MRAJIS ATAKA VYAMA VYA USHIRIKA VISIMAMIE WAJIBU WAO, AONYA KUHUSU “MAGOMA ” NA UBADHIRIFU |Shamteeblog.

Meneja wa Mbifacu (Mbinga Farmers  Co-operative Union Ltd)Faraja Komba akimkaribisha mgeni rasmi mrajisi Msaidizi Mkoa wa Ruvuma Peja Muhoja katika Mafunzo ya wenyekiti na watendaji wa vyama vya ushirika vilivyopo chini ya mwamvuli wa Mbifacu

Wenyekiti na watendaji wakimsikiliza mgeni rasmi Mrajisi Msaidizi Mkoa Peja Muhoja pichani hayupo

Na Regina Ndumbaro Mbinga, Ruvuma 

Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Ruvuma, Peja Muhoja, ametoa wito mzito kwa viongozi na watendaji wa vyama vya ushirika chini ya mwamvuli wa Mbifacu kuhakikisha wanasimamia wajibu wao ipasavyo, wakiepuka uzembe, migogoro, na vitendo vya kuhujumu uchumi wa wakulima. 

Akizungumza katika mafunzo ya wenyekiti na watendaji wa vyama vya ushirika yaliyofanyika katika ukumbi wa Mbicu Hotel Wilayani Mbinga, Muhoja amesisitiza umuhimu wa ubora wa kahawa, uwajibikaji wa viongozi, na usimamizi madhubuti wa mikataba.

Muhoja ameeleza kuwa baadhi ya vyama vitano vimekuwa na changamoto kubwa, ikiwa ni pamoja na kutokuwa na mikataba rasmi, kutowalipa wakulima, na viongozi kutotekeleza majukumu yao ipasavyo. 

Amesema mikataba imegeuzwa kuwa kichaka cha kuweka bei zisizo rasmi kwa manufaa binafsi. 

Ameonya kuwa mwaka huu, mikataba isiyopitishwa na chama cha Mbifacu haitatambuliwa, na akaagiza viongozi wa vyama vyote wakutane na wakurugenzi wa halmashauri, maafisa kilimo na biashara kwa ajili ya uthibitisho rasmi wa mikataba hiyo.

Katika hotuba yake, Muhoja amekemea vikali matumizi ya kile alichokiita “magoma” – watu wanaotumiwa kuhujumu mfumo wa ushirika kwa manufaa ya wachache. 

“Kwa nini mtumike kama magoma? Mnagawana hela za wakulima, huu ni uhujumu uchumi wa wananchi,” amesisitiza. 

Amesema hatua kali zitachukuliwa dhidi ya viongozi wanaoendekeza tabia hizo, na kwamba kila chama kinapaswa kuwa na nidhamu, kuelewa wajibu wake, na kuhakikisha fedha za wanachama zinawekwa kwenye benki ya ushirika kama alivyoagiza Waziri.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwasilisha taarifa za utendaji kwa wakati, kukamilisha miongozo, kutumia mfumo wa kidigitali (online) na kuzingatia mpango mkakati wa vyama. 

Pia amewataka usajili wa wakulima kufanyika kikamilifu ili kupunguza malalamiko ya kiholela. 

 Amewaasa viongozi kujifunza kutoka kwa viongozi wakuu wa nchi katika kuonyesha uwajibikaji, nidhamu na uadilifu katika utendaji kazi wa kila siku.



By Mpekuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post