
Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mtwara Mkoani Mtwara Mhandisi Hamis Mashindike aliyeshika fimbo,akimuonyesha Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi miundombinu ya mradi wa maji Dihimba uliofanyiwa ukarabati mkubwa ili kuboresha hduma ya majisafi na salama kwa Wananchi wa Vijiji vinne vya Dihimba,Mpondomo, Kinyamu na Ndumbwe.

Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa Mwaka 2025 Ismail Ali Ussi,akiangalia kisima cha maji katika kilichofanyiwa ukarabati mkubwa kwa ajili ya kuboresha huduma ya maji kwa Wananchi wa Vijiji vya Ndumbwe,Dihimba,Mpondomo na Kinyamu Wilayani Mtwara,kushoto Meneja wa Ruwasa Wilaya ya Mtwara Hamis Mashindike na kulia Mkuu wa Wilaya

Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mtwara Hamis Mashindike aliyeshika fimbo akitoa maelekezo kwa kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa Ismail Ali Ussi wakati alipokwenda kukagua kisima cha maji kilichokarabatiwa na kuboreshwa kwaajili ya huduma ya wananchi wa vijiji vinne wilayani humo
Na Regina Ndumbaro-Mtwara
Serikali kupitia Wizara ya Maji imetoa Shilingi 815,453,185 kwa ajili ya kukarabati Mradi wa Maji wa Dihimba unaohudumia wakazi zaidi ya 7,489 katika vijiji vya Dihimba, Mpondomo, Kinyamu na Ndumbwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara.
Mradi huu ni hatua muhimu katika kuboresha huduma ya majisafi na salama kwa wananchi waliokuwa wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa maji kwa muda mrefu.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mtwara, Mhandisi Hamis Mashindike, amesema kuwa kati ya fedha hizo, Shilingi 694,271,895 zilitumika kumlipa mkandarasi na Shilingi 121,181,200 zilinunulia mabomba kupitia RUWASA Makao Makuu.
Ukarabati huo ulianza Januari 2024 na unatarajiwa kukamilika Juni 2025 baada ya kuchelewa kutokana na changamoto kama mvua nyingi na ucheleweshaji wa malipo.
Mradi huu unatekelezwa na wakandarasi M/S Zonghi Plumbing & General Supplies na M/S Seba Construction, ambapo hadi sasa umekamilika kwa asilimia 75.
Kazi zilizofanyika ni pamoja na ujenzi wa tenki la lita 100,000 katika kijiji cha Mpondomo, ukarabati wa matenki mawili ya lita 200,000 katika Ndumbwe, ujenzi wa vituo 17 vya kuchotea maji, nyumba ya muhudumu, ofisi ya Jumuiya ya Watumia Maji (CBWSO), pamoja na ulazaji wa bomba wa zaidi ya kilometa 24.
Utekelezaji wa mradi umeongeza upatikanaji wa huduma ya maji kutoka asilimia 37.04 hadi 93.47 kwa mwaka 2025.
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2025, Ismail Ali Ussi, alipata fursa ya kutembelea na kukagua miundombinu ya mradi huo huku akielezwa mafanikio yaliyopatikana.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Patrick Sawala, ameeleza kuwa mradi huo ulioanzishwa mwaka 1989 haujawahi kufanyiwa ukarabati mkubwa na sasa umeleta ahueni kubwa kwa wananchi, ambao awali walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata maji.
Mwananchi wa Kijiji cha Dihimba, Mwanahawa Rashid, ameeleza kuwa kabla ya ukarabati huo walilazimika kutembea hadi vijiji vya jirani kwa ajili ya maji.
Ameishukuru serikali ya awamu ya sita kwa kusikiliza kilio cha wananchi na RUWASA kwa usimamizi mzuri wa mradi huo ambao sasa umewapunguzia adha kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama.
By Mpekuzi
Post a Comment