WANANCHI 1,640 WAPATIWA ELIMU YA KUJIKINGA NA WANYAMA WAKALI NA WAHARIBIFU |Shamteeblog.



Na Dotto Kwilasa,Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna ya kujikinga na wanyama wakali na waharibifu, ambapo jumla ya wananchi 1,640 kutoka vijiji vya Engikaret na Kiserian, Wilaya ya Longido mkoani Arusha, wamefikiwa kati ya Julai 2024 hadi Aprili 2025.

Hayo yameelezwa leo Mei 23, 2025 Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dunstan Kitandula, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Mhe. Zaytun Seif Swai, kuhusu mikakati ya Serikali katika kukabiliana na uvamizi wa tembo katika Kata ya Engikaret.

Akifafanua, Mhe. Kitandula amesema kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kudhibiti changamoto hiyo ikiwa ni pamoja na kufanya doria za mwitikio wa haraka. Amesema kuwa kati ya Julai 2024 na Machi 2025, jumla ya doria 34 zimefanyika katika Kata ya Engikaret kwa lengo la kukabiliana na matukio ya wanyamapori wakali.

Aidha, Naibu Waziri huyo amebainisha kuwa Serikali ilianzisha kituo maalum cha askari mwaka 2021 katika Wilaya ya Longido ili kuimarisha ulinzi dhidi ya wanyamapori hao. Kituo hicho kina jumla ya askari 18 wakiwemo wahifadhi 8 na askari wa wanyamapori wa vijiji (VGS) 10. 

Vituo hivyo vimewezeshwa kwa vitendea kazi ikiwemo gari moja na pikipiki nne ili kufanikisha shughuli za ulinzi.

Katika hatua nyingine, Kitandula amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wananchi kwa kuwajengea uelewa juu ya namna bora ya kuripoti matukio ya wanyama wakali kwa wakati, ili hatua za haraka zichukuliwe. Amesisitiza kuwa elimu hiyo inatolewa kwa njia ya mikutano ya hadhara, vipeperushi, na kupitia vyombo vya habari vya jamii.

Vilevile, Serikali inaendelea na jitihada za kuongeza idadi ya askari wa wanyamapori na kuwawezesha vifaa vya kisasa zaidi ili kuongeza ufanisi wa operesheni za kuwalinda wananchi, mali zao pamoja na uhifadhi endelevu wa wanyamapori nchini.


By Mpekuzi

Post a Comment

Previous Post Next Post