozi.
Waandishi wa habari wana jukumu kubwa la kuwaelimisha na kuwahamasisha wanawake kujitokeza kugombea nafasi za uongozi. Kupitia redio, wanawake wanaweza kupata taarifa sahihi na motisha ya kushiriki katika siasa, hatimaye kuchangia maendeleo ya jamii kwa ujumla.
By Mpekuzi
Post a Comment