SERIKALI YAPONGEZWA KWA KUWAONDOLEA WANANCHI KERO YA MAJI SINAI NA MANG’ULA |Shamteeblog.


Mhandisi Vicent Bahemana (kulia) akiwa pamoja na Diwani wa kata ya Lilambo Exsaveri Iyobo wakati wa kukabidhi mabomba ya mradi wa maji Sinai na Mang’ula katika Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma
Mhandisi Vicent Bahemana kutoka kulia akizungumza na Mheshimiwa Diwani wa kata ya Lilambo Exsaveri Iyobo baada ya kukabidhi mabomba ya mradi wa maji Sinai na Mang’ula
Gari likiendelea na zoezi la kushusha mizigo ya mabomba Sinai kata ya Lilambo Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma
Mhandisi Vicent Bahemana akizungumza na wananchi baada ya kukabidhi mabomba ya mradi wa maji katika mtaa wa Sinai na Mang’ula Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma
Wananchi wa mtaa wa Sinai na Mang’ula Kata ya Lilambo waliojitokeza kupokea mabomba ya mradi wa maji kutoka mamlaka ya maji safi na salama SOUWASA Manispaa ya Songea Mkoani Ruvuma
Na Regina Ndumbaro - Songea. 

Wananchi wa mtaa wa Sinai na Mang’ula Manispaa ya Songea, mkoani Ruvuma, wameipongeza Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa juhudi kubwa za kuleta maendeleo, hususan katika sekta ya maji. 

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wananchi hao akiwemo Winfrida Gama na Renatus Sevelini wamesema wamekuwa wakikosa huduma ya maji kwa muda mrefu, hususan mashuleni, lakini sasa wanashuhudia mabadiliko makubwa na kuondokana na adha ya kubeba ndoo kichwani kwenda kutafuta maji mbali na makazi yao.

Kwa upande wake, Mhandisi Vincent Bahemana kutoka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Vijijini na Mijini (SOUWASA) amesema kuwa utekelezaji wa mradi wa maji katika maeneo hayo umegharimu shilingi bilioni 1.5. 

Mradi huo unahusisha ulazaji wa mabomba kwa umbali wa kilomita 44.9, uchimbaji wa visima vya maji pamoja na ujenzi wa tanki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 200,000 za maji ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma endelevu.

Mhandisi Bahemana ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu ya mradi huo, amewasisitiza kuwa mafanikio ya mradi huo yanahitaji ushirikiano mzuri kati ya jamii na mafundi. 

Aidha, amewataka wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa mafundi wanaotekeleza mradi huo ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa ufanisi mkubwa.

Diwani wa Kata ya Lilambo, Mhe. Exsaveri Iyobo, ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) pamoja na Mbunge wa Jimbo la Songea Mjini, Mhe. Damas Ndumbaro, kwa kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi. 

Amesema hapo awali wananchi walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata maji, lakini sasa wanapata huduma hiyo karibu na makazi yao, jambo ambalo limeleta faraja kubwa.

Wananchi wa mitaa ya Sinai na Mang’ula sasa wanafurahia matokeo ya juhudi za Serikali katika kuwapelekea huduma muhimu. 

Wametoa wito kwa wenzao kuendelea kulinda miundombinu hiyo kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo, huku wakisisitiza kuwa maendeleo yanapokuja, ni jukumu la kila mmoja kuyatunza.


By Mpekuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post