
Na Lydia Lugakila - Kyerwa
VYAMA vya ushirika vya Mkombozi na juhudi (AMCOS) vilivyopo Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera vimeiomba Serikali kuweka mkakati wa kuzuia uvunaji Kahawa mbichi ili kulinda zao hilo sokoni.
Meneja wa Mkombozi AMCOS Alphonce Vedasto alisema kuwa kuna changamoto katika uvunaji Kahawa na namna ya kutunza Kahawa ambapo kwa msimu huu uliomalizika kumekuwa na changamoto kubwa sana kwani Kahawa iliyopokelewa ilivunwa ikiwa mbichi ambapo ameiomba Serikali Wilayani humo kuweka mikakati ya pamoja ili kukomesha uvunaji Kahawa mbichi.
"Kahawa ikiwa mbichi inanunuliwa kwa bei ya chini sana na Kahawa ikifikishwa kule bila ubora inaharibu masoko yetu, tunajua mikakati ya Serikali ni mizuri hivyo wakulima wahimizwe kwenda sokoni wakiwa na Kahawa safi"alisema Vedasto.
Vedasto aliongeza kuwa wao kama Mkombozi wanaendelea kuwaelimisha Wanachama wake kuhakikisha wanavuna Kahawa iliyo iva na kuhakikisha pia wanaitunza vizuri mpaka inaenda sokoni.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Juhudi AMCOS Donath Bishanga Emmanuel alisema wataalamu wapo wanapima na kufundisha Wakulima namna ya uvunaji na utunzaji Kahawa hivyo wao kama ushirika watahakikisha msimu huu ujao wa Mwaka 2025 Kahawa itakuwa safi.
"Kahawa ikivunwa ikiwa nzuri na sisi tupo tayari kutafuta fedha na tukaikusanya kuanzia msimu utakapofunguliwa mwezi mei mwaka huu" alisema Mwenyekiti Juhudi AMCOS.
Akitoa ushauri katika suala hilo Mbunge wa Jimbo la Kyerwa Innocent Bilakwate alisema kuwa suala la uvunaji wa Kahawa mbichi sio la makampuni tu yanayonunua Kahawa bali ni la Halmashauri kuhakikisha wanadhibiti uvunaji Kahawa mbichi.
Bilakwate Aliwasisitiza maafisa kilimo kuendelea kutoa elimu ili Wananchi waache kuvuna Kahawa mbichi kwani ni kosa kisheria lakini pia ukosefu wa ubora.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa Bahati Henerico aliwataka viongozi wa Wilaya hiyo kutoa elimu kwa Wakulima kila mara juu ya changamoto hiyo.
"Kule tuna watendaji, Madiwani mpo mlinda Nchi ni Mwannanchi na nyiyi mkiweza kuweka mikakati kama walivyoweka huko kata ya Bugomora juu ya ukamataji wa wavunaji Kahawa mbichi mtawakamata tu wahusika "alisema Bahati Henerico.
Aliongeza kuwa mikutano ni muhimu kuwaelimisha wakulima ili watambue kuwa madhara ya kukamatwa ni makubwa kuliko walichokitarajia kukipata kupitia uharibifu huo bapo pia Aliwasisitiza viongozi wa kata kutoa elimu zaidi.
By Mpekuzi
Post a Comment